RC ahimiza uadilifu kutimiza wajibu

VIONGOZI na watumishi wa umma mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuwa waadilifu na waaminifu wakati wanapotekeleza majukumu yao kwa wananchi. Rai hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu wakati akizindua baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Tunduru.

Aliwaeleza madiwani na watendaji wa halmashauri kuwa tatizo la ukosefu wa uadilifu na uaminifu miongoni mwao limesababisha upotevu mkubwa wa mapato ya halmashauri na utoaji mbovu wa huduma kwa wananchi.

Mwambungu aliwataka watumishi wa halmashauri kudhamiria kwa dhati kuwahudumia wananchi wakizingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

“Uadilifu na uaminifu hakuna chuo chochote kinachofundisha bali ni kwa watumishi wote kujipima na kuheshimu sheria za utumishi zilizopo na kuepuka rushwa inayosababisha kuzorota kwa huduma kwa wananchi,” alisema Mwambungu.

Amewaasa pia watumishi wa halmashauri kutambua kuwa si wakubwa wa wananchi, bali ni wananchi hivyo wawe mfano wa kuigwa kwa ubora wa utoaji huduma zinazochangia maendeleo bila upendeleo. Mwambungu alisema watumishi wa serikali hawana budi kuchukia rushwa na ufisadi ili Tunduru na Ruvuma kwa ujumla ipate maendeleo.

Alisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano ikijiridhisha dhidi ya mashaka kuwa mtumishi anajihusha na rushwa haitosita kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ya kuleta maendeleo bora kwa kuhimiza kila mtu kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kwa kasi kubwa.

Katika hatua nyingine, madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru wamemchagua Mbwana Sudi, ambaye ni diwani wa kata ya Mchoteka (CCM) kuwa mwenyekiti mpya wa halmashauri hiyo.