23Mei2013

 

Zanzibar haina daktari bingwa wa akili

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haina daktari mzalendo bingwa wa kutibu maradhi ya ugonjwa wa akili kwa sasa.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Sira Ubwa Mamboya alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Mohamed Said (CCM) aliyetaka kufahamu idadi ya madaktari bingwa wenye uwezo wa kutibu maradhi ya akili kwa sasa.

Dk Sira alisema katika Wizara ya Afya wapo madaktari bingwa wawili wanaotibu maradhi ya akili ambao wote ni raia wa kigeni kutoka Cuba.

“Ni kweli Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa inakabiliwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa madaktari bingwa wa kutibu magonjwa ya akili katika hospitali za Unguja na Pemba,” alisema.

Naibu Waziri alizitaja baadhi ya sababu za kuwapo kwa upungufu mkubwa wa madaktari katika kada ya kutibu maradhi ya akili ikiwamo vijana kugoma kusomea fani hiyo.

Alisema Wizara ya Afya kwa sasa imeanza kushajihisha vijana mbalimbali wanaomaliza masomo ya juu kwenda kusomea kada ya masomo ya kutibu ugonjwa wa akili.

“Tumeanza kushajihisha vijana wanaomaliza masomo ya elimu ya juu kwenda kusomea kada ya magonjwa ya akili...tunakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa masomo hayo,” alisema.

Dk Sira alisema yupo daktari bingwa mmoja tu mzalendo kwa sasa ambaye amestaafu kazi na anakwenda katika hospitali za Serikali kwa kujitolea tu.

Hata hivyo, alisema dunia inakabiliwa na tatizo la upungufu wa madaktari bingwa kutibu maradhi hayo ambapo kwa sasa daktari mmoja anatibu wagonjwa 200,000 duniani kote.