Kutongoza kwamsababishia kifo

WATU wawili wamejeruhiwa na mmoja wao kupoteza maisha katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Katavi hivi karibuni. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahri Kidavashari akizungumza na gazeti hili alisema katika tukio la kwanza mkazi wa kijiji cha Kalovya – Inyonga wilayani Mlele, Ramadhani Ally (20) amefariki dunia akipatiwa matibabu hospitalini.

Akifafanua Kidavashari alisema kuwa Ramadhani alifikwa na umauti baada ya kujeruhiwa na kijana mwenzake Ntema Kabembenya( 26), mkazi wa kijiji cha Ipwaga. Akisimulia tukio hilo, Kidavashari alidai kuwa lilitokea Januari 22, mwaka huu saa 12:55 jioni ambapo Ntema alimkuta Ramadhani (marehemu) akimtongoza dada yake (Ntemwa) mwenye umri wa miaka 12 (jina limehifadhiwa).

“Ntemwa alikasirishwa na kitendo cha Ramadhani kumtongoza dada yake mwenye umri wa miaka 12, alimshambulia Ramadhani kwa kumpiga na fimbo na kumjeruhi vibaya,” alieleza Kamanda Kidavashari.

Inadaiwa Ramadhani alikimbizwa katika Hospitali ya wilaya ya Mlele kwa matibabu lakini alifariki dunia siku iliyofuata akiwa anatibiwa. Kwa mujibu wa Kidavashari, mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi ambapo anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili.

Katika tukio lingine lilotokea Januari 24, mwaka huu saa 1:00 usiku ambapo mkazi wa kitongoji cha Mzabwela kijijini Mchangani wilayani Mpanda, Elia Edward (40) alichomwa tumboni na kitu chenye ncha kali na kusababisha utumbo wake kutoka nje.

Kamanda Kidavasshi akithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtu aliyefanya uhalifu huo bado hajafahamika. “Mara baada ya mtuhumiwa kutenda kosa hilo alikimbia kusikojulikana. Aidha majeruhi amepelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mpanda kwa matibabu zaidi” alisema.