‘Wakulima fikeni maonesho ya Nanenane’

WAKULIMA wa Kanda ya Mashariki, wameshauriwa kufika kwenye maonesho ya wakulima Nanenane yaliyotarajiwa kumalizika jana katika Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ili kupata elimu ya kilimo.

Rai hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alipotembelea maonesho hayo ambapo alisema mwaka huu yamekuwa ya tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma, kutokana na kukua kwa teknolojia.

Aliwataka wananchi watakaotembelea maonesho hayo, kujikita katika kupata mafunzo yatakayowasaidia waepukane na matumizi ya dawa ambazo hazina maana kwenye mazao yao.

Mwanga aliwataka wakulima walioko katika kanda hiyo, kuitumia fursa hiyo kujijengea uwezo utakaowawezesha kulima mazao yenye tija kwao na kwa Taifa.

Alishauri Chama cha Wakulima (TASO), Kanda ya Mashariki, kushirikisha wadau mbalimbali walioko katoka viwanja hivyo, ili kusaidia kuchangia kwa kutoa kitu chochote walichonacho, ili kuboresha zawadi za wakulima.