JICHO LANGU: Usikose zawadi hii nono kwa mtoto

NIKIWA katika hospitali moja binafsi ya jijini Dar es Salaam, alifika mama mmoja aliyekuwa amechanganyikiwa kutokana na hali ya afya ya mtoto wake.

Akiwa amembeba mtoto wake mikononi, alikwenda mapokezi ya hospitali hiyo kubwa na maarufu kuomba msaada wa haraka wa matibabu kwa mtoto huyo ambaye alikuwa katika hali mbaya. Kutokana na namna mtoto alivyokuwa amelegea, alihitaji huduma ya haraka sana kuokoa maisha yake, lakini tofauti na mategemeo ya wazazi na hata watu waliokuwa hospitalini hapo, mama huyo hakufanikisha hata kuandikisha cheti mapokezi.

Mhudumu wa mapokezi wa hospitali hiyo, hakuwa na njia ya kumsaidia kwa kuwa mama huyo hakuwa na fedha kuwezesha mchakato wa matibabu. Nakumbuka, kipindi hicho ndipo madaktari katika hospitali za serikali walikuwa wamegoma. Hospitali zote kubwa za Serikali ambazo mama huyo angeweza kwenda, ambazo ni Mwananyamala, Amana, Temeke na Muhimbili, hazikuwa na huduma kutoka na mgomo huo.

Masikini huyo mama katika kujaribu kuokoa maisha ya mtoto wake, akaona akimbilie hospitali hiyo binafsi akiamini angepata huruma na ahudumiwe haraka. Alikiri hakuwa na fedha yoyote ya kulipia matibabu ikiwemo kufungua jalada. Hivyo alitarajia huruma ya madaktari imwezeshe mtoto huyo aliyekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja, apone. Lakini kumbe mambo ni tofauti kwenye hospitali binafsi.

Maana wahudumu waliogopa kujifunga kitanzi. Ingawa wengi walimwonea huruma mtoto sanjari na mama yake, lakini hawakuwa na uamuzi wa moja kwa moja wa kumhudumia mtoto. Badala yake, walilazimika kufanya mawasiliano na wakubwa wao kama wamtibu au la. Sikufuatilia ni nini kiliendelea kwa kuwa mimi pia nilikuwa na mtoto niliyekuwa nimempeleka hospitalini. Hivyo sielewi kama ‘malaika’ huyo alipata matibabu na wala sifahamu hatma ya maisha yake.

Nimekumbuka kisa hiki cha takribani miaka minne iliyopita, baada ya kusikia taarifa za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulioanzisha huduma mpya ya Toto Afya Kadi. Huduma hiyo inalenga kuhudumia watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 . Watajiunga kwa gharama ya Sh 50,400 kwa mwaka na kupata huduma za matibabu kutoka kwenye kitita cha mfuko. Hapo ndipo nilikumbuka kwamba, laiti mama wa mtoto huyo angekuwa na kadi ya bima ya afya, asingekumbwa na wakati mgumu huo wa kukosa huduma katika hospitali binafsi.

Naipongeza sana NHIF kwa fursa hii kwa kuwa watoto ni kundi ambalo limekuwa katika wakati mgumu wa kukumbwa na magonjwa. Mfuko umewapa mazingira mazuri ya uhakika wa matibabu. Nategemea kila Mtanzania mwenye kuona mbali na ambaye hakuwa na fursa ya bima, hatakosa kuchangamkia huduma hii. Sina shaka hata mama wa mtoto huyo aliyekuwa hoi, ambaye mama yake alishindwa kumudu gharama kubwa za matatibu katika hospitali hiyo binafsi, akipata fursa ya kuelezwa juu ya mpango huu wa NHIF, hawezi kubisha kujiunga nao.

Nashauri NHIF ambayo imeanza uhamasishaji kwa watu kujiunga na kunufaika na huduma hiyo, iongeze nguvu kuhakikisha umma wa Watanzania unaelewa huduma hii. Waelimishaji wengine mitaani na wafikie makundi mbalimbali ya kijamii kuhakikisha fursa hii inachangamkiwa. Watumishi wa mfuko sanjari na wadau wanaoelimisha umuhimu wa kukata bima ya afya kwa mtoto, wawe tayari kufikisha ujumbe pia kupitia nyumba za ibada.

Lakini pia kwenye sherehe mbalimbali kama vile ‘kitchen party’ ambazo hukusanya wanawake, kwenye vikundi vya Vicoba na Saccos, pia vitumiwe kuwasilisha ujumbe. Vilevile maeneo ya kazi, biashara na mikusanyiko mingine ikiwemo, mikutano ya hadhara, itumike ipasavyo kuwasilisha ujumbe huu ili watu wote wachangamkie bima hii ya watoto. Kwa ujumla, kiasi ambacho mfuko umepitisha kwa ajili ya kujiunga na huduma ni kidogo ikilinganishwa na gharama ambazo mtu huingia kutokana na ugonjwa. Ugonjwa hauchagui gharama.

Hauangalii uwezo wa kifedha. Hauangalii aina ya shughuli afanyazo mtu. Bali unaweza kumpata mtu yeyote, wakati wowote na mahali popote. Kwa muktadha huo, Sh 50,400 si chochote si lolote pale ambapo ndani ya nyumba kutaingia ugonjwa wa aina yoyote. Ikumbukwe, kadi inawezesha mhusika kwenda hospitali mbalimbali kubwa zikiwemo za watu binafsi. Wapo wanaoweza kujenga hoja kuonesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa sana.

Lakini wakasahau linapokuja suala la kuchangia harusi, ngoma, kitchen party, kipaimara au ubatizo, wengi hujitoa hata kuzidi kiasi hicho kinachohitajika kwa Toto Afya Kadi. Imefika wakati, ule utamaduni wa kudhani wenye kadi za bima ya afya ni watu wa kundi fulani, uishe mara moja. Zawadi hii ya NHIF kwa watoto haina budi kupongezwa na kuenziwa. Huu ni mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya vifo vya watoto hususan wa chini ya umri wa miaka mitano. Hakika bima hii ni zawadi nono si tu kwa watoto, bali pia wazazi na walezi wote nchini . Hii ni mkombozi kwa jamii, tuichangamkie.

Twessige@yahoo. com