24Mei2013

 

Mbatia aanika uozo katika elimu

MBUNGE wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) ameweka wazi udhaifu ulioko katika sekta ya elimu nchini, ikiwemo kugubikwa kwa harufu ya ufisadi katika uchapishaji wa vitabu vya kiada na ziada.

Akiwasilisha hoja binafsi jana bungeni, Mbatia alisema mbali na udhaifu huo, pia kuna tatizo la kisera, mitaala na mihutasari, hali inayosababisha Taifa kuwa kwenye mgogoro mkubwa katika sekta ya elimu. 

Akizungumzia udhaifu katika vitabu vya kiada na ziada, aliliambia Bunge kwamba kitengo kinachotoa Ithibati kwa vitabu hivyo katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kimeshindwa kutekeleza wajibu wake na kusababisha vitabu kupotosha wanafunzi.

“Kwa mfano, sio tu kwamba vitabu vingi vya somo la Hisabati vilivyopewa Ithibati, vina makosa mengi ya kitaaluma, lakini hata mfumo wa uandaaji wa vitabu hivyo una harufu ya ufisadi,” alisema Mbatia.

Mbatia ambaye aliungwa mkono na wabunge wengi, kwamba sekta hiyo ina udhaifu mkubwa, alisema harufu ya ufisadi ipo katika mambo matatu ambayo ni mgongano wa kimaslahi; hasa watendaji wa Ithibati waliposhiriki kuandika vitabu walivyovipatia Ithibati.

Ufisadi mwingine ni kwenye utayarishwaji wa andiko, ambao ulifanyika nchini Malaysia na upigaji chapa ukafanyika nchini Kenya; Kazi alizosema zinaweza kufanyika hapa nchini kwa maslahi ya Taifa letu.

Aidha vitabu viliandikwa kwa idadi ya waandishi isiyowiana, kwa maana kwamba Wamarekani walikuwa 10 na Watanzania wanne.

“Pia lugha iliyotumika katika matoleo yote manne siyo sahihi. Kiingereza kisicho sahihi jambo ambalo linapotosha wanafunzi na kuwafanya wasielewe mada au maudhui yaliyokusudiwa.

“Hii ni mifano michache tu inayothibitisha mgogoro mkubwa uliopo katika sekta ya elimu hapa nchini,” alisema. Kwa upande wa udhaifu katika Sera, alisema Sera ya Elimu ya Taifa inayotumika imekuwapo kwa muda mrefu, hali inayohitaji ifanyiwe tathmini kubwa ili iendane na mahitaji ya sasa.

Alisema masuala mengi ya kisera katika elimu yanayofuatwa nchini, yametokana na masharti au maelekezo yaliyotolewa na vyombo vya kimataifa kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Mbatia alisema maelekezo ya vyombo hivyo badala ya kusaidia kuinua ubora wa elimu, yameleta matokeo yasiyokuwa mazuri na yanayumbisha.

“Mathalani miaka ya themanini vyombo hivi vilitutaka tupunguze matumizi ya rasilimali za umma katika kugharimia huduma za jamii ikiwemo elimu, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa uduni wa shule za umma nchini,” alisema.

Kuhusu tatizo la mitaala, Mbatia alisema hadi mwaka 2011 nchi haikuwahi kuwa na mitaala rasmi ya kitaifa kwa ajili ya elimu ya shule za msingi au sekondari. Alisema pamoja na kuwepo malalamiko kuwa mitaala ni mibovu, ukweli ni kwamba mitaala hiyo haikuwepo.

Alisema nchi haijawahi kuwa na andiko mahususi la mitaala ya elimu kwa Taifa. “Kwa mantiki hiyo kwa miaka mingi tumekuwa na chombo ‘mfumo wa elimu’ lakini kisicho na usukani," alisema na kuongeza kwamba Taasisi ya Elimu imekuwa ikiajiri wakuza mitaala kwa zaidi ya miaka 15 bila ya kutoa mitaala yoyote katika namna ya andiko mahususi.

Kamati teule Mbatia alipendekeza iundwe kamati teule, kuchunguza udhaifu katika sekta hiyo, lakini pendekezo lake hilo lilizua malumbano baina ya wabunge baada ya Serikali kutaka isiundwe.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipewa nafasi akatoa ufafanuzi, ambapo alisema tangu nchi ipate Uhuru, mitaala imebadilika mara nne na kutaja miaka ya mabadiliko ni 1967, 1979, 1997 na ya mwaka 2004-2009.

“Ingawa mitaala imebadilika mara nne tu, wadau wengi wamejenga hisia kuwa imebadilika mara kwa mara kwa sababu ya kuchanganya dhana ya mtaala na muhtasari,” alisema Kawambwa.

Pamoja na ufafanuzi wa mambo mengine, Dk Kawambwa alikubaliana na ukweli kwamba yapo mambo yanahitaji kufanyiwa kazi.

Aliomba Bunge, libadilishe maneno katika hoja ya Mbatia, badala ya kusema iundwe kamati teule, hoja iwe kwamba Bunge litake Serikali kuzingatia hoja zilizotolewa kwenye hoja ya Mbatia na kuzifanyia kazi kwa kina, wakati ikikamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo.

Spika Anne Makinda alisema Kanuni ya 57 inaruhusu kufanya mabadiliko katika hoja na kutaka wabunge wachangie ;na kama hoja ya Serikali itakataliwa, waendelee na ya msingi.

Uamuzi huo uliibua mvutano baina ya wabunge, hasa wa chama tawala waliounga mkono mapendekezo ya Serikali na wa upinzani walioyapinga wakisema ni ukiukwaji wa kanuni. Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu (Chadema) alitaka kupata ufafanuzi wa kiti cha Spika, kama hoja ya Serikali ya mabadiliko ni halali, akajibiwa kwamba hakuna kosa.

Hata hivyo, Lisu alipinga kwa kusema hoja ya Waziri huyo, ilitakiwa iwiane na ya msingi ambayo ni kuunda kamati teule. Spika alijitetea kwamba hakuvunja kanuni na kusisitiza kwamba uamuzi wa kumpa nafasi Waziri kujibu hoja ni sahihi.

Baadaye, Spika alihoji Bunge, ambapo wabunge walipitisha mabadiliko hayo na kuzuia hoja ya kuundwa kwa kamati teule.