Mbunge- Tundu Lissu mgonjwa wangu
- Imeandikwa tarehe 05 Februari 2013
- By Magnus Mahenge, Dodoma
- Imesomwa mara: 5081
BUNGE limegeuka uwanja wa malumbano wakati Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangala (CCM) alipomrushia maneno makali bila kumung’unya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kwamba ni mgonjwa wake.
Malumbano hayo yaliibuka bungeni jana wakati Dk Kigwangala akihitimisha hoja binafsi ya kuanzisha mpango maalumu wa kukuza ajira kwa vijana kwa kuanzisha mfuko wa mikopo wanaowekeza kwenye kilimo na viwanda vyenye uhusiano na kilimo.
Dk Kigwangala alisema kuwa Mbunge Lissu wakati akichangia Ijumaa iliyopita, aliiponda hoja hiyo ya kuanzisha benki ya vijana kuwa haina fikra wala tafakuri za kutosha na ililetwa bungeni hapo kwa lengo la ‘kutongozea’ wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa 2015.
Mbunge Kigwangala alipopewa saa moja ya kuhitimisha hoja yake, ilikatishwa zaidi ya mara tano, ambapo alitumia muda mwingi kumshambulia Mbunge Lissu kwamba alidharau hoja yake aliyoiwasilisha bungeni wiki iliyopita.
Kauli iliyochochea malumbano bungeni ilikuwa ya kwamba Mbunge Lissu alikuwa mgonjwa wa mtoa hoja wakati akiwa daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na yupo tayari kulieleza Bunge kama Mbunge huyo atabisha.
Kutokana na kauli hiyo, Mbunge Lissu aliomba mwongozo wa Spika na kusema Dk Kigwangala amesema uongo bungeni kwa kuwa hajawahi kuwa mgonjwa wake.
Akifafanua kuhusu vifungu hivyo, alisema kuwa mtoa hoja amelidanganya Bunge kwamba alikuwa mgonjwa wake wakati akiwa Muhimbili na kama hawezi kudhibitisha kauli hiyo basi afute usemi.
Alisema, mbunge amelidanganya Bunge kwamba alikuwa mgonjwa wake wakati yeye ndiye alikuwa Mwanasheria wao na akafanya kazi hiyo bila malipo wakati madaktari hao walipogoma hospitali hapo na kufukuzwa kazi mwaka 2006.
Kutokana na malumbano hayo kuendelea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisimama na kumtaka Mbunge Kigwangala kuacha kauli mbaya na kufuta kauli za kutaka kutamka bungeni kuhusu ugonjwa wa mbunge huyo.
Naibu Spika, Job Ndugai alimwamuru, Mbunge Kigwangala asithibitishe kauli hiyo badala yake afute maneno hayo, jambo ambalo alikubali.
Utaratibu wa kuchangia Naye Stella Nyemenohi, anaripoti kuwa Naibu Spika, Job Ndugai ametishia kuweka utaratibu wa wabunge kuchangia bungeni kwa kuzingatia uwiano wa vyama, ili kuondoa malalamiko kwamba kiti kinapendelea wabunge wa chama tawala. Ndugai alisema bungeni kwamba atakwenda kumshawishi Spika aanzishe utaratibu huo kwa kuzingatia malalamiko ya wabunge wa upinzani kwamba anapendelea CCM. Msingi wa kauli hiyo unatokana na mambo yaliyojiri wiki iliyopita bungeni; Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alipowasilisha hoja binafsi iliyozua malumbano baina ya Kiti cha Spika na baadhi ya wabunge akiwemo mtoa hoja.
Aliomba wabunge wanapokwenda kuandika kanuni zao za kudumu, uchangiaji kwa uwiano liingizwe ili kuondoa malalamiko husika.
Akizungumzia malalamiko kuhusu kutoruhusu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, kuwasilisha mezani kwake nakala ya mtaala, alisema kanuni inamruhusu ama kutoa mwongozo papo hapo au kuutoa baadaye kama alivyofanya.
Kuhusu wabunge kutoka nje ya ukumbi wiki iliyopita, Ndugai alisema wanachofanya, wanakuwa wamekwenda kunywa chai isipokuwa kama watatoka moja kwa moja nje ya viwanja vya Bunge.
“Waandishi mkiona mbunge yeyote au kikundi chochote kinatoka nje, mjue wanakwenda kunywa chai. Mbunge yeyote anaruhusiwa kutoka nje mmoja mmoja, kikundi,” alisema.


