Wakulima wa tumbaku watakiwa kutokata tamaa

WAKULIMA wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo wametakiwa kutokatishwa tamaa kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili zao hilo, badala yake kuongeza juhudi katika uzalishaji ili kuweza kuinua maisha yao.

Mwito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ali Mpenye alipokuwa akieleza mikakati mbalimbali ya kufufua zao hilo kwa waandishi wa habari ofisini kwake mjini Namtumbo.

Mpenye alisema kushuka kwa uzalishaji wa tumbaku wilayani humo katika miaka ya karibuni kumechangiwa sana na wakulima kukatishwa tamaa na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika walioshirikiana na kampuni zinazonunua tumbaku kuwaibia wakulima na wakati mwingine kuwabambikia madeni makubwa ya pembejeo.

Hata hivyo, aliishukuru serikali kuanza kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wote waliohusika kutafuna fedha za wakulima na wale walioua vyama vya ushirika ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walioshiriki kuua zao la tumbaku kwa kufanya vitendo visivyofaa dhidi ya wakulima.

Alisema vitendo hivyo vimechangia kuwakatisha tamaa wakulima wengi ambao walishakataa kulima tena zao hilo, lakini kutokana na hatua mzuri ya serikali kuanza kuwachukulia hatua wezi hao, baadhi wamekubali kuanza tena uzalishaji wa zao hilo lililokuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa Namtumbo miaka ya nyuma.

Katika hatua nyingine, Mpenye alisema Halmashauri imeanza mkakati wa kulima zao la kahawa na zaidi ya miche 16,000 imenunuliwa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kahawa cha Ugano wilayani Mbinga na kusambaza kwa wakulima katika kata ya Namabengo na Msindo.

Alisema lengo la halmashauri ni kuwa na mazao matano ya biashara yatakayosaidia wananchi kuondokana na umasikini kwa sababu watakuwa na mazao mengi ya biashara badala ya kutegemea tumbaku na ufuta.