Ligi ya netiboli kisiwani Unguja yapamba moto

LIGI ya netiboli Kanda ya Unguja imezidi kupamba moto katika uwanja wa Gymkhana huku timu ya Polisi ikiendeleza wimbi lake la ushindi kwa kuifunga Sogea mabao 62-24.

Mchezo huo ambao ulitanguliwa na mchezo kati ya JKU na Sogea wanawake ulichezwa saa 11:00 jioni na kutoa burudani tosha machoni mwa mashabiki waliofika kuangalia mchezo huo.

Katika mchezo huo Polisi iliongoza katika robo zote hali iliyowakatisha tamaa mapema wapinzani wao hao ambao walivuna mabao 24 na Polisi kuvuna mabao 62.

Kwa upande wa mchezo kati ya JKU na Sogea ulimalizika kwa timu ya JKU kushinda mabao 61-13.

Ligi hiyo leo itakuwa ni mapumziko na itaendelea keshokutwa kwa michezo miwili ambapo mchezo wa kwanza utakuwa ni kati ya JKU na Zimamoto na wa pili utakuwa ni KVZ na Sogea zote zikiwa ni mechi za wanawake.