Vyombo vya usafiri majini kulipia utabiri hali ya hewa

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inakusudia kuanza kutoza tozo katika vyombo vya usafiri wa majini, kutokana na huduma wanayopata ya utabiri wa hali ya hewa.

Hayo yalisemwa juzi na Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi katika wizara hiyo, Aaron Kisaka wakati wa mahafali ya wanafunzi wa kozi ya utoaji wa taarifa ya hali ya hewa katika vituo vya anga nchini, iliyotolewa na Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma.

Kwa mujibu wa Kisaka, kwa sasa wapo katika utafiti kujua namna ya kutoza tozo hiyo, kwa wanaohitaji huduma hiyo baharini na kama wana uwezo wa kulipia kama inavyofanyika katika usafiri wa anga. Katika mahafali hayo ya kozi ya tatu, wahitimu walikuwa 11 na kati yao wanawake wakiwa wanne.

Alisema wanaotaka huduma hizo wanaweza kulipia ili kuboresha utolewaji wa huduma za hali ya hewa kama ilivyo usafiri wa anga, jambo linalosaidia wasafiri kuwa na uhakika wa safari kutokana na matumizi ya taarifa za hali ya hewa.

Kisaka alisema kwa sasa mjadala huo unaendelea na wanatarajia kufanya mazungumzo na vyombo vya usafiri Zanzibar na kuhamasisha matumizi sahihi ya taarifa hizo ili kuepuka maafa.

Akizungumza katika mahafali hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Burhani Nyenzi, alisema maisha ya abiria na usalama wa vyombo vya usafiri wa anga, yako mikononi mwao hivyo lazima kuwe na moyo wa kujituma katika kutoa taarifa za hali ya hewa mara kwa mara na kutaarifu wahusika.

Alisema ni vema kuhakikisha watu wanaotumia huduma hizo wanaridhika kwa huduma nzuri na hivyo ndiyo itaonesha kiwango chako kilivyokua katika kutoa huduma na siyo kuangalia ufaulu wako katika vyeti na kujisifia .

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi alisema mafunzo hayo ni utekelezaji wa mkakati wa mamlaka hiyo, kuendeleza watumishi ili kukidhi viwango vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Alisema mpaka sasa Tanzania ni miongozi mwa nchi chache zinazopiga hatua ya kutekeleza agizo la shirika hilo, kuwa ifikapo Desemba mwaka huu, wafanyakazi wanaotoa huduma za hali ya hewa kwenye vituo vya anga wawe na elimu ya shahada ya kwanza na uelewa wa kutosha.

Alisema katika kuboresha mafunzo hayo sasa yatafanyika chuoni Kigoma ili wanafunzi wapate muda zaidi wa kujifunza. Naye Mkuu wa Chuo cha Hali ya Hewa Kigoma, Joseph Aliba alisema kozi hiyo ni sehemu ya kozi fupi zitolewazo chuoni hapo kuwaendelea wafanyakazi wa TMA na kutaka wanawake wahamasike zaidi katika kuongeza uwezo kazini.