Magufuli: Wekezeni maeneo yenye tija

RAIS John Magufuli ameitaka mifuko ya jamii kuacha kuwekeza kwenye maeneo yasiyo na tija yasiyosaidia kuongeza ajira na wanachama zaidi.

“Hifadhi za jamii zinaingiza kwenye maeneo ya ajabu ajabu, wawekeze kwenye viwanda wapate faida. Ukiwekeza kwenye viwanda utapata wanafanyakazi wengi na utapanua wigo wa ajira,” alisema Magufuli. Rais Magufuli aliyasema hayo juzi mjini hapa akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Alisema ni muhimu kwa wenye mifuko ya jamii kuwekeza kwenye viwanda kwani watapata wafanyakazi wengi ambao watakuwa wanachama watakaojiunga na mifuko hiyo na kupanua wigo wa ajira. “Ukiwekeza kwenye viwanda cha ngozi au viatu wafanyakazi watakuwa wanachama na vijana watakaomaliza vyuo watapata ajira,” alisema Rais.

Aliwataka kuangalia mbele zaidi kwa kuona fursa ambazo zitasaidia kuinua mifuko hiyo na si kuwekeza kwenye miradi ambayo haina tija yoyote kwao na kwa jamii pia. “Ukiwekeza kwenye daraja au kalvati ambalo likijengwa kwa mwezi mmoja wafanyakazi watakuwa wa mkataba na wakimaliza kazi wataondoka na hawatafaidika,” alisema.

Alisema pia anakubaliana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kupunguza idadi ya mifuko ya hifadhi ibaki miwili.

“Kazi hiyo ifanyike kwa umakini na kuangalia historia iliyoanzisha mifuko hiyo na ninaahidi kazi hiyo nitaikamilisha katika mwaka 2016/2017 na namkabidhi kazi hiyo Waziri Jenista Mhagama,” alisema Magufuli. Pamoja na hayo alisema serikali imeshalipa Sh bilioni 500 kati ya Sh bilioni 710 fedha iliyokuwa ikidaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii.

Alisema suala la kujiunga na vyama vya wafanyakazi ni hiari na waajiri wawaruhusu wafanyakazi kujiunga bila kushurutishwa au kuchaguliwa chama. Alivitaka vyama visitumike kuchochea migogoro ya kikazi bali lengo ni kuimarisha uhusiano.

Alisema waajiri wengi wamekuwa hawatekelezi sheria za kazi na kuwa na wafanyakazi kwa muda mrefu ambao hawana mikataba ya ajira na serikali ya awamu ya tano haitavumilia. Rais Magufuli alisema pia serikali itarekebisha sheria ya mahusiano kazini na waajiri watatozwa faini ya papo kwa papo na waajiri watalipa faini kila itakapobaimnika wameshindwa kutekeleza sheria.

Aidha, Magufuli alisema serikali ya awamu ya tano imelenga kuhakikisha wananchi wengi wanajiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii na ya bima za afya. Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata huduma za afya zilizo bora.

Awali Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya alisema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, imeleta matumaini kwa wafanyakazi tofauti na serikali zilizopita, kwani usimamizi na utawala wa sheria unatekelezwa kwa dhati na ujasiri, hali inayorudisha matumaini ya wafanyakazi yaliyopotea.