Waridhishwa na ahadi ya ongezeko la mishahara

WATUMISHI wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na idara na taasisi zake wameipongeza hotuba ya Rais Ali Mohamed Shein katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani ya kutangaza kutekeleza ahadi ya kuongeza kima cha chini cha mishahara kufikia Sh 300,000 kuwa itaongeza ufanisi wa kazi na ari ya uzalishaji mali.

Baadhi ya wafanyakazi waliohojiwa walisema Dk Shein ameonesha uwezo wa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo ambazo alizitoa kwa nyakati tofauti, ikiwemo kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu, kwa kusema akichaguliwa kuongoza awamu ya pili ataongeza mishahara katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa fedha.

Ali Issa ambaye ni mfanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali alisema wamefurahishwa na uamuzi huo ambao sasa utaongeza ari ya kufanya kazi na kupambana na hali ngumu ya maisha.

“Nimefurahishwa na uamuzi uliochukuliwa na Rais Shein wa kuongeza kima cha chini cha mshahara kufikia Sh 300,000 utasaidia kuongeza ari ya kazi na kuleta ufanisi kwa ajili ya kuboresha maisha ya wafanyakazi na kupambana na ugumu wa maisha,” alisema Issa.

Tukena Abdalla Amour anayefanya kazi Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi alisema Rais Shein ameonesha muungwana anavyotakiwa kuwa kwamba akiahidi kwa kutoa ahadi huitekeleza bila ya ajizi kwa wakati mwafaka.

Alisema ahadi aliyoitoa katika kipindi cha kampeni za Uchaguzi Mkuu baadhi ya wananchi waliikejeli, ikiwemo wapinzani wa vyama vya siasa na kusema haitekelezeki kwa sababu nchi haina uchumi imara ambayo ilikuwa na lengo la kutaka kuwavunja moyo watumishi wa serikali tu.

“Mimi nimefurahishwa na kauli ya Rais Shein ya kutangaza kima cha chini cha mshahara kupanda kutoka Sh 150,000 hadi 300,000 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyokuwa akituambia katika kipindi cha mikutano ya hadhara ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwamba nikichaguliwa nitaongeza mishahara,” alisema.

Hassan Iddi wa sekta ya binafsi ya hoteli za kitalii aliwataka wawekezaji binafsi nao kuitikia mwito wa rais kuongeza mishahara ili iende sambamba na hali ya maisha iliyopo kwani utalii ndiyo tegemeo la uchumi wa Zanzibar kwa sasa.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (ZATUC), Khamis Mwinyi alisema hotuba ya rais ni dira kwa wafanyakazi na watumishi wa serikali ambao ndiyo wanaotegemewa kutekeleza majukumu mbalimbali.

Alisema wamefurahishwa na rais ambaye amedhihirisha kwamba ni mtu anayewapenda wafanyakazi kwa kuzingatia maslahi bora kwa mujibu wa hali ya maisha ilivyo kwani ukweli ni kwamba maisha yamepanda.