Rais alivyowatia moyo wafanyakazi maadhimisho Mei Mosi

SIKUKUU ya Wafanyakazi Duniani imeisha na kuwaacha wafanyakazi wakifurahia uongozi wa Serikali ya Awamu wa Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu kwa kupunguza kodi ya mishahara, kuboresha huduma za mashirika ya hifadhi ya jamii na kudhibiti ajira kwa wageni.

Kwa hotuba yake iliyoonesha maamuzi yake, Rais Magufuli amefufua matumaini ya wafanyakazi ya kufanikiwa kuwa na hali bora kwa kutekelezewa madai yao na pia kuoneshwa uwapo wa juhudi zinazofanywa na serikali za kuweka mambo sawa. Ingawa wafanyakazi hawakutangaziwa ongezeko la kima cha chini cha mshahara cha Sh 315,000, ambacho serikali imekuwa ikisema haiwezi kukilipa kwa muda mrefu, imetoa jibu kuhusu kilio cha wafanyakazi kutaka kupunguzwa kwa kodi ya mshahara.

Akihutubia hivi karibuni kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi iliyofanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, Rais Magufuli amesema kodi ya mishahara itapunguzwa kutoka asilimia 11 za sasa hadi asilimia tisa ili kuwapa unafuu wafanyakazi. Kupungua kwa kodi hiyo, kumeelezwa na wachumi kwamba kutasaidia zaidi watu wanaopata mishahara kuanzia laki tatu na sitini kwenda juu, ambapo serikali itaachia kiasi cha 3,800 wakati chini yake serikali itaachia Sh 1,100.

Kuna mawazo tofauti kuhusu suala hilo la upunguzaji wa kodi ya mishahara, lakini kiujumla zote zinaonesha nafuu kwa mfanyakazi ingawa wapo wanaosema kwamba wenye kipato cha juu ndio watanufaika zaidi. Mkufunzi chuo kikuu cha Iringa, Essau Ntabindi, amesema kwamba punguzo hilo litakuwa na manufaa kwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara mikubwa tu. Hata hivyo anasema kwamba rais amefanya vyema kupunguza kodi hiyo, ingawa angelifurahi kuona kwamba rais anaongeza kima cha mshahara wa chini.

Hata hivyo, kwa watu wa kawaida , wanaona kwamba kitendo cha Rais ni cha kuungwa mkono hasa kwa kuangalia kwamba wafanyakazi kupitia TUCTA wamekuwa wakitaka angalau kupunguzwa kodi ya mashahara kufikia digiti moja. Rais katika maamuzi yake alisema, ameamua kuanza na hilo la kupunguza kodi ya mishahara na baadaye mambo yakiwa mazuri ataangalia suala la kupandisha mishahara.

Hata hivyo anasema kodi ikipungua kutoka asilimia 11 hadi tisa kutakuwa na pengo la makusanyo ndani ya serikali na wao wataangalia namna ya kufidia pengo hilo. TUCTA yenyewe kupitia kwa Katibu wake mkuu Nicholaus Mgaya amesema wamefurahishwa na Rais kupunguza kodi kwani ndio kilikuwa kilio chao kikubwa.Anasema punguzo hilo litasaidia kuleta ahueni kwa kiwango kikubwa na kwamba wafanyakazi wameshinda mtihani kwa asilimia 35 kati ya 100, kama wangelikuwa darasani, kwani Rais amewakumbuka.

Rais wa TUCTA, Gratian Mukoba anasema kwamba rais ameonesha mwanga kwa wafanyakazi na anastahili kupongezwa. Hata hivyo, anasisitiza kuwa TUCTA itaendelea na kampeni ya kudai haki za wafanyakazi ikiwamo kupandisha kima cha chini cha mishahara ili kuendana na gharama halisi za maisha. Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Haji Semboja, anasema kwamba maamuzi ya rais yana ishara nzuri na pia yanaweza kuwasaidia waajiri kuongeza idadi ya wafanyakazi kutokana na kuwepo kwa kiwango kidogo cha malipo ya kodi ya mishahara.

Hata hivyo, anasema vibarua au watu wa mikataba hawataguswa na punguzo hilo kwani wao hulipwa kwa jinsi wanavyofanya kazi. Serikali ambayo ndiye mwajiri mkubwa nchini, kwa kupunguza kodi itakuwa imejitengenezea pengo kubwa la pato ambalo kama rais alivyosema wataangalia wapi pa kupata za kuziba pengo hilo ambalo lilikuwa linajazwa moja kwa moja. Kwa muda mwingi wafanyakazi wa Tanzania wamekuwa wakidai kupunguzwa kwa kodi hiyo, kupandishwa kwa mishahara na kuangaliwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo ilikuwa inafanya mambo ndivyo sivyo na kuumiza zaidi wastafu.

Pamoja na mafanikio hayo ya TUCTA katika kodi, taasisi hiyo pia kwa hotuba ya Rais imepata maksi hasa kwa kuangaliwa kwa uwezekano wa kuandaliwa kwa sheria na masharti mapya ya uwekezaji yatakayosaidia jamii na taifa linufaike kutokana na uwekezaji huo. Kulingana na taarifa mbalimbali hali ya uwekezaji Tanzania bado si nzuri na licha ya sheria zilizotungwa kuwa na masharti nafuu kwa wawekezaji, bado kuna ajira nyingi za Watanzania zinakwenda kwa wageni na Rais amesema hilo halikubaliki, huku akitolea mfano kazi za huduma katika mahoteli kupokwa na wageni kwa kuwa wanajua kiingereza.

Akitoa mfano Rais Magufuli anasema wafanyakazi wa mahoteli ya Urusi, China, Ujerumani hawazungumzi Kiingereza, hivyo hoteli za Tanzania zitahudumiwa na Watanzania wanajua Kiswahili na kuwaasa wafanyakazi wa hoteli kuacha kuajiri wageni kwa kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania. Kwa kauli ya Rais Magufuli maana yake ni kuwa mapungufu yaliyo katika sheria yanayotoa mwanya kwa baadhi ya wawekezaji kuwa mabingwa wa kukwepa fidia, kulipa kodi ya mapato na ushuru hivyo taifa kutonufaika na uwekezaji huo yatashughulikiwa na Watanzania kunufaika na uwekezaji.

Kabla ya Mei Mosi maswali kwa rais yalikuwa mengi na yote yaligusa ustawi wa wafanyakazi, kima cha chini cha mshahara na kuhusu makato makubwa ya kodi ambayo yalionekana ni mambo ya uonevu kwa wafanyakazi. Miezi ya nyuma Katibu wa TUCTA mkoa wa Dodoma, Ramadhani Mwendwa amewahi kusikika akilalamika kuwa wafanyakazi wana makato makubwa ya kodi Serikali haijafanya jitihada za kupunguza wakati huohuo makampuni makubwa yakionekana kukwepa kodi.

Baada ya kushuka kwa kodi kinachofuata sasa ni wa wafanyakazi kuendelea na majadiliano ya kupandishwa kwa kima cha chini cha mshahara hadi kufikia Sh 315,000. Ni kweli kuwa kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi kinamtosha kuishi kwa muda wa siku saba tu halafu siku 23 zinazobaki anaishi kwa kukopa. “Mshahara huo ambao mfanyakazi anaupata kwa muda wa mwezi mmoja unalingana na posho ya siku moja ya baadhi ya viongozi wa Serikali au taasisi mbalimbali,” anasema Mwendwa.

Anasema pamoja na mshahara huo mdogo, wafanyakazi hao bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kupanda kwa gharama za umeme na mafuta, hali inayosababisha gharama za maisha kuwa juu. Katika mahojiano pia Mwendwa alisema wafanyakazi wanaitaka Serikali kuendelea kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali ikiwemo kuendelea kukabili ubadhirifu na rushwa kama walivyoanza kwa kubana wanaotumia hovyo ofisi, kutowajibika na hata wenye harufu ya ufisadi kwa lengo la kuwa na nidhamu na matumizi ya fedha za serikali.

Katika suala la kukabili rushwa, Rais Magufuli amesema ataendelea kulala nao mbele watu wanaotengeneza wafanyakazi hewa mpaka kieleweke. Anasema watumishi hewa sasa wamefikia 10,295 ambao wanalipwa mishahara kila mwezi ndio wamekuwa wakichelewesha mambo mengi ya ustawi wa wafanyakazi mtu mmoja mmoja na kijamii. “Tanzania tumechezewa sana na wafanyakazi hewa ambao wamo miongoni mwetu,” anasema rais na kuongeza kuwa wafanyakazi hao wamekuwa wakilipwa bilioni 11.6 kwa mwezi ambapo kwa mwaka wamekuwa wakilipwa Sh bilioni 139.2 na kwa miaka mitano wanalipwa bilioni 696.1.

Fedha ambazo zingeweza kutosha kujenga madaraja matatu kama lile la Mwalimu Nyerere lililopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam. “Hizo bilioni 696 zingetosha kujenga barabara za juu saba, pia kama zingetumika kulipa mishahara ndani ya serikali ingeongezeka na ingeamua kujenga hospitali nyingi hawa ndio wamechelewesha huduma nzuri kwa wafanyakazi."

Pamoja na kukabili rushwa na kupunguzwa kwa kodi kama ilivyotakiwa na wafanyakazi, bado ipo kazi kubwa kwa wafanyakazi wenyewe, kwani wanatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa kujiamini na kujituma ili kuokoa kiasi cha fedha kwani mabilioni yamekuwa yakipotea. Suala la hifadhi ya jamii ambalo limekuwa likilalamikiwa sana na TUCTA,limeonekana kufanyiwa kazi kiasi cha taasisi hiyo kuipongeza serikali kwa juhudi za kuliokoa Shirika la Hifadhi la Jamii la PSPF.

Aidha TUCTA wanasema Rais ameonesha kujali madai ya wafanyakazi pale alipoitaka mifuko ya jamii kuacha kuwekeza kwenye maeneo yasiyo na tija na kuwekeza katika maeneo yatakayosaidia kuongeza ajira na kujipatia wanachama zaidi. “Hifadhi za jamii zinaingia kwenye maeneo ya ajabu, wawekeze kwenye viwanda ili wapate faida. Ukiwekeza kwenye viwanda utapata wafanyakazi wengi na utapanua wigo wa ajira, ukiwekeza kwenye daraja au kalvati likajengwa kwa mwezi moja wafanyakazi watakuwa na muda wanaweza kufanya kwa wiki mbili na wewe umewekeza fedha,” anasema.

Anasema ni muhimu kwa wenye mifuko ya jamii kuwekeza kwenye viwanda, kwani watapata wafanyakazi wengi ambao watakuwa wanachama watakaojiunga na mifuko hiyo na kupanua wigo wa ajira. Kwa miaka mingi wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia tabia ya uwekezaji ya hifadhi ambayo haiendani na kazi zake katika jamii. Lakini la maana kabisa ambalo Rais alisema ni kukubaliana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) la kupunguzwa idadi ya mifuko ya hifadhi ili ibaki miwili.

“Kazi hiyo ifanyike kwa umakini na kuangalia historia iliyoanzisha mifuko hiyo na ninaahidi kazi hiyo nitaikamilisha katika mwaka 2016/2017 na namkabidhi kazi hiyo Waziri Jenister Mhagama.” Katika kuuhuisha uhai wa mifuko, Rais anasema kwamba serikali imeshalipa Sh bilioni 500 kati ya bilioni 710 fedha iliyokuwa ikidaiwa na mifuko ya hifadhi. “Nilishatoa maagizo Hazina wamelipa sh bilioni 500 bado bilioni 210,” anasema.

Aidha aliwataka waajiri wote kulipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili isiwe kero kwa wafanyakazi pale wanapostaafu. Ni dhahiri kama alivyosema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano tangu imeingia madarakani na kuleta matumaini kwa wafanyakazi, tofauti na serikali zilizopita.

Anasema ni matumaini yake kwamba ishara zilizojionesha zinatia moyo wafanyakazi kujituma zaidi na ni matumaini yao kuwa katika kipindi cha miaka mitano anayoiongoza, mishahara ya wafanyakazi itaboreshwa kwa sababu hata mapato ya serikali sasa yanaonekana kupanda tofauti na miaka iliyopita. “Katika hili tunapendekeza serikali itunge sera ya mishahara itakayosimamia urekebishaji na uboreshaji wa mishahara na marupurupu ya mfanyakazi wa umma na sekta binafsi,” anasema Mgaya.