si Watoto 9 wenye vichwa vikubwa wafanyiwa upasuaji

WATOTO tisa waliokuwa na vichwa vikubwa na mmoja mwenye tatizo la mgongo wazi, wamefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Upasuaji huo ulifanywa na timu ya madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), kwa kushirikiana na wataalamu kutoka shirika lisilo la Serikali la GSM.

Kati ya watoto 35 waliojitokeza 25 wameshindwa kufanyiwa upasuaji kwa kuwa maradhi yao yameonekana kukomaa. Profesa Josephati Kahamba kutoka MOI, alisema hayo baada ya kuhitimisha kazi ya upasuaji iliyofanyika kwa siku mbili, huku akieleza kuwa watoto 35 walijitokeza na waliofanyiwa upasuaji ni 10, mmoja akiwa ni mwenye mgongo wazi.

Alisema, lengo ni kuipa elimu jamii kuondokana na imani potofu kuhusu maradhi hayo na kuwafikisha watoto katika vituo vya afya mapema kuepusha tatizo kuwa kubwa na kushindikana.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Nuru Mpuya, alisema kuwa, wataalamu walishiriki kikamilifu na kuwapa mafunzo wataalamu wa hospitali hiyo ya mkoa kutoa elimu ili jamii iondokane na mila potofu juu ya matatizo hayo.