Kampuni ya TBL yaelimisha matumizi sahihi dawa za kilimo

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL Group) imesema imejikita katika kuelimisha wakulima inaoshirikiana nao katika matumizi sahihi ya dawa za kilimo zenye kemikali za sumu na jinsi ya kujikinga wasiathirike na matumizi yake ikiwemo kuwapatia vifaa vya kujikinga.

Kampeni hiyo inayotekelezwa kwa kushirikiana na kampuni ya kuuza mazao na pembejeo za kilimo ya Syngenta Tanzania, tayari imeanza kutekelezwa kwa wakulima wa shayiri mkoani Arusha na itaendelea kufanyika katika mikoa mbalimbali.

Meneja anayesimamia uendelezaji wakulima kutoka TBL Group, Dk Bannie Basson alisema hivi karibuni kuwa mkakati huo una lengo la kuhakikisha wakulima wanafanya kazi yao katika mazingira ya usalama ili waweze kufanya uzalishaji wenye tija.

Aliwataka wauzaji wa dawa za kilimo na pembejeo nchini kuhakikisha wanakuwa na wataalamu wa kutoa elimu ya usalama kwa wakulima kuwaepusha madhara ya dawa ambayo yamekuwa yakiathiri afya za wakulima kutokana na kutokuwa na elimu ya matumizi yake.

Meneja Biashara wa Syngenta Tanzania Ltd, Samuel Muturi alisema kampuni yake inafurahia kufanya kazi na TBL katika kuwapatia wakulima elimu juu ya matumizi ya dawa za kilimo zenye kemikali za sumu na vifaa vya kujikinga na aliwaasa wakulima kuzingatia kanuni za usalama wanazofundishwa.

Godwin Mollel, Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa zao la shayiri cha Fungamano kilichopo Monduli, Arusha, akizungumza kwa niaba ya wenzake alishukuru jitihada zinazofanywa na TBL kusaidia wakulima tangu ilipoanzisha mpango wa kushirikiana nao.