RC acharukia miradi ya maji Bariadi

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka ameitaka Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Bariadi kukabidhi taarifa ya miradi ya maji iliyotekelezwa na serikali katika wilaya hiyo ndani ya siku nne kuthibitisha kama imekamilika.

Miradi hiyo ambayo ilikuwa ikitekelezwa na wazabuni na baadaye kukabidhiwa kwa serikali imeonekana kutokamilika kwa muda mwafaka huku kujengwa chini ya kiwango.

Mtaka aliyasema hayo jana katika kikao cha Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo kilichofanyika mjini Bariadi huku akisema wazabuni waliojenga miradi hiyo chini ya kiwango watashughulikiwa.

Alisema serikali haiwezi kupoteza fedha katika ujenzi wa miradi ya maji ambayo haikamiliki pia imebainika kujengwa chini ya kiwango kwa gharama kubwa ambazo ni kodi za wananchi.

‘’Naagiza kamati ya ulinzi na usalama, mkurugenzi na watu wako mniletee taarifa ya miradi yote ya maji iliyojengwa katika halmashauri yenu ili tujiridhishe kama imejengwa chini ya kiwango tuweze kuwashughulikia wahusika,’’ alisema Mtaka.

Aliongeza kama kuna mzabuni alipewa kujenga mradi wa maji kwa kuwa ni kada wa chama tawala, serikali haitasita kumchukulia hatua kwa kuwa ameharibu rasilimali fedha za taifa.

Katika hatua nyingine, Mtaka alisema hawezi kuwavumilia watumishi wazembe wanaoiangusha serikali kwa kutosimamia miradi ya maendeleo kamilifu ambayo imekuwa ikijengwa na wakandarasi chini ya kiwango.

Aidha, amewataka madiwani kuhakikisha wanawachukulia hatua wataalamu wa halmashauri hiyo ambao wamekuwa na mazoea ya kuandika taarifa za uongo katika mabaraza, huku akiitaka halmashauri hiyo kuanza kukusanya ushuru wa mazao kwa njia ya kielektroniki bila kutegemea wazabuni hali itakayoongeza makusanyo mapato ya halmashauri.