25Mei2013

 

OUT kuimarisha ushirikiano na TSN

CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kimeahidi kuimarisha ushirikiano na Kampuni ya Tanzania Standard Newspaper (TSN) Ltd, kwa kuwa dhamira zao ni moja, kuijenga nchi na kuleta maendeleo kwa jamii.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, anayeshughulikia Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa (DVC, LT & RS), Profesa Modest Varisanga alisema hayo jana alipotembelea ofisi za TSN na kukutana na Menejimenti yake.

Ziara hiyo ya Profesa Varisanga, ilitokana na mwaliko wa Kaimu Mhariri Mtendaji wa TSN, inayochapisha magazeti ya Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo, Gabriel Nderumaki, ikiwa ni hatua ya kufahamu kazi za kampuni na kukuza ushirikiano wa kijamii na kibiashara baina ya taasisi hizo mbili.

“TSN na sisi OUT tuna jukumu moja kubwa la kujenga nchi yetu, nyie ni wadau wakubwa sana katika hili, mimi na timu yetu tutakaa tuone namna ya kusaini makubaliano ya kufanyakazi pamoja na tupo tayari kuendeleza ushirikiano baina yetu,” alisema Profesa Varisanga.

Awali akiukaribisha ujumbe huo TSN, Nderumaki alisema kampuni imejizatiti kutoa habari za ukweli hata kama wengine wataona haziuzi, kuliko kuandika kwa ushabiki na uongo.

“Uhusiano baina yetu ni wa muda mrefu, lakini inawezekana hapa na pale tumekwaruzana, nitumie nafasi hii kuomba radhi kwa lolote, lakini sisi TSN ajenda yetu ni ukweli daima, kuwa kiini cha taarifa sahihi na sehemu ya kufanyia utafiti kuhusu mambo mbalimbali,” alifafanua Nderumaki.

Alisema OUT ni miongoni mwa wadau muhimu wa TSN na kutokana na umuhimu huo, imeandaa utaratibu wa namna nzuri ya malipo ya matangazo na imeanzisha kitengo maalumu cha kusikiliza malalamiko, kero na mrejesho, ili kuwaondolea wateja usumbufu wa kupata huduma bora.