Simba na ahadi za mafanikio

SIMBA ina kiu ya ubingwa, ina kiu ya muda mrefu ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, lakini kwa sasa imekata tamaa kwa vile tayari watani zao wa jadi, Yanga wamebakisha mchezo mmoja watangaze ubingwa.

Mashabiki wamechoka kutaniwa na wapinzani wao kuwa ni ‘wa hapa hapa’ kwa kushindwa kutwaa ubingwa na kuishia kuambulia nafasi ya tatu huku wakiacha upinzani kwa Yanga na Azam FC. Yanga inahitaji pointi mbili tu itangaze ubingwa, huenda Mei 10 ikifanikiwa kuinyuka Mbeya City mjini Mbeya, kwa sasa ina ina pointi 68 itakuwa imefikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote si Azam wala Simba.

Simba ana pointi 58, ana michezo minne mkononi akichuana na Azam ambayo ina pointi 60 ina michezo mitatu mkononi iwapo atashinda michezo yote atakuwa na pointi 69 hivyo kwa sasa Simba na Azam ndizo zinazowania nafasi ya pili kila mmoja anamuombea adui yake ‘njaa’, atakayepoteza mchezo mmoja imekula kwake.

Kiu hiyo ya kutocheza michuano ya kimataifa kwa mara ya nne mfululizo, imekuwa ikiwaumiza mashabiki wa Simba ambao sasa kupitia makundi mbali mbali katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakiutupia lawama uongozi kwa kushindwa kuwapa raha na kutimiza ahadi zake, ikiwemo kuhakikisha timu hiyo inacheza michuano ya kimataifa. Baadhi ya ahadi za Aveva alipoingia madarakani ni pamoja na:

Timu imara

Wakiingia madarakani Juni 29, 2014, Rais wa Simba, Evans Aveva na wajumbe wake waliahidi kuwa na timu ya Simba imara na yenye ushindani ambayo ingechukua ubingwa na kuwakilisha vema kimataifa, ikiwa ni pamoja na usajili mzuri na timu kuwika katika anga za kimataifa, hali hiyo imekuwa tofauti na sasa mashabiki wa klabu hiyo wanawika kwa jina la ‘Wamatopeni’.

Soka la vijana

Ahadi nyingine ni kuendeleza timu imara ya vijana chini ya miaka 20, hili lilikuwa ni hitaji kubwa kwa Wanasimba wote, hasa ukizingatia kwa wakati huo tayari walianza kunufaika na vijana wao kama Ramadhani Singano “Messi”, Harouna Chanongo, Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo.

Lakini katika hali isiyotegemewa kikosi cha ‘Simba B’ kilichokuzwa kwa miaka mitatu, ikiwa ni mpango wa ukuzaji vijana ikiwa na wachezaji kama Ramadhani Singano ‘Mess’, Japhet Makaray ‘Baloelli’, Carlos Protus, Miraji Madenge ‘Sheva Go’, Abdallah Sesemme, Hassan Khatibu na Edward Christopeher ‘Edo’ walijikuta wakifungashiwa virago ndani ya klabu hiyo ya Msimbazi na kwa sasa wanakipiga timu ya Toto African na siku chache zilizopita walifanikiwa kuzima ndoto ya Simba kucheza kimataifa baada ya kuwanyuka bao 1-0 kwenye uwanja wa Taifa.

Kuongeza wanachama

Wakati akiingia madarakani Aveva alisema Simba itakapokuwa inafanya vizuri wanachama wenyewe watarudi ‘waliondoka kutokana na timu kufanya vibaya’ lakini itavutia wanachama wapya na hivyo kuwa na idadi kubwa ya wanachama ambao ni rasilimali nzuri kwa timu. Wakati uongozi wa Simba ukiingia madarakani Juni 29 , 2014 Simba ilikuwa ina wanachama takribani 7,000 ahadi ilikuwa ni kufikisha wanachama 50,000. Hata hivyo, kusuasua kwenye ligi kumeibua makundi ndani ya klabu hiyo ya mtaa wa Jangwani.

Uwanja wa Bunju

Fimbo kubwa ya kuwachapia wanyonge waliojitokeza kusikiliza sera za viongozi wao wakati wa kampeni na sasa umegeuka wimbo usiochuja, ni uwanja wa Bunju, ambao uongozi uliahidi kuukamilisha mwezi uliopita, Machi mwaka huu.

Mapema Februari Aveva akizungumza na mwandishi wa makala haya anasema ‘Nyasi zipo bandarini, zitafika baada ya wiki mbili tayari kwa ujenzi wa uwanja.” Muziki huo wa uwanja, gitaa lake likaendelea kuchagizwa vilivyo na na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zakaria Hanspope ambaye amedai anaujenga uwanja huo. “Nyasi zimekwishaagizwa kutoka China na zinatarajiwa kuwasili nchini kuanzia Machi, maana yake ujenzi wa Uwanja wa Simba uko mbioni kuanza."

Nyasi hizo zinaonekana bado zipo majini zikielea huku muziki wake ukiendelea kuvumishwa masikioni mwa mashabiki wa Simba ambao walianza kuusikia miaka saba iliyopita, enzi za utawala wa Hassan Dalali, ambaye alifanikiwa kupatikana kwa eneo hilo, Ismal Aden Rage naye akaingiza sauti yake katika muziki huo wa uwanja wa Bunju. Ilifikia mahali akatoa siku 90 kuukamilisha lakini baadaye akasema hawezi kuujenga uwanja kwa miaka minne wakati serikali imechukua miaka 50 kuujenga Uwanja wa Taifa.

Bado uongozi uliopo madarakani nao ukaja na wimbo huo huo. Hata hivyo, akizungumzia suala hilo la Rais wa Simba, Evans Aveva wamejipanga kufanya mabadiliko makubwa kukiboresha kikosi chao na hata wao hawafurahishwi na mambo yanavyoendelea. “Ubingwa tumeshafeli kupata labda ni kwa muujiza, tutafanya marekebisho kadhaa, tunahitaji mshambuliaji aina ya Okwi ambaye ataweza kuamua matokeo ya mchezo kama Donald Ngoma,” alisema.