Snura: Aponzwa na chura wake

WIMBO wa Chura umekuwa ni wimbo maarufu katika maeneo mbalimbali nchini na umekuwa ukitumika pia kwenye hafla mbalimbali za burudani. Huo ni wimbo wa msanii Snura Mushi ambaye kwa sasa anasifika zaidi na wimbo huo wa Chura baada ya kutamba na wimbo wa Majanga na mwingine uitwao Nimevurugwa.

Msanii huyo amekuwa akisifiwa zaidi kutokana na uwezo wake wa kucheza na kuimba hasa kucheza kwa kutingisha mwili wake. Amekuwa akicheza akihusisha zaidi staili ya kukatika huku akiwashirikisha zaidi wacheza shoo wake katika kunogesha zaidi uchezaji wake huo. Hasa akiwa kwenye shoo zake sehemu mbalimbali ndio amekuwa akitumia zaidi uwezo wake huo wa uchezaji na kuwavutia mamia ya watu.

Video yake mpya

Kwa hivi karibuni msanii huyo ametengeneza video ya wimbo wake mpya uitwao Chura ambapo wimbo huo umejikuta ukimwingiza matatizoni kwa sasa. Wimbo huo unaonesha wanawake wenye shepu wakicheza wakiwa kwenye hali isiyo ya kistaarabu huku wakionesha maungo yao ya mwili. Katika video hiyo inawaonesha wanawake hao wakicheza huku wakiwa wamevalia kanga, nguo nyepesi pamoja na madera.

Wanacheza huku wakiwa katika mazingira ya bahari na wanacheza kwa kukata mauno katika maji hali ambayo inachochea zaidi ushawishi hasa kwa watu kuangalia miili yao. Video hiyo imekuwa gumzo sehemu mbalimbali na hasa katika maeneo ya mijini, ambapo watu wamekuwa wakiipakua katika mitandao na kuiangalia.

Alijua alichofanya

Mwanamuziki huyo aliamua kuisambaza zaidi video hiyo katika mitandao ya kijamii kwa kuwa anajua akiisambaza katika luninga ingefungiwa na hata yeye kuingia matatani. Lakini kumbe alichokifikiria kukikwepa huko katika luninga ndicho anakuja kukumbana nacho katika mitandao ya kijamii kwa kuwa kwa sasa anakabiliwa na adhabu sawa na ile ambayo angekutana nayo katika luninga. Ni hivi juzi tu imeamriwa kusitisha video hiyo na pia ikaenda mbele zaidi kwa kusitisha pia na wimbo wa msanii huyo.

Imezuiliwa kuchezwa katika vituo mbalimbali vya luninga hadi pale ambapo ataufanyia marekebisho wimbo huo. Msemaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Zawadi Msalla akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa hukumu hiyo alisema kuwa video hiyo haiendani na maadili ya watanzania. Zawadi anasema kuwa ni wakati kwa wasanii kujifikiria mara mbili kabla ya kuingiza kazi zao sokoni kwa kuwa wanaweza kujiingiza katika matatizo.

Anasema ni vema kwa wasanii kujiuliza mara mbili kabla ya kubuni kazi zao za sanaa kwa kuwa wanafanya kazi katika jamii za kitanzania ambapo kuna ndugu, jamaa na marafiki wanaotaka kuona maadili yakitekelezwa. “Ni vema wasanii wakatambua kuwa sanaa sio uwanja wa kudhalilisha watu wala utu wa mwanamke ila ni vema wakaendeleza misingi mizuri ya kimaadili”, anasema Zawadi.

Anatoa mwito kwa wasanii kutojihusisha na tabia ya kusambaza video za nyimbo zisizokidhi maudhui katika mitandao ya kijamii kwa kuwa wanaweza hata kuchukuliwa hatua za kisheria. Lakini hakuishia hapo ila anamtaka Snura kwanza kabisa kukamilisha taratibu za usajili wa kazi zake za Sanaa katika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ili aweze kuendelea na kazi za sanaa. Anasisitiza kuwa kwa sasa msanii huyo hatakiwi kushiriki katika onesho lolote la muziki hadi hapo atakapotekeleza maagizo hayo.

Hoja hiyo ya Wizara imekuja muda mwafaka kwa kuwa wimbo ndio kwanza ulikuwa umezidi kushika chati katika mitandao ya kijamii. Lakini pia ni vema kwa wasanii wengine nao kutambua kuwa kumbe kukwepesha wimbo kuchezwa kwenye luninga na badala yake kuupeleka kwenye mitandao ya kijamii sio suluhisho na wala sio kwamba ndio wataachwa. Na ieleweke kuwa video ya aina yoyote ya muziki kabla ya kwenda hewani ni vema ikapelekwa kwanza BASATA na kisha ifahamike kuwa kwa kufanya hivyo ni njia bora ya uhakika wa kazi hiyo ya sanaa.

Kwa kile alichokifanya Snura ni sawa na kile kilichofanywa na msanii Ney wa Mitego ambaye wimbo wake ulizuiliwa kuchezwa kwenye Radio na yeye kuupeleka kwenye mitandao ya kijamii na akitumia hasa mtandao wake wa Instragram kuutangaza zaidi. Kinachotofautiana na huu wa Snura ni kitu kimoja kuwa huu wa Snura ni video ila wa Ney ni wimbo wa kusikilizwa. Kwa hiyo mamlaka husika zinatakiwa kuhakikisha kuwa zinapambana na aina hiyo ya ubabaishaji ili kuzuia maadili kupotea.

Kwa upande wake, Snura baada ya kudhibitiwa na BASATA amejitokeza hadharani na kuomba msamaha kwa wimbo huo pamoja na video yake. Anasema kuwa ameshaanza kutekeleza maelekezo ya Wizara na kwa sasa anatengeneza video mpya ambayo inakuwa na maadili. Anasema kuwa video hiyo itashirikisha watu waliovaa nguo nzuri na za heshima huku wakicheza kwa nidhamu.

Anasema kuwa pia hata wimbo wake huo ataurekebisha na kuwa wenye tija zaidi kwa jamii. Anafafanua kuwa yeye kama mwanadamu ana kasoro zake na kuwa anaweza kuwa alikosea kama mwanadamu na kuwa kushindwa huko kufanya wimbo wenye maadili haikuwa kosa lake kuidhalilisha haiba ya mwanamke. “Jamani na mimi ni kama mtanzania, nimeamua kuomba msamaha kwa kile kilichotokea na kwa sasa ninatengeneza video ya wimbo mwingine ambayo inaonekana kuwa ni ya kimaadili zaidi,” anasema Snura.

Anaongeza kuwa, “nitahakikisha kuwa ninafuata yale yote niliyoambiwa kuyafuata na kila kitu kitaenda sawa”. Pia anasema kuwa ameanza mchakato wa kujisajili BASATA na ili awe msanii huru na mwenye kufuata taratibu.

Kwa upande wake Ofisa Habari wa BASATA, Aristides Kwizera anasema kuwa kwa kuwa moja kati ya masharti aliyopewa ni kuhakikisha kuwa anajisajili katika Baraza hilo na kumtaka kufanya hivyo haraka. “Inatakiwa wasanii sasa wajue kuwa hapa ni kazi tu na kila kitu lazima kifuate maadili yanavyotaka na sio kufanya mambo kwa mazoea, ukiachana na hilo la Snura na maelekezo aliyopewa na Wizara kufanya ni vema kwa wasanii wengine pia wakaja kujisajili pia,” anasema Kwizera.