24Mei2013

 

Mahakama ya Rufaa yatupa pingamizi la Dawans kwa Tanesco

MAHAKAMA ya Rufaa imetupilia mbali ombi la Kampuni ya Dowans, kutaka taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga Shirika la Umeme (TANESCO) kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh bilioni 122, ifutwe.

Katika ombi hilo, Dowans inapinga taarifa hiyo iliyowasilishwa na Tanesco, baada ya Mahakama Kuu kukubali kusajili uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Uamuzi huo wa ICC uliosajiliwa Mahakama Kuu, umeitaka Tanesco iilipe fedha hizo kama fidia ya kuvunja mkataba wa biashara kinyume cha sheria.

Dowans wanadai kwa mujibu wa kanuni za Mahakama ya Rufaa, taarifa hiyo ya Tanesco ilitakiwa kuwasilishwa ndani ya siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu, lakini iliwasilishwa baada ya muda huo hivyo waliomba ombi hilo litupwe kwa gharama.

Hata hivyo, Tanesco kupitia kwa Wakili Richard Rweyongeza, walidai walichelewa kuwasilisha kwa sababu Mahakama Kuu ilichelewa kuwapa nakala za hukumu, kikazia hukumu na mwenendo wa kesi, ambazo ni nyaraka zinazotakiwa kuambatanishwa wakati wa kukata rufaa.

Aliongeza kuwa waliandika barua kwa msajili wa Mahakama hiyo kuomba nyaraka hizo, lakini mpaka jana hawajapata.

Akisoma uamuzi uliotolewa na jopo la majaji Steven Bwana, Benard Luanda na Edward Rutakangwa, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Ester Mkwiza, alisema ombi la Tanesco liliwasilishwa kabla ya muda wake unaostahili.

Msajili Mkwiza alisema, Tanesco hawakuwa na wajibu wa kumkumbusha Msajili kuwapa nyaraka zinazohitajika katika kuwasilisha rufaa yao. Aidha alisema hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa Tanesco walipewa nyaraka hizo kama inavyodaiwa na Dowans.

Alisema kutokana na sababu hizo, anatupilia mbali ombi la Dowans na kuwataka kulipa gharama. Katika hukumu ya Mahakama ya ICC, iliyotolewa Novemba 15 mwaka juzi, Tanesco iliamriwa kuilipa Dowans Holding SA na Dowans Tanzania Ltd (Dowans) dola za Marekani milioni 65, pamoja na riba na gharama za kuendesha kesi, baada ya kuvunja mkataba na kampuni hiyo kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Tanesco ilipinga hukumu hiyo lakini Septemba 28 mwaka jana, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu, alikubali kusajili tuzo ya malipo ya Dowans na kuiamuru Tanesco kulipa fedha hizo pamoja na gharama za uendeshaji kesi.

Kwa mujibu wa Wakili wa Dowans, Kenedy Fungamtama, hadi kufikia Novemba mwaka jana, deni la Dowans lilifikia zaidi ya Sh bilioni 122 kutokana na kuongezeka kwa riba ya asilimia 7.5 ya deni la awali la kila siku.