Maguli bado atamani kucheza nje

MCHEZAJI wa Stand United, Elias Maguli amesema mipango yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania bado ipo, atajipanga zaidi msimu ujao kulinda kiwango chake na kutimiza malengo.

Maguli alianza kwa kasi mara tu baada ya kujiunga na Stand United msimu huu akitokea Simba, ambapo hadi sasa ameifungia timu yake mabao 11.

Mchezaji huyo siku za hivi karibuni kiwango chake kimeonekana kushuka, baada ya kudaiwa kutoelewana na Kocha wake Patrick Liewig kwa kumuweka benchi kwa muda mrefu, hali iliyomfanya kushindwa kung’ara.

Akizungumza na gazeti hili, alisema hajakata tamaa, ana imani mambo yatakuwa mazuri siku zijazo baada ya kumalizika kwa msimu.

“Bahati yangu kama ipo naamini Mwenyezi Mungu atanisaidia, bado nina uwezo wa kufanya vyema, na kucheza soka nje ya Tanzania,” alisema.

Maguli aliwahi kufanya majaribio Misri katika timu ya Al Ahly, lakini hakufuzu na kusema anaendelea kuvuta subira huenda mambo yakawa mazuri zaidi msimu ujao.