Rais Magufuli ameonesha njia

 LICHA ya wakazi wa mikoa ya Rukwa na Katavi kupongeza hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati akizindua Bunge la 11 na hatua mbalimbali alizochukua katika kipindi kifupi na anazoendelea kuchukua, sasa wanawataka viongozi na wananchi kwa ujumla wao kutimiza majukumu yao pia. Wananchi waliohojiwa na mwandishi wa makala haya wanasema inapotokea Rais wa nchi analazimika kuingilia kati suala zima la usafi ni kiashiria kuwa kuna ambao wameshindwa kabisa kutimiza vyema majukumu yao. “Yaani inashangaza watu hata viongozi wetu wamejenga tabia ya kujibweteka mpaka Rais achukue hatua basi utashangaa jinsi wanavyohaha. Hii pia inaonesha kwamba katika maeneo mengi tunaongozwa na viongozi ambao si wabunifu na si wawajibikaji. "Hebu tujiulize kama viongozi kuanzia ngazi za chini kabisa zikiwemo ngazi za mitaa, kata, vijiji halmashauri za wilaya na manispaa hadi ngazi ya Taifa wangekuwa wabunifu na kutimiza wajibu wao ipasavyo kulikuwa na haja gani ya Rais kulazimika kutumia nguvu kuhamasisha wananchi na viongozi wao kufanya usafi tena nchini kote? Ni vyema hili tulichukulie kuwa ni aibu na sasa tubadilike, tujipange tusipate aibu hii tena," anasema Kadogo Kajibambe mkazi wa wilayani Nkasi mkoani Rukwa. Wananchi hao wanasema Kajibambe anasema anaunga mkono agizo la hivi karibuni alilolitoa Rais Magufuli la kufuta gwaride na shamrashamra za miaka 54 ya Uhuru wa Tanganyika katika sherehe ambazo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 9, ili fedha ambazo zingelitumika zielekezwe kwenye matumizi mengine. Lakini wanasema kuenea kwa kipindupindu ni matokeo ya uchafu na ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya nchi yetu kuna uchafu kuanzia sokoni hadi shuleni, kwani kuna shule ambazo hazina matundu ya vyoo lakini viongozi husika hawachukui hatua stahili. Wanasema hatua ya wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri wote nchini, kuagizwa kuandaa vifaa vya kufanyia usafi Desemba 9 na kwamba ifikapo Januari kusiwe na maeneo yatakayokuwa bado yana ugonjwa wa kipindupindu kutokana na uchafu, yote ni mafunzo kwa wananchi na watendaji. “Bila shaka Rais wetu hakufuta sherehe hizo kwa kutotambua umuhimu wake. La hasha bali ni kutokana na watu kutumia sherehe kujinufaisha zaidi kwa kununua vitu hewa lakini na pia, haiingii akilini kutumia pesa kwa ajili ya sherehe wakati wananchi wanakufa kwa kipindupindu, ugonjwa ambao sababu yake kubwa ni uchafu," anasema John Mwambao, mkazi wa Sumbawanga. Kwa hili la usafi, wengi walisema ni muhimu sana lichukuliwe kama funzo, kwamba utekelezaji wa majukumu kwa watendaji mbalimbali serikalini usisubiri maagizo kutoka ngazi za juu, bali kila mmoja atimize wajibu wake pale pale alipo. Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kipindupindu kimeshaua watu zaidi ya 100 kote nchini. Watu wengi mkoani Rukwa waliohojiwa wameeleza kuvutiwa na kuguswa na hatua mbalimbali zilizokwishachukuliwa na Rais Magufuli tangu aapishwe Novemba 5 mwaka huu, ikiwemo udhibiti wa matumizi ya fedha za umma huku akiagiza fedha zinazookolewa zitumike kwa shughuli za kijamii ama maendeleo. Mbali na Rais kusitisha safari za nje ya nchi zisizo na ulazima kwa watumishi wa umma, Rais Magufuli pia hivi karibuni aliingilia kati matumizi ya shughuli za uzinduzi wa Bunge la 11 na kuokoa zaidi ya Sh milioni 200 alizoagiza zielekezwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ili kununua vitanda kwa ajili ya wagonjwa. “Mie kwa hakika tangu awali nilikuwa simuungi mkono Magufuli wakati akijinadi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi. Badala yake nilikuwa nikimuunga mkono mgombea wa chama kingine... Lakini sasa ameweza kunibadili kabisa, ninamkubali baba huyu na kwakweli naona kumbe nilipoteza bure pesa yangu. "Hakika ahadi zake hazikuwa za danganya toto bali kiongozi huyo ameweza kuonesha kwa muda mfupi tu tangu aingie madarakani kuwa ana dhamira ya kweli kwa nchi hii," anasema mkazi wa mkoani Katavi aliyejitambulisha kwa jina la Jackson Msemakweli alipotakiwa kutoa maoni yake kwa jinsi anavyoona utendaji wa Rais Magufuli tangu aingie madarakani. Mkazi wa wilayani Kalambo, Maria Nankamba anasema: “Hakika baba huyu (Rais Magufuli) ameonesha jinsi alivyo na uwezo wa kufanya maamuzi kulingana na umuhimu wa jambo katika wakati husika kwa manufaa ya sisi wananchi tulio wengi. Katika kipindi kifupi amedhihirisha kwamba siyo tu kwamba ni kiongozi mchapakazi bali pia mbunifu." Wakizungumzia hotuba yake aliyoitoa bungeni mjini Dodoma hivi karibuni wakati akizindua Bunge la 11, wananchi wengi wa Rukwa na Katavi waliohojiwa na mwandishi wa makala haya wanakiri kuwa imefufua matumaini mapya kwa Watanzania na inaendana na falsafa ya ‘Hapa ni Kazi Tu.’ “Hakika hotuba ya Rais aliyoitoa bungeni ni ya kihistoria. Kwa muda mrefu mimi sijawahi kusikia hotuba inayosisimua kama hii hadi kutamani kuisikiliza kila siku ukiacha zile za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambazo hadi leo utapenda kuzisikiliza. Rais aliweza kugusa maeneo karibu yote muhimu, ikiwemo rushwa na ufisadi ulioshamiri nchini ambao ni kilio chetu kikubwa. “Mie binafsi nilifarijika sana kumsikia akitamka bungeni kuwa atapambana na rushwa na ufisadi kwa kuwa naye pia anauchukia... Hakika kauli yake hii ilinisisimua kwa kuona kuwa sasa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi nchini anatangaza vita sio vita vya mtutu wa bunduki katika kipindi hiki cha amani bali vita dhidi ya rushwa na ufisadi na kwa kweli hicho ndicho kilio chetu kikubwa," anasema Patrick Chazya. Akizindua Bunge la 11, Rais Magufuli aliwataka watendaji kote nchini kuhakikisha wanashiriki katika vita ya kuondoa umasikini, ili ukuaji wauchumi wa nchi uendane na ukuaji wa uchumi wa watu na kusisitiza kuongeza ajira kupitia viwanda. Alisisitiza kuwa kwa kuwa hakuna viwanda vingi vinavyotoa ajira kwa sasa, ni vyema watendaji wote wakaacha unyanyasaji kwa wafanyabiashara ndogo, wakiwemo mamalishe, machinga na bodaboda ambao wamelazimika kwenda huko ili kujitafutia. Akifafanua, Rais alisema biashara hizo ndogo, ndizo zinazosaidia vijana kuacha kujiingiza katika vikundi viovu na kujikita katika utafutaji wa kipato, huku akiongeza kuwa baadhi ya watendaji wakinyang’anya mama lishe chakula chao wanakila! Mbali na agizo hilo la kutosumbua wafanyabiashara ndogo, Dk Magufuli aliahidi kusimamia sekta ya viwanda kwa kuanza kufufua vilivyopo na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika eneo hilo. Kadhalika alisema ni muhimu viwanda hivyo vikajielekeza katika katika kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza thamani ya mazao na kipato cha wakulima, wavuvi, wafugaji na ajira na kwamba anataka hadi mwaka 2020, asilimia 40 ya ajira itokane na viwanda vinavyohusika na kilimo, uvuvi na mifugo. Katika viwanda vipya, Dk Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kupunguza urasimu serikalini huku akionya watendaji ambao wamekuwa wakizungusha wawekezaji, mpaka wanaamua kwenda kuwekeza katika nchi jirani, kwamba atawatimua mara moja.Dk Magufuli alisema pia atahakikisha umeme unakuwa wa kutosha na wa uhakika, kwa kuwa hawezi kuzungumzia viwanda wakati hakuna umeme wa kutosha, huku akionya watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), ambao wamekuwa wakihujumu miundombinu ya umeme, baada ya kuhongwa na wafanyabiashara wa majenereta na wanaouza mafuta. Rais alisema amejipa kazi ya kutumbua majipu, kazi ambayo anajua kuwa utumbuaji huo unauma, lakini hana namna na hivyo akawataka Watanzania kumuunga mkono na kumuombea. Anasema wakati wa kampeni, alilalamikiwa sana na masuala mbalimbali hasa rushwa na ufisadi ambao wananchi walionesha hisia zao namna wanavyochukia. Dk Magufuli amesema ataziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali kwa kuanza na kupunguza safari za watumishi zisizo na lazima nje ya nchi na badala yake atatumia mabalozi na ikilazimika, kiongozi hatakwenda na misururu ya watu. Dk Magufuli pia alitoa onyo kwa viongozi atakaowateua, kukumbuka kwamba anayo mamlaka ya kuwawajibisha akibaini wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, kwani atawatimua mara moja na baada ya hapo hatua za kisheria zitafuata. Alisema Watanzania wana maisha ya chini na wameshindwa kunufaika na rasilimali zao, wakati nchi yao ni tajiri hivyo Serikali itafuatilia mienendo ya watendaji wake na wakibainika kuwa na vitendo hivyo, watachukua hatua katika ngazi zote. Kuhusu Katiba mpya, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekuta kiporo cha katiba ambacho hakikukamilika kuandikwa, kutokana na kuchelewa kwa suala la kuandikishwa wapigakura na kwa kuthamini haki ya wananchi waliotoa maoni yao ya katiba mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Bunge la Katiba, serikali yake itatekeleza wajibu wake. Rais Magufuli pia alizungumzia kuimarisha misingi imara ya kiuchumi kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara za mikoa, wilaya na katika maeneo muhimu. Alisema uboreshaji wa barabara, bandari utafanyika pamoja na ujenzi wa reli mpya kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam- Tabora-Kigoma hadi Mwanza na Uvinza –Burundi, Mtwara-Songea- Bambabay na kwingineko. Akizungumzia suala la madini, maliasili na gesi asilia, alisema yatatumika kwa manufaa ya Taifa kwa kuzingatia sheria na taratibu huku akipongeza Sheria Mpya ya Usimamizi wa Mapato ya Gesi iliyopitishwa na Bunge la 10. Hayo ni machache kati ya mengi aliyozungumza kwenye hotuba yake. Lakini kinachotakiwa kwetu sisi wananchi na viongozi wetu, si kuendelea tu kusifia hotuba hiyo na mambo anayoyafanya bali kuchapa kazi kwa dhati na kusaidia juhudi za kurejesha uwajibakaji, uzalendo kwa nchi yetu na kuchukia rushwa na ufisadi.

Add a comment

CCM na furaha ya kutwaa majimbo

KATIKA mfumo wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi hakuna chama chochote chenye hati miliki na jimbo la uchaguzi hivyo ni wajibu wa kila chama kutumia ushawishi katika uchaguzi wenye ushindani ili kuhakikisha kinapata ushindi kwa njia halali katika uchaguzi huru na wa haki. Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni umedhihirisha hali hiyo baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mwanza kushinda katika majimbo ya Ilemela na Nyamagana yaliyokuwa yamechukuliwa na upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Add a comment

Papa Francis aleta ujumbe kwa jamii zenye shida

HATIMAYE Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ametimiza ndoto yake aliyoigusa Mei mwaka huu ya kutaka kuzuru Afrika, baada ya katikati ya wiki iliyopita kukanyaga ardhi ya Kenya kuanza ziara yake ya kiserikali na kichungaji kwa nchi tatu za Bara la Afrika. Kwa ujio wake mwaka huu, anafanya Afrika Mashariki kuwa na baraka za kipapa mara tatu katika kipindi cha miaka 50 tangu kujitawala kwa nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania.

Add a comment

Ukeketaji ni mila yenye madhara mengi

JUMATANO wiki iliyopita, wanaharakati kutoka taasisi mbalimbali waliandamana kuanzia Uzuri Sinza hadi ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Wakati hayo yakifanyika Dar es Salaam, Shirika la Plan International lilikuwa limejichimbia wilayani Tarime mkoani Mara likifanya kampeni dhidi ya mila ya ukeketeaji, ambayo pia inatajwa kuwa moja ya ukatili wa kijinsia.

Add a comment

Funguka, chukua hatua kumlinda mtoto apate elimu

WIKI iliyopita, Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) lilizindua siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zinazoendelea hadi leo. Moja ya mambo yaliyohimizwa katika uzinduzi huo, ni uwepo wa mazingira bora kwa mtoto nyumbani na shuleni. Siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia hufanyika kila mwaka kwa kushirikisha wadau mbalimbali ambao wote kwa pamoja wanatetea haki za watoto na wanawake.

Add a comment

Kumekucha mbio za Karatu 2015

MSIMU mwingine wa tamasha la michezo la Karatu umewadia, ambapo mwaka huu kilele chake kinatarajia kuwa, Desemba 19 katika viwanja vya Mazingira Bora mjini humo. Ni msimu wa michezo wa mwisho wa mwaka, ambapo hufanyika tamasha la aina yake linahusisha michezo kibao na hivyo kutofautisha na mashindano au matamasha mengine.

Add a comment