Ongezeko la watu, mifugo ni changamoto

SERIKALI imesema kasi ya ongezeko la idadi ya watu na mifugo, ikilinganishwa na upatikanaji wa ardhi iliyopangwa na kupimwa ni moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi nchini. Kutokana na hilo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi.

Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi alisema hayo juzi bungeni mjini hapa wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2016/2017. Lukuvi alizitaja changamoto nyingine kuwa ni uratibu wa utekelezaji kazi za sekta ya ardhi inayosimamiwa na mamlaka zaidi ya moja, hivyo kupeleka kuibuka migogoro baina ya watumiaji ardhi.

Nyingine ni uhaba wa wataalamu na vitendea kazi vinavyohitajika ili kukidhi utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi na ucheleweshaji ulipaji wa fidia stahiki kwa ardhi iliyotwaliwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

“Uelewa mdogo wa wananchi kuhusu sera na sheria za ardhi unapelekea wananchi kuvamia maeneo yasiyo yao,” alisema Lukuvi. Akielezea mikakati ya kukabili changamoto hizo, alisema wizara kwa kushirikiana na halmashauri itaendelea kuhakiki viwanja na mashamba ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu, k uyafutia miliki na kuyapangia matumizi mengine.

Kuhusu uhaba wa wataalamu na vitendea kazi, alisema serikali itaishirikisha sekta binafsi chini ya uratibu wa ubia katika utekelezaji wa sekta ya ardhi. “Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tamisemi inaandaa utaratibu wa kuzishirikisha kampuni binafsi katika urasimishaji wa maeneo yasiyopangwa katika halmashauri nchini,” alieleza.

Ili kuziba mianya inayosababishwa na migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji, alisema serikali kwa kushirikiana na wadau, inafanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ardhi 1995 kwa lengo la kuiboresha iende sawia na mahitaji ya sasa ya jamii.

“Kuhusu uelewa mdogo wa wananchi juu ya sera na sheria za ardhi, wizara itaendelea kuelimisha umma kuhusu sera, sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta ya ardhi,” alisema Lukuvi.