'HabariLeo msiache habari za Zanzibar'

SAID Omar Mohamed, ni wakala wa muda mrefu wa magazeti mbali mbali visiwani Zanzibar ambaye pia hulipokea na kulisambaza gazeti la Habarileo. Anapoulizwa kulizungumzia kwa maneno machache gazeti hili, anasema:

"Ni gazeti lenye mvuto na muonekano mzuri mbele ya wasomaji. Kikubwa linaandika habari za kweli."

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili katika mahojiano, Omar mwenye umri wa miaka 41 anautaka uongozi wa gazeti la HabariLeo pamoja na waandishi kuzipa kipaumbele habari zinazotoka Zanzibar ikiwemo za kisiasa ambazo anasema ndizo 'zinazouza' zaidi gazeti katika eneo hili la muungano.

Anasema wakati umefika kwa habari zinazotoka Unguja na Pemba kupewa kipaumbele ikiwemo kuwekwa katika kurasa za mbele sambamba na kutenga ukurasa maalumu.

Kadhalika anawataka waandishi wa HabariLeo kuandika kwa wingi habari za vijijini ili watu waliopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufahamu kinachoendelea visiwani humo.

Anasema ni vyema waandishi wakajua kwamba wananchi wengi wenye asili ya Zanzibar waliopo katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara, wangependa pia kujua mambo mbali mbali yanayotokea Zanzibar.

"Ili gazeti la Habarileo liweze kukubalika zaidi katika soko la biashara, basi ni vyema lizidishe kuandika habari zinazotoka Unguja na Pemba... Nashauri habari za visiwani ziandikwe kwa kina zaidi na wasomaji waliopo Bara wazipate kwa kina na kuzifahamu," anasema.

Anazidi kutoa ushauri wake kwa uongozi na Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) unaozalisha gazeti hili pamoja na la Kiingereza la Daily News sambamba na la michezo la SpotiLeo kuhakikisha wanafikisha magazeti sokoni mapema.

"Tatizo ninaloliona ni kwamba magazeti ya kampuni ya TSN yanachelewa kuingia sokoni... Unaona tumemaliza kugawa magazeti na sasa yanaingia mitaani lakini magazeti ya HabariLeo na Daily News hayapo. Hili ni tatizo kubwa," anasema.

Hata hivyo, Omar anaupongeza uongozi wa kampuni ya TSN kwa kutoa kamisheni nzuri kwa wauzaji wa gazeti hilo kuliko makampuni mengine ya kusambaza magazeti, hatua ambayo anasema inawapa nguvu na moyo wa kuchangamkia kuuza magazeti hayo.

"Kwa hili tunaupongeza sana uongozi wa kampuni ya magazeti ya TSN kwa kuwajali wauzaji wa magazeti yake na sisi ndiyo maana tupo tayari kuhakikisha gazeti hilo linauzwa na hapa ndiyo maana tunatoa maoni yetu ambayo tunataka yafanyiwe kazi kwa sababu gazeti ni zuri sana," anasema akitoa mchango wake katika kuadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa gazeti hili.

Waziri asiye na Wizara maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Juma Khatib, kwa upande wake analipongeza gazeti hili kwa kutimiza umri wa miaka kumi. Anasema, kwa mtazamo wake analiona HabariLeo limepiga hatua kubwa ikiwemo kuandika taarifa mbali mbali za vijijini.

Hata hivyo, anataka habari za wajasiriamali pamoja na vikundi vya ushirika, hususani akinamama, kuandikwa zaidi ili kuwasaidia kupata mbinu za kujinasua na hali ngumu ya uchumi.

"Sina tatizo na taarifa za gazeti la Habarileo, wamekuwa wakiandika taarifa zetu sisi wanasiasa kwa uhakika... Sasa wanatakiwa kuelekeza nguvu zao kuandika taarifa za vijijini ikiwemo za wajasiriamali na makundi ya wanawake," anasema Khatib ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa chama cha Ada-Tadea.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani akizungumza na gazeti hili huko Vuga, Mji Mkongwe wa Zanzibar analipongeza HabariLeo kwa kuwa miongoni mwa magazeti machache nchini yenye kuandika habari zenye kuzingatia weledi wa taaluma ya uandishi wa habari bila ya kukanushwa kanushwa na wahusika.

"Sijasikia habari zinazoandikwa na gazeti la HabariLeo kukanushwa au za uongo kiasi ya kutishiwa kufikishwa mahakamani kama ilivyo kwa magazeti mengine," anasema.

Hata hivyo anautaka uongozi wa gazeti la Habarileo kuandika habari mbalimbali zinazohusu jamii pamoja na vyama vya siasa ikiwemo vya upinzani kwa sababu ni gazeti la serikali linalopaswa kuhudumia watu wote.

"Bado habari za vyama vya upinzani ikiwemo CUF haziandikwi kwa kina na zikiandikwa wakati mwingine inakuwa kama kwa bahati mbaya sana," anasema na kuahidi kutoa habari kwa gazeti hilo pale anapotafutwa.

Parmukhi Hoogan Sikh ni mbunge mstaafu maarufu kwa jina la ‘Singasinga’ ambaye alichangia na kutoa maoni yake wakati wa kuanzishwa kwa gazeti hilo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano Dodoma mwaka 2006. Yeye anasema gazeti la HabariLeo ni mdomo wa Serikali kwa hivyo linatakiwa kufanya kazi huku likizingatia maadili pamoja na matakwa ya Serikali.

"Sisi wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano tuliunga mkono kuanzishwa kwa gazeti hilo wakati tukipewa taarifa mbele ya Bunge ambapo tuliutaka uongozi wa gazeti kuzingatia weledi na maadili ya taaluma.Tulitaka gazeti liripoti matukio mbali mbali yenye maslahi ya wananchi wetu pamoja na kero zao," anasema na kusema kwa kiwango kikubwa gazeti hilo limekuwa likitekeleza maelekezo hayo ya wabunge.

Waride Bakari Jabu ni katibu wa kamati maalumu ya Halmashauri kuu ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi na Uenezi.

Yeye analitaja HabariLeo kuwa ni moja ya tegemeo la wananchi katika kusoma habari mbalimbali zenye ukweli katika mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mimi nikiwa nashughulikia masuala ya siasa na mawasiliano ya umma katika Chama Cha Mapinduzi, kwa ufupi tumeridhishwa na jinsi gazeti la HabariLeo linavyofanya kazi zake za kuhabarisha jamii kwa kuripoti taarifa mbali mbali ikiwemo za serikali pamoja na chama tawala hadi upinzani ambapo tuliona hali hiyo wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana," anasema.

Ali Issa ni mmoja ya wauzaji wa magazeti ambaye hutumia baiskeli kutembeza magazeti na kuuza katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Yeye anasema gazeti la HabariLeo limeanza kuzoeleka na kukubalika na wasomaji mbalimbali kutokana na taarifa zake zinazoandikwa kukubalika zikiwa zimesheheni mambo mbalimbali ya nchi kiasi cha kuonekana kwamba ni gazeti la kitaifa.

"Kadri siku zinavyokwenda HabariLeo limekuwa likipata wasomaji ambao hupenda kulinunua kwa ajili ya kupata habari nyingi zenye mchanganyiko... Lakini ninawaomba wahusika waongeze juhudi kwa kuandika zaidi habari za kijamii na siasa," anasema.