Utalii wasonga mbele Zanzibar

"JAMANI, hicho chumba kinakaa vipi? Lakini kiko kweli?" Swali kama hilo ama linalotaka kujua mtu anavutaje hewa akiwa kwenye chumba kilichojengwa chini ya bahari yaliulizwa sana wakati wa uwekaji wa jiwe la nanga la chumba hicho katika hoteli ya Manta Resort iliyopo umbali wa takribani kilomita 50 kutoka mji wa Chake Chake, Pemba.

Manta Resort ni hoteli ya kitalii iliyopo kijiji cha Mkangale Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Wenyeji na walioshuhudia uzinduzi wa chumba hicho, awali hawakuamini na hivyo kuuliza maswali mengi.

Wapo waliodiriki kusema, kuwa tokea milango ya biashara huria kufunguliwa, iliyotokana na Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, sasa kila kitu kinawezekana na kila jambo la maendeleo litawasili Zanzibar kama zilivyo nchini nyingine.

Siku ya uzinduzi wa chumba hicho ilikuwa ni wakati wa kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi, ambapo wananchi wengi walifurika huku wakimsumbiri mgeni rasmi aliyepangwa kuweka jiwe la nanga la chumba hicho (under water room) ambae alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi. Kubwa walilosubiri si hotuba bali kujua chumba hicho cha kitalii kikoje hasa.

Maswali yalijibiwa na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbaruok.

Alisema umbali wa chumba hicho kutoka kwenye ufukwe ni kama mita 300, sawa na viwanja vitatu vya mpira wa miguu.

Alisema ujenzi wa chumba hicho ni ishara ya kupevuka na kutanuka kwa sekta ya utalii na kwamba chumba hicho kina hewa ya kutosha hata kama kiko chini ya bahari.

"Hiki chumba, nasema kimeanza kufungua milango kwa watalii wakubwa na wa juu wakiwemo matajiri wakubwa duniani, maana sasa akina Bill Gates (tajiri mkubwa duniani) wakija watapata sehemu ya kiutalii kwa mujibu wa hadhi na fedha zao,’’ anasema Mkuu wa Kamisheni ya Utalii Pemba, Suleiman Amour.

Leo, wakati tukisherehekea miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, utalii katika kisiwa cha Pemba umezidi kuimarika huku chumba hicho cha chini ya bahari kinachotimiza miaka mitatu kikizidi kuwa kivutio cha watalii wengi.

Chumba hicho cha chini ya bahari, ni cha kwanza duniani kwa upande wa bahari, lakini ni cha pili, baada ya kile kilichoko nchini Sweden lakini kikiwa kwenye ziwa la maji baridi.

Hapa sasa ndio unapoona umuhimu wa kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambayo leo hii yamebadilisha sura ya kila kona na vichochoro mbalimbali katika visiwa vya Unguja na Pemba. Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume alipata kusema maeneo haya Januari 12, mwaka 1964:

“Leo ndugu wananchi tumeshajikomboa, na kila mmoja wetu nitahakikisha atakaa na kuishi kwa mazingira bora, na sasa hakuna tena kutawaliwa.’’

Na kweli, pamoja na changamoto mbalimbali, miaka 53 baada ya uhuru, Kisiwa cha Pemba kinazidi kung’ara kwa utalii unakua na hivyo kutoa ajira kwa wananchi kila uchapo.

Tukirudi kwenye chumba hicho cha chini ya bahari, kutokana na upekee wake katika bara la Afrika kimeendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na nje. Meneja wa hoteli ya Manta resort, Matthew Saus kutoka Sweden, anasema kuwa ujenzi wa chumba hicho umegharimu kiasi cha dola laki tano za Marekani.

"Mimi na mwenzangu tulifika Pemba miaka kumi iliyopita, na tukaanza harakati za kujenga chumba cha chini ya bahari, na taasisi kadhaa zilitukubalia," anasema.

Unapokuwa kwenye chumba hicho ukiwa umelala au unajipatia chakula, samaki wa aina mbalimbali watakuwa wanakupita kwa karibu sana na unaweza kutamani kuwagusa lakini unazuiwa na viambaza maalumu vya chumba hicho kilicho mitihili ya kioo kigumu cha plastiki.

Chumba hicho inaelezwa kwamba kinatumia umeme wa jua ili kuwapa mwangaza wa kutosha wapendwa wanapokuwa chini ya maji ya bahari.

Ni chumba ambacho kwa juu ni mithili ya boya ambalo lina umbile la mlango wa nyumba ya kawaida, hivyo unaweza kuingia humo kwa njia ya kushuka ngazi hadi chini na ukiwa ndani ya chumba hicho unakuwa na uwezo wa kuona umbali wa mita 100 ndani ya maji, huku samaki na bustani ya bahari ikiwa ndio bustani yako.

Imekuwa ikielezwa kwamba mwekezaji huyo ana nia ya kuongeza idadi ya vyumba vya aina hiyo katika eneo hilo, iwapo hicho cha mwanzo ambacho ni cha majaribio kitafanikiwa vizuri.

Gharama ya kukaa kwa usiku mmoja kwenye chumba hicho, kwa mujibu wa meneja wa hoteli hiyo ni Sh 3,270,000.

Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakitaka gharama ziwe chini kwa ajili ya kuvutia watalii wa ndani kwenda kuvinjari kwenye chumba hicho cha chini ya bahari.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis, hakosi cha kusema juu ya chumba hicho.

Yeye anawataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano mwekezaji huyo ambaye mbali na kulipa kodi ya serikali pia anatoa ajira kwa wananchi.

Asha Ali Omar wa Makangale, anasema uwepo wa chumba hicho cha chini ya ardhi, kunadhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

“Leo tunapoadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar, mimi binafsi ninajionea namna utalii ulivyotanua mbawa zake," anasema.

Muhidini Makame Haji wa Mchanga mdogo, anasema hakuna mwananchi wala kiongozi wa Zanzibar, ambae hajanufaika na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

“Kila mmoja leo hii hakuna ambae hajala keki ya taifa, iwe kwenye utalii, afya, elimu au miundombinu ya barabara,’’ anasema.

Anaishauri serikali kila atakayebeza Mapinduzi ya Zanzibar kwa njia moja ama nyengine, ni vyema akashughulikiwa maana, atakuwa mpinga maendeleo.