Utalii ni mambo yote Zanzibar

VIVUTIO vya utalii vya asili au vilivyotengenezwa na binadamu vimeendelea kuwa chachu ya mafanikio ya utalii katikia visiwa hivi. Moja ya vitu vinavyoifanya Zanzibar izidi kushamiri kiutalii ni fukwe zake, misitu ya asili ikiwa na viumbe adimu kama kima punju, mji mkongwe, jengo la maajabu na mengi mengineyo.

Zanzibar pia inajivunia usanii wa asili uliotumika kwenye majengo yake, hususani kwenye milango. Pia visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na aina mbalimbali ya viungo na matunda, vitu vinavyopatikana kwa miaka yote, sambamba na utamaduni wa ukarimu wa Wazanzibari kwa wageni.

Vivutio vinavyotokana na bahari pia vipo tele. Lakini kwa bahati mbaya bado havijaendelezwa kikamilifu na hivyo kutotoa upinzani wa kutosha kama ilivyo kwa visiwa vingine vidogo vya Mauritius na Ushelisheli ambako wamefanikiwa zaidi katika utalii wa majini.

Mtazamo wa kisera uliopo ni kuboresha utalii kwa kuufanya kuwa endelevu na ambao unazingatia uharibifu wa mazingira, bayoanuai na ambao ni rafiki wa tamaduni za watu wa Zanziba lakini unaochochea uchumi kwa maana ya kuifanya Zanzibar kuwa kvutio ziaidi cha utalii duniani.

Pia sera zilizopo zinalenga katika kuongeza zaidi vivutio vya utalii. Hii ni pamoja na kuimarisha fukwe, vivutio vya kiutamaduni na kuwa makini katika suala zima la kusaka masoko.

Dira ya 2020 inahimiza wawekezaji wa ndani kuingia ubia na wale wanaotoka ughaibuni ili kusaidia katika kuvifanya visiwa hivi kuwa na vivutio zaidi vya utalii kulinganisha na maeneo mengine duniani.

Katika siku za karibuni, utalii wa Zanzibar umezidi pia kuimarika kutokana na ujenzi wa barabara za lami.

Kwa sasa vituo vingi vya utalii vimeunganishwa na barabara imara zilizojengwa katika miaka ya karibuni. Halikadhalika, vituo vingi vya utalii, vina vyumba vya kisasa na mahoteli na hivyo kuzidi kuwa sababu ya 'kuwashika' watalii.

Zaidi ya hayo, watalii wanaofika Zanzibar wamekuwa wakifurahia mchanga mweupe wa fukweni, mabawa ya kuogolea, kupiga mbizi na kupata chakula kitamu cha aina mbalimbali.

Baadhi ya maeneo yanayovutia watalii wengi wanaofika Zanzibar ni pamoja na Kiwengwa, Nungwi na Paje.

Leo tunaposherehekea miaka 53 ya Mapinduzi, Zanzibar ina hoteli zaidi ya 140 zenye hadhi tofauti huku zikitoa huduma bora kwa gharama za wastani.

Takwimu kutoka Wizara ya Fedha, na wizara ya utalii zinaonesha kuwa utalii inachangia asilimia 25-27 ya pato la visiwa hivi (GDP), na pia kuingiza kati ya asilimia 70 hadi 85 ya fedha za kigeni.

Sekta ya Utalii imekuwa ikikua kwa kasi na biashara nyingi Zanzibar kwa sasa hutegemea watalii. Baadhi ya biashara hizo ni pamoja na wachuuzi wa samaki, wajasiriamali, benki au maduka ya kubadilishia fedha, maduka ya vyakula, migahawa, waongoza watalii, kumbi za burudani na sekta ya usafiri.

Sekta ya biashara na mashirika ya umma yamekuwa yakizidi kufaidika kiuchumi kutokana na utalii, kuanzia ngazi ya taifa hadi ya mtu mmoja mmoja ikiwa ni pamoja na wakulima na hata mama lishe.

Hii inatokana na ukweli kwamba wapo baadhi ya watalii wanaopendelea kula kwa mama lishe. Kimsingi utalii unatoa faida kwa shughuli nyingi za kiuchumi visiwani hata kama siyo faida ya moja kwa moja.

Wizara ya Kazi na Utumishi wa Umma inakadiria kuwa takribani watu 40,000 wameajiriwa katika sekta ya utalii visiwani.

Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Said Ali Mbarouk anasema kwamba hatua ya kuanzisha taasisi zinazoshughulika na Utalii ni ushahidi mwingine wa kuonesha kwamba sekta hiyo inakuwa kwa kasi visiwani.

Anazitaji taasisi hizo kuwa ni pamoja na Shirika la Utalii Zanzibar (ZTC), Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (Zati) na Chama Cha watendaji kwenye sekta ya utalii (Zato). Vyama hivyo vyote vinalenga katika kukuza utalii sambamba na kuutangaza kwa ajili ya kuboresha miundombinu na huduma.