Mapinduzi ni fahari ya Mzanzibari, unayasusiaje?

LEO wananchi wa Zanzibar sambamba na wenzao wa Bara wanaungana kuadhimisha miaka 53 ya kumbukumbu ya Mapinduzi Matukufu Zanzibar ya mwaka 1964. Sherehe za Mapinduzi huadhimishwa Januari 12 kila mwaka, kwa lengo la kutunza historia hii adhimu na pia kukifahamisha kizazi cha sasa Zanzibar ilipotoka, ilipo sasa na inakokwenda.

Sherehe hizo pia zimekuwa zikitumika mara kwa mara kwa ajili ya ufunguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Kabla ya Mapinduzi hayo, Wazanzibari walitawaliwa na mataifa mbalimbali wakiwamo Waarabu, Wajerumani na Waingereza.

Watu weusi waliwekwa katika daraja la chini ambapo walidharauliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa wakiwa ndani ya nchi yao wenyewe.

Baada ya kupigania uhuru kwa muda mrefu bila kupewa, Waingereza waliamua kutoa uhuru kwa Sultani aliyekuwa akitawala Zanzibar. Kitendo hicho kilisababisha Wazanzibari wengi kuendelea kukosa uhuru kamili kwa kuwa uongozi wa Kisultani uliendelea kuwaweka waafrika katika daraja la chini.

Mpango wa Mapinduzi ulifanikiwa siku kama ya leo mwaka 1964 na hivyo kuung'oa utawala wa Kisutani na kisha wananchi walio wengi, wakashika hatamu ya kuongoza dola, chini ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume.

Mapinduzi ya Zanzibar ni tukio muhimu ambalo wananchi wanapaswa kulikumbuka na kujivunia kwani kuanzia mwaka 1964 Wazanzibari wamekuwa huru katika nchi yao, wakijipangia mambo yao wenyewe kwa ajili ya maendeleo yao.

Haki zote ambazo wananchi wazalendo walistahiki kuzipata ikiwemo elimu, matibabu na matumizi ya ardhi kwa kilimo na makazi ambavyo walinyimwa na utawala dhalimu wa Kisultani sasa wakawa wanazipta kutokana na mapinduzi hayo.

Kwa lugha rahisi, ni mapinduzi hayo ndiyo yaliyomrejeshea haki mwafrika, haki ambayo aliyo nayo hadi leo ikiwemo kuunda chama cha siasa na kujiendeleza kadri anavyoweza.

Ni mapinduzi yaliyokuwa pia chanzo cha Zanzibar kuungana na Tanganyika na kuzaliwa Tanzania. Ni vigumu mtu kupata picha hali ingelikuwaje kuhusu muungano kama Sultani angeendelea kutawala visiwa vya Zanzibar.

Pamoja na umuhimu wa mapinduzi haya yaliyomrejeshea Mzanzibari uhuru wake alionao leo pamoja na haki yake kama mkazi halali wa visiwa hivi, mwaka jana wakati wa kuadhimisha miaka 52 wa mapinduzi hayo wapinzani, hususani Chama cha Wananchi (CUF) walisusa.

Kinachoonekana mtindo ni huohuo hata mwaka huu.

Huko nyuma pia, kabla ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, CUF walikuwa na kawaida ya kukisusa pia sherehe za kuadhimisha mapinduzi haya matukufu.

Lakini kitu ambacho kimekuwa kikiwashangaza wengi ni CUF kuchukia hata kutamka neno "Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar" au kwa kufupi "SMZ".

Mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kwamba kwa muda mrefu viongozi wa CUF walikuwa wakipinga neno SMZ lisitumike kwa kile alichosema ni kama wanachukizwa na mapinduzi! “Viongozi wa chama hicho kwa muda mrefu walikuwa wakipata kigugumizi kuyatambua mapinduzi hayo kiasi cha baadhi yao kudiriki kusema kwamba eti yalikuwa ni ya umwagaji wa damu,” alisema Vuai.

Vuai alifika mbali na kuonya kwamba inaonekana siku CUF wakichukua uongozi wa dola, upo uwezekano wa kufuta sherehe hizo moja kwa moja.

Lakini kwa upande wake, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa chama cha upinzani cha AFP, Said Soud amekuwa akisema kwamba sherehe za mapinduzi ni za kitaifa na hazipaswi kuhusishwa na itikadi ya vyama vya siasa.

Soud aliwahi kukaririwa akisema kwamba sherehe hizo ni utambulisho wa wananchi wa Zanzibar walivyojikomboa kutoka kwenye utawala wa Kisultani kwa hivyo zinatakiwa kuenziwa na kutunzwa na sio kubezwa au kususwa kama wanavyofanya wanasiasa wengine.

Kama ambavyo wamekuwa wakisema watu wengi, Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ni fahari ya wananchi wa Zanzibar kama wanavyofanya nchi nyingine ambazo hutumia fedha nyingi kusherehekea siku ya kujiondoa kwenye minyooro ya ukoloni.

Lakini pia, kama ilivyodokezwa hapo juu ni kuwakumbusha vijana wafahamu wapo wapi na wanatoka wapi. Inawezekana CUF wakawa na hasira zao kutokana na kufutwa kwa uchaguzi wa mwaka juzi, lakini ilikuwa busara kushiriki katika maadhimisho ya mapinduzi haya kwa kuwa ni fahari ya Wazanzibari wote (na hata Watanzania wote) bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Kumekuwepo pia na madai kwamba wapo viongozi wa CUF wasiyoyatambua Mapinduzi ya Zanzibar isipokuwa wanautambua Uhuru wa Desemba 1963 uliotolewa na Uingereza kwa Sultani. Inashangaza sana mzalendo anapotambua uhuru wa aina hii ambao kimsingi haukuwa na lengo la kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar isipokuwa kundi la wachache akiwemo Mwingereza mwenyewe kupitia kibaraka wake, yaani Sultani.

Hali hii ndio imekuwa ikiwafanya baadhi ya watu kutoa madai kuwa kuna viongozi wanaotamani kuona Sultani anarudi kwa mlango wa nyuma kutawala Zanzibar.

Hivyo ni vyema, CUF wakaacha siasa za chuki na wakawa wanashiriki katika matukio kama haya ya kitaifa, hali ambayo inaweza pia kusaidia kurahisisha mazungumzo ya kusaka mwafaka.