DIT yafunga kamera ‘kiboko’
- In Makala
- Post 13 Septemba 2012
- By Magnus Mahenge
- Imesomwa mara: 898
TAASISI ya Teknolojia Dar es (Salaam), kupitia idara zake mbalimbali, imetoa mchango mkubwa katika ugunduzi, uvumbuzi na uendelezaji vipaji vya nchini.
Jopo la wahadhiri wa Idara ya Kompyuta na wasaidizi wao kwa pamoja wamefanya ugunduzi, uvumbuzi na ubunifu wa mifumo rahisi na mifumo ya kutumia kompyuta katika kuendesha au kukusanya taarifa mbalimbali.
Idara ya kompyuta chini ya mkuu wake, Nkundwe Mwasaga, imekuwa kinara katika uvumbuzi wa miradi mbalimbali na imekuwa chachu ya mafunzo ya teknolojia nchini. Katika mahojiano na Habari- Leo, Mwasaga anasema, idara yake kimekuwa chanzo kizuri cha ubunifu, uvumbuzi na utumiaji teknolojia katika kuendesha mifumo mbalimbali ya mawasiliano.
Mifumo ya mawasiliano na ukusanyaji habari imekuwa ikibuniwa na wahadhiri na kutekelezwa na wanafunzi ambao wamekuwa wakiibuka na matokeo mazuri. Mhadhiri Msaidizi Emmanuel Kondela anasema katika siku za hivi karibuni, taasisi hiyo imeendesha miradi miwili ya ubunifu wa mifumo rahisi ya kiteknolojia.
Mmoja kati ya miradi hiyo ya kuunda mifumo rahisi, ni wa kuweka vifaa vya kuongozea taa za barabarani. Kifaa hicho ni msaada mkubwa katika kupanga, kuruhusu na kugawa muda wa kuruhusu magari. Kifaa hicho ni mkusanyiko wa mashine rahisi nyingi zenye mchanganyiko wa matumizi na ukusanyaji taarifa ya magari na kuyapanga, kuyaratibu na kuyaingiza katika mfumo wa kompyuta.
Mmoja wa wahadhiri wa chuo hicho, Portin Ng’imba na Stanley Mwalembe kwa nyakati tofauti wanasema, mashine hizo zilizofungwa kwenye taa mbalimbali za kuongozea magari jijini Dar es Salaam, zinaweza kutumika ama kufungwa katika majiji mengine makubwa kama Mbeya, Arusha, Mwanza na Tanga na miji mingine.
Vifaa hivyo vya kuongozea magari vimefanyiwa majaribio tangu mwaka 2001 na kuboreshwa mwaka 2008 na kuonesha mafanikio mazuri. Vifaa hivyo vimefungwa kwenye muunganiko wa barabara za Lumumba na Morogoro, Uhuru na Bibi Titi, Co-cups na Kamata na eneo la Palm Beach.
Maeneo mengine ni Daraja la Selander, Kinondoni na Ali Hassan Mwinyi, Umoja wa Mataifa na Morogoro, eneo la Serena Hoteli na maeneo mengine. Vifaa hivyo ambavyo vinafuta matumizi ya kizamani ya kuongoza magari kwa kuratibu kienyeji, vimekuwa msaada mkubwa kwa magari na watumiaji wake.
Ubunifu huo umeingiza teknolojia ya matumizi ya mashine za uongozaji taa barabarani na kuendana na nchi nyingine duniani zilizoendelea. Vifaa hivyo vinaongoza magari, vinaongozwa na kuratibiwa kupitia mfumo wa kompyuta ambao unajirekebisha wenyewe na kupanga matumizi kadiri ya wingi wa magari.
Mfumo huo wa mashine hizo, unaruhusu kuongeza muda wa magari kupita nyakati za asubuhi na jioni kutokana na wingi wa magari lakini unapunguza muda mchana. Mashine hizo zimewekwa kwenye nguzo zilizopakwa rangi ya njano na nyeusi, tofauti na zile za zamani ambazo ziliwekwa kwenye miti yenye rangi ya silva.
Mkuu wa Idara ya Kompyuta, Mwasaga anasema, zimewekwa kwenye rangi hizo si kwa bahati mbaya bali zinasaidia kuonesha magari hata kama mvua inanyesha. Katika kuongeza vifaa hivyo katika maeneo mengine jijini na miji mingine, Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wana wajibu wa kuwasiliana na DIT ambayo ipo tayari kuendelea kupanua huduma hiyo.
Vifaa vya kuongozea magari, vinasaidia kuonesha magari katika njia zote nne au zaidi kwa muda wake na kwa muda mrefu kutokana na wingi wa magari. Kifaa hicho kinaongozwa na mashine maalumu inayoratibu na kudhibiti moja kwa moja, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo trafiki wa waliratibu upishanaji magari kwenye viunganishi kwa kutumia mikono.
Mtambo wa mashine hizo ndogo unakuwa na chipu ndani yake ambayo ikitolewa inaweza kuingizwa kwenye kompyuta na kuonesha matukio ya mwendo na uratibu wa magari yaliyotukia barabarani hapo.
Mhadhiri Msaidizi, Haji Fimbombaya anasema, mashine za kuongozea taa barabarani ni muhimu sana jijini, zimefungwa kifaa hicho ambacho kinajipanga chenyewe namna ya kuruhusu magari mengi kadiri ya wingi wa magari ya njia hiyo.
Kifaa hicho kinasaidia pia kuangalia mwendo wa magari kwenye barabara hasa katika maeneo hayo yanapopishana. Mfumo huo wa kuratibu mwendo wa magari barabarani, unajibadili wenyewe kwa kuongozwa na kuratibiwa na kompyuta ambazo zinafanya kazi saa zote.
Vifaa hivyo vya kuongozea magari barabarani, vimeongezewa ubora kwa kufungwa kamera ambazo ni rasmi kwa kutoa taarifa ya matukio yanayokea katika eneo hilo. Kwa majaribio, mradi huo wa kufunga kamera umefanyika katika eneo la Kamata, Dar es Salaam. Kamera hiyo inakusanya taarifa na matukio yote katika eneo hilo.
Kamera hiyo, ni msaada mkubwa kwa raia na hasa polisi katika kusaidia kubaini wanaofanya makosa na wavunja sheria katika makutano hayo. Kamera hiyo inayofanya kazi kwa saa 24, inakusanya taarifa zote ambazo sasa zinaweza kurekodiwa na kutumika kubaini wahalifu.
Hadi sasa pamoja na kufungwa kamera hiyo, taarifa zake hazifiki Polisi kutokana na kutotandaza kebo za kusafirisha moja kwa moja habari za barabarani hadi kituo cha Polisi. Kamera hiyo inarekodi picha na sura ambazo kwa sasa zinaweza kurekodiwa kwenye chipu na kuonekana kupitia mtandao wa kompyuta.
Kufungwa kwa kamera hiyo kulifanyika kwa majaribio, lakini kumeonesha mafanikio makubwa. Kamera hiyo inafanya kazi tu kunapokuwapo na umeme, lakini si lazima uwe wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) tu, bali hata umeme wa sola, inveta na upepo.
Kamera hizo zitasaidia kupunguza makosa yanayotokea katika eneo hilo ambalo mara nyingi limekuwa miongoni mwa maeneo ya matukio mabaya. Ufungaji wa vifaa vya kuongozea magari sambamba na kamera, kupunguza misongamano lakini pia kunasaidia kuweka usalama wa abiria na mali zao.
Kamera hizo zinaweza kuwajua ni watu gani ambao watakuwa wanapita wakati taa nyekundu zinawaka badala ya mfumo wa sasa ambao watu wanaweza kuvuka. Uwekaji wa vifaa vya kuongozea magari na kufunga kamera kwa pamoja, kumesaidia kuhakikisha usalama wa magari na abiria.



