19Mei2013

 

Korogwe yabuni mikakati kukabili tatizo la mgawo wa dawa

HALMASHAURI ya wilaya ya Korogwe Vijijini imeanza kutekeleza mikakati inayohakikisha kwamba vituo vya kutolea huduma za Afya vinajitosheleza kwa dawa muhimu ili kupunguza tatizo la ukosefu wa muda mrefu la dawa kutoka Bohari Kuu (MSD).

Lengo la mikakati hiyo pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha vituo vyake vyote vya kutolea huduma vinajitosheleza kwa dawa, vitendanishi na vifaa tiba ili kukabiliana na changamoto ya sasa katika mfumo wa usambazaji ndani ya halmashauri hiyo.

Ukosefu wa dawa za MSD tayari umeathiri uendeshaji wa baadhi ya vituo vya huduma hasa zahanati zilizoko maeneo ya vijijini na kuvilazimu sasa kutegemea makusanyo hafifu ya fedha zitokanazo na malipo ya wateja wa papo kwa papo, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Bima ya Afya ya Taifa(NHIF).

Hata hivyo, utegemezi pekee na viwango vya malipo ya kati ya Sh 500 hadi Sh 2,000 na gharama za vipimo mbalimbali wanavyotozwa wateja wanaofika kila siku pamoja na michango ya wanachama wachache waliojiunga CHF au NHIF kamwe haviwezi kutosheleza mahitaji, hasa ikilinganishwa na idadi kubwa ya wagonjwa wakiwemo wazee, wanawake na watoto ambao wanategemea sana huduma za afya kutoka kwenye vituo hivyo vya serikali kwa kuwa wanapata msamaha au gharama za uchangiaji ni nafuu zaidi kuliko kwingine.

Kutojitosheleza ki huduma kwa zahanati na Vituo vya Afya ndani ya halmashauri hiyo kunawanyima haki wagonjwa hasa ambao hawana uwezo wa kuchangia papo kwa hapo wakati wanapougua kwa dharura ukilinganisha na wachache kati yao wanaomudu gharama za kutibiwa kwenye vituo binafsi au kununua dawa dukani.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini (DMO), Dk Rashid Said anakiri kwamba suala la upatikanaji usio wa uhakika wa dawa muhimu za MSD hasa kwa ajili ya kutibu magonjwa 10 sasa ni changamoto kwa jamii na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Korogwe kwa ujumla.

Anayataja magonjwa hayo ambayo ni malaria, kuharisha, homa ya mapafu, magonjwa ya njia ya hewa (ARI), minyoo ya tumbo, maambukizi ya njia ya mkojo, magonjwa ya macho, ngozi, upungufu wa damu na pumu ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayowasumbua wanajamii kwenye halmashauri hiyo.

“Ki msingi mfumo wa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu usioridhisha kutoka MSD umesababisha vituo vya huduma vya serikali vilivyoko chini ya halmashauri hii kushindwa kujitosheleza kwa dawa muhimu na vifaa tiba na kufanya wagonjwa kukosa imani navyo ki huduma”.

Dk Rashid anaeleza chanzo cha tatizo hilo ni kukosekana kwa mrejesho sahihi na kwa wakati kutoka MSD kuhusu tatizo linalosababisha upungufu endelevu wa dawa muhimu na kusema mpaka sasa hawajaamua kuwa wa kweli katika kuieleza jamii kwa usahihi kuhusu visababishi vya upungufu huo wa dawa unaoendelea.

Chanzo kingine cha tatizo anasema ni bajeti inayotengwa na serikali kwenda MSD kwa ajili ya kuzinunulia halmashauri dawa muhimu ambayo inalipwa kwa asilimia kati ya 50 na 60 bado ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi waliyonayo kwa mwaka.

“Hali hiyo inasababisha kutokuwemo kwa dawa tunazoahidiwa kupata kutoka huko MSD hususan kwa uwiano na mahitaji halisi ya kituo au ukilin- ganisha na yale magon- jwa kumi yanay- osumbua wateja kwenye eneo husika kwa kuwa sasa wanalazimika kusambaza kulingana na dawa walizonazo wao”.

Anaongeza; “Kwa hali halisi hivi sasa naweza kusema kwamba MSD imeshindwa kusambaza dawa kwa wakati na kusababisha ucheleweshaji katika utaratibu wake mzima wa mzunguko wa ugawaji wa dawa ambao unakawia kwa kati ya miezi 2 hadi 3 kwenda vituoni na hata wanapopeleka ni pungufu ikilinganishwa na kile ambacho waganga wameomba”.

Upungufu huo kwenye halmashauri hiyo anasema unajumuisha uhaba wa aina mbalimbali za vitendanishi, dawa za kutibu maradhi zikiwemo mseto zinazotibu ugonjwa wa malaria na zile za kuzuia wajawazito wasitoke damu nyingi wakati wa kujifungua.

Dk Rashid anasema upungufu mwingine mkubwa uko katika vifaa tiba, hasa nyuzi maalumu za kushonea majeraha makubwa au yaliyotokana na ajali, gozi/pamba zinazotumika kwenye vidonda vya operesheni, vifaa vya kutunzia damu, katheta, urine bud pamoja na POP kwa wateja wanaovunjika viungo.

“Wakati mwingine imetulazimu kuwaelekeza wagonjwa wakajinunulie dawa kwenye maduka binafsi ingawa halmashauri nayo tunajitahidi kutumia fedha za mfuko kununua dawa na vifaa lakini ki ukweli hazitoshelezi kumaliza tatizo la muda mrefu la ukosefu wa dawa kutoka huko MSD”, anaeleza.

Aidha, anasema waganga wafawidhi katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma mara kadhaa wanajikuta wakilazimika kutoa rufaa zisizo za lazima kwa wagonjwa kutokana na hali hiyo ya kukosekana matibabu sahihi ambayo yangeweza kupatikana kwa urahisi kwenye ngazi husika.

“Tunalazimika kumrifaa mgonjwa aliyetoka kwenye zahanati, Kituo cha Afya au Hospitali ya wilaya kwenda hospitali ya mkoa wakati mwingine hata kwa kukosa vifuko vya damu (blood bags) au POP ...kwa kweli hiyo ni kero kwetu watumishi na mteja pia”, anaeleza Dk Rashid.

Anasema kutokana na mapungufu hayo ambayo yanakwamisha juhudi za kufikisha huduma bora za Afya kwa wananchi ndipo halmashauri ya Korogwe Vijijini ikaamua kujiwekea mikakati ili kupunguza tatizo hilo haraka.

“Tumedhamiria kuongeza makusanyo ya kila kituo kupitia CHF, NHIF kwa kuhamasisha wanachama zaidi kujiunga lakini pia kuhakikisha wanachama hao wananufaika zaidi kwa kuwatengea dawa zao na kwa wale wa malipo ya papo kwa hapo nao kujumuisha malipo na michango hiyo kupunguza uhaba wa dawa uliopo ili kuwavuta wateja wengi zaidi”.

DMO huyo anasema hivi karibuni halmashauri ilitumia shilingi milioni 79 ambazo milioni 29 kati ya hizo zilikusanywa kupitia CHF na Sh milioni 50 ni za malipo ya papo kwa hapo zilizotumika kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba ili kusaidia kupunguza tatizo.

Pia anasema wamefanikiwa kuajiri kwa asilimia 95 watumishi wenye sifa kwa kada za Uganga na Uuguzi kwenye kila kituo cha huduma kama mbinu ya kurejesha imani ya wananchi kwenye vituo vya serikali ambapo hivi sasa mwamko umeongezeka kwa kuwa wananchi wana uhakika wa kupata ushauri sahihi wa kitabibu hata kama hakuna dawa.

Aidha anasema badala ya kusubiri mgawo pekee wa dawa za MSD tayari katika mwaka huu wa fedha halmashauri imejitahidi kuweka bajeti ya kutosha ya dawa kwa kuzingatia mipango kamambe ya halmashauri hiyo.

“Kwa mfano kwenye bajeti ya mwaka huu wa 2012/2013 asilimia 33.3 ambayo ni sawa na Sh 196,953,736 ya fedha za serikali tunaitumia kwenye ununuzi wa dawa muhimu ambapo msisitizo mkubwa wa matumizi ya hizo fedha zimepelekwa kwenye zahanati ili kuhakikisha huduma bora zinafika kwa walengwa”, anaeleza.

Anautaja mkakati mwingine wa kukabili tatizo la upatikanaji dawa kwenye halmashauri kwamba ni kuendelea kushirikiana na wadau wengine wanaosambaza dawa yakiwemo mashirika kama Aids Relief pamoja na madhehebu ya dini kutoka makanisa ya Katoliki na Anglikana.

Baadhi ya wanavijiji wakiwemo wa kata za Hale, Kwenango na Makuyuni katika halmashauri ya wilaya ya Korogwe ambako tayari wameanza kunufaika na utekelezaji wa mkakati huo wa kupatikana dawa muhimu kwenye zahanati wamesema umewapunguzia kero iliyowakabili kwa muda mrefu.

Suleiman Mohamed mkazi wa kitongoji cha Kichangani Hale anasema kabla ya kutekelezwa kwa mkakati huo miezi kadhaa iliyopita hawakuona faida ya kuwepo kwa zahanati yao ya kijiji kwa kuwa haikuwa na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo. Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Hale Sisi kwa Sisi, Kabula Nzwalla ametoa pongezi na kusema utekelezaji wake kwa muda mfupi umeongeza idadi ya wateja wanaofika kituoni kwa siku.

“Sasa tumejikuta tunapokea dawa nyingi na za aina tofauti kulingana na mahitaji yetu, wagonjwa wameongezeka kutoka wastani wa watu 30 zamani mpaka 70 au 90 kwa siku, tofauti kabisa na mwanzoni wakati wa uhaba wa dawa”, anaeleza Kabula.

Kwa upande wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Makuyuni, Judith Silayo ambayo inahudumia vijiji vitano vya Mwenga, Gomba, Kwasunga, Makuyuni na Kwasunga Mpirani anasema wameongeza makusanyo ambayo yanaiwezesha zahanati kumudu gharama za kununua dawa zake kulingana na mahitaji yao tofauti na walipokuwa wakitegemea mgawo wa kila baada ya miezi mitatu kutoka MSD.

Pamoja na mafanikio hayo yaliyoanza kuonekana kwa muda mfupi katika baadhi ya vituo, Silayo anashauri juhudi za makusudi za kuendeleza uhamasishaji zifanywe na viongozi wa kamati za maendeleo za vitongoji, vijiji na kata nyingine zilizosalia ili nazo ziweze kujitosheleza kwa dawa kupitia fedha zinazochangwa na wateja wa vituo husika.

“Napendekeza tuongeze uhamasishaji kwa kutumia mbinu nyingi zaidi, ikiwemo watumishi wa idara ya afya kuhutubia kwenye mikutano ya hadhara, kuzunguka shuleni, gereji kwa vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na kiuchumi ili wajiunge na CHF ambapo michango yao itasaidia kununulia dawa muhimu.

Kutokana na changamoto hiyo ya upungufu wa dawa muhimu katika vituo mbalimbali vya serikali vya kutolea huduma za afya nchini ni vema sasa Wizara ya Afya ikaangalia uwezekano wa kuanzisha utaratibu wa kupokea taarifa kuhusu hali ya upatikanaji dawa kutoka kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya ili kuelewa uhalisia wa mahitaji yao.

Aidha, pia Wizara ya Afya inapaswa kuwa na utaratibu wa kutoa mrejesho sahihi kila mara na kueleza jamii ni nini kinafanyika ili kuboresha upatikanaji wa dawa muhimu, vitendanishi na vifaa tiba katika kila halmashauri.

Kwa kuwa tatizo la kukosekana kwa dawa muhimu kwenye vituo vya serikali ni kero na changamoto ya kitaifa ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi naamini wakati umefika kwa wananchi kuacha kupeleka lawama kwa watoa huduma badala yake serikali na msd wajaribu kutoa taarifa za wazi kuhusu hali ya upatikanaji dawa kwenye vituo kupitia midahalo na vyombo vya habari ili kuwawezesha watanzania kuelewa hali halisi.

Halmashauri ya wilaya ya Korogwe inayokadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya 300,000 inazo Zahanati 37, vituo vya Afya vitatu na hospitali ya wilaya.