25Mei2013

 

Uzazi wa mpango ni tiba kwa familia

UZAZI wa mpango ni njia mbalimbali ambazo hutumiwa na mwanadamu kwa lengo la kuzuia utungaji wa mimba kwa muda fulani hadi pale wanapotaka kupata mtoto au watoto.

Pia Uzazi wa Mpango kwa maana nyingine ni uamuzi wa mume na mke kupanga wazae watoto wangapi, na wapishane kwa muda gani, kati ya mtoto mmoja hadi mwingine.

Faida za kutumia Uzazi wa Mpango kwa wanandoa hata wale wasio na ndoa ni kuwa na uwezo wa kutunza watoto, kuwa na muda wa kuwasomesha pia mama anaweza kurudisha nguvu ya mwili baada ya kujifungua na kupata muda wa kutosha kumnyonyesha mtoto.

Njia za uzazi wa mpango zipo za aina tofauti, zipo vidonge vya kumeza, sindano, vijiti, kitanzi, mipira (kondomu), kufunga kizazi kwa baba au mama, njia za asili (kalenda) na kwamba zipo njia tofauti kwa sababu watumiaji hutofautiana kimwili katika mahitaji.

Akitoa mafunzo ya afya ya uzazi wa mpango kwa watumishi wa Kampuni ya magazeti ya serikali, Tanzania Standard Newspapers (TSN), wachapishaji wa Daily News, Sunday News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili, Mkufunzi kutoka Kampuni ya T-MARC, Grace Dibibi anasema uzazi wa mpango ni njia salama na haina madhara kwa watumiaji.

Anasema njia hizo za uzazi hutofautiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine na kwamba wapo wanaotumia njia ya uzazi kwa kutumia vidonge na wasipate usumbufu wowote na kwamba wapo wengine wanatumia njia hiyo na ikawaletea usumbufu na wanapobadilisha na kutumia njia nyingine kama vile vijiti ikawafaa.

“Yapo maneno mengi mtaani kwamba njia za uzazi wa mpango zina madhara, jambo hili si sahihi, ukitumia ipasavyo kwa kufuata maelekezo na ukafahamu njia ipi inakufaa, hakuna madhara yoyote, ila kwa kuwa watu wanasikiliza ushauri mitaani na si kwa wataalamu wa afya ya uzazi, wanajenga akilini mwao uzazi wa mpango una madhara,” anasema Dibibi.

Anasema kama mtumiaji ametumia njia moja ikamletea maudhi madogo madogo kama vile kichefuchefu au kujisikia vibaya jambo ambalo anasema ni vitu vya kawaida, anaweza kumuona mtaalamu wa afya ya uzazi amkashauri na kubadilishiwa njia nyingine ambayo ataiona inamfaa.

Ambapo anasema kwa wale wanaotumia njia ya uzazi kwa sindano, mama huchomwa sindano yenye kichocheo kimoja kila baada ya miezi mitatu na kwamba njia hiyo humfaa mama asiyetaka kumeza vidonge kila siku.

Anasema njia ya uzazi wa mpango ni salama na hazimzuii mama kunyonyesha mtoto kama ambavyo baadhi ya watu huko mitaani wanavyosema, jambo ambalo linawafanya wakina mama wengine kutotumia uzazi wa mpango kwa kuogopa madhara.

Anataja njia nyingine ni vipandikizi (Vijiti), vijiti vya plastiki vyenye kichocheo kimoja huwekwa chini ya ngozi ya mama na kwamba njia hiyo inafaa kwa wale wanaohitaji kupumzika kuzaa kwa muda mrefu, kuanzia miaka miwili au zaidi.

Pia njia nyingine ya uzazi wa mpango ni ile ya kufunga uzazi kwa mwanaume au mwanamke, na kwamba njia hiyo kwa watanzania wengi, hususan wanaume hawaipendi kwani hadi sasa wanaume waliofunga uzazi ni watatu tu nchi nzima.

Anasema kwa upande wa wanawake waliokwisha kufunga uzazi hadi sasa ni asilimia 30, wengi wao wakiwa ni wanawake wasomi, ambao wameshauriana na wenza wao kuona idadi ya watoto walionao inawatosha na hivyo kufunga uzazi kabisa.

Anasema pamoja na changamoto nyingi za kuhusu uzazi wa mpango, bado jamii inapaswa kuelewa kwamba uzazi wa mpango ni njia nzuri inayotoa mwanya kwa wazazi kupanga idadi ya watoto wawatakao kwa muda fulani, na pia inampa mama nguvu na kuepusha vifo vinavyoweza kuzuilika.

“Mama akizaa mara kwa mara bila kupumzika, kunamchosha na wakati mwingine anaweza kufa yeye na mtoto anayetegemea kumzaa, hiyo inachangiwa na sababu nyingi zikiwemo za hali ya afya yake na lishe”, anasema Dibibi.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za afya nchini zinaonesha kwamba matumizi ya njia za kisasa za Uzazi wa Mpango kwa wanawake walioolewa ambao wamefikia umri wa kuzaa yameongezeka, lakini ongezeko hilo ni la pole pole, hasa katika miaka ya hivi karibuni.

Kadhalika tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonesha kwamba matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango yaliongezeka kutoka asilimia 7, mwaka 1991/92 hadi kufikia asilimia 13 mwaka 1996 na asilimia 17 mwaka 1999 hadi kufika asilimia 20 mwaka 2004/05.

Hivi sasa matumizi ya njia ya uzazi yameongezeka, ingawa ongezeko hilo bado ni la chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki na Kusini mwa Afrika. Hata hivyo, bado kuna kiwango kikubwa cha mahitaji ya njia za uzazi wa mpango ambayo hakijakidhiwa na hiyo ni kwa mujibu wa Utafiti wa Hali ya Afya na Uzazi (TDHS) nchini.

Hivi karibuni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi wakati akiwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake, alisema Tanzania itatenga fedha kwa ajili ya uzazi wa mpango katika bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Fedha zinazohitajika kwenye utekelezaji wa uzazi wa mpango kwa miaka mitatu kuanzia sasa ni takriban shilingi bilioni 140, fedha ambazo zitapatikana kutoka bajeti ya ndani ya serikali pamoja na wabia, lengo likiwa ni kuwafikia wanawake zaidi ya milioni 3.2 nchini.

Dk Mwinyi anasema uwekezaji huo ni mkubwa ambao una lengo la kuhimiza matumizi ya uzazi wa mpango nchini ili kuhakikisha Tanzania inakamilisha lengo lake la kufikia asilimia 60, ya wanawake ifikapo mwaka 2015.

Hata hivyo, anasema hivi sasa wanawake wanaofikiwa na huduma ya uzazi wa mpango ni takribani milioni 2.4 na kwamba lengo ni kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika kama ambavyo sera ya serikali inavyotaka kupunguza vifo vya mama na mtoto, ambavyo ni vingi.

Hivi sasa ongezeko la watu nchini ni asilimia tatu kwa mwaka, na kwamba uwiano wa sasa ni kwamba mama mmoja anazaa watoto watano, jambo ambalo linachangia ongezeko la vifo kutokana na ukweli kwamba hali ya maisha na pato la mtanzania haliendani na idadi ya watoto hao watano kwa mama mmoja.

Hivyo msisitizo unawekwa kwamba, ni vyema familia ikapanga uzazi, ili kuwa na idadi ya watoto watakaoweza kuwalea na kuwasomesha na pia hiyo itapunguza vifo vya kina mama na watoto nchini.