Waarusha: Kabila lenye mila na desturi za Kimaasai
- In Makala
- Post 15 Juni 2012
- By Kaanaeli Kaale
- Imesomwa mara: 1224
KAMA ulibahatika kukutana na watu wa kabila la Arusa wakifanya kazi mashambani unaweza kukadhani ni wabantu.
Pia ukiwakuta njiani wakiwa wamevalia mavazi yao ya asili, unaweza ukadhani ni wafugaji wa Masaai, ambao lugha yao ni jamii ya nailoti. Kwa mujibu wa historia, kabila hilo linajulikana kama Arush. Wamaasai husema ni kabila la Ilarusa na asilimia kubwa ya wazungumzaji wa Kiswahili huwaita Waarusha.
Inadaiwa kuwa watu wa kabila la Arusa walipewa jina hili na Wamaasai. Katika kabila la Wamaasai ng’ombe dume mwenye rangi mbili huitwa Arus. Inasemekana kuwa baada ya Wamaasai kuona watu wenye mila na desturi kama zao, lakini wanatofautiana katika shughuli za kiuchumi waliamua kuwafananisha na ng’ombe mwenye rangi.
Awali Wamaasai na Waarusha waliogopana na walioneshana uadui lakini baadaye walipatana, hasa pale Wamaasai alipobaini kuwa wanaweza kupata tumbaku, inayolimwa na watu hao wenye tabia mbili tofauti.
Inadaiwa kuwa baada ya kujenga urafiki na kubaini kuwa watu hao ni wakarimu na wana tabia zinazofanana na makabila mawili tofauti, waliwafananisha na ng’ombe wawili wenye rangi mbili tofauti na kuwaita Il-Arusa, jina ambalo limeboreshwa na kuwa Arusha.
Kabila la Arusa limekuwa likiwachanganya watafiti wa masuala ya utamaduni, mila na desturi za makabila. Baadhi ya watafiti wameandika ripoti, zinazoelezea kuwa Waarusha ni Wabantu na wengine wanasema kabila hilo lipo kwenye kundi la Nailoti kama Wamaasai.
Kila mtafiti anatoa sababu zake jambo ambalo linazua swali: “Waarusha ni watu wa namna gani na kabila lao liko kwenye kundi lipi kati ya Bantu na Nailoti?” Watu wa kabila la Arusha wajihusisha na kilimo kama ilivyo kwa makabila ya kibantu, yanayoishi sehemu za mwinuko katika Kanda ya Kaskazini wakiwamo Wachagga, Wameru na Wasambaa.
Hata hivyo watu wa kabila la Arusha, huzungumza kama Wamaasai na mila na desturi zao zinafanana na zile za Wamaasai. Inaaminika kuwa mwaka 1930 kabila la Waarusha lilikuwa likiishi katika mteremko wa mlima Meru na kufanya shughuli za ufugaji kama Wamaasai, lakini walipochanganyika na Wabantu, walibadili shughuli zao za kiuchumi na kujihusisha na kilimo kama Wabantu.
Baadhi ya watu ambao hawafahamu vyema, kuhusu kabila hilo wanasema ni “Wakulima wa Kimaasai.” Kama ilivyo ada ya wakulima, Waarusha wanaishi katika eneo lenye ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa katika mteremko wa Mlima Meru. Kabila hilo limejikita katika kilimo cha kahawa, ndizi, viazi na kunde.
Pia kinajihusisha na ufugaji, lakini ufugaji wao sio mkubwa kama ilivyo kwa kabila la Maasai. Kabila hilo huendesha shughuli za kilimo, eneo la Kusini Magharibi mwa Mlima Meru na wana ushirikiano wa karibu na jirani zao ambao ni Wameru.
Shughuli za kiuchumi na hasa kilimo zinasababisha utamaduni wa kabila hilo kufanana na utamaduni wa makabila ya Kibantu, lakini ukweli, lugha, mila na desturi zinashabihiana na kabila la Kimaasai, hivyo Kabila la Waarusha liko kwenye kundi la Nailoti.
Ingawa lugha ya Waarusha inatofautina na ile ya Wameru, makabila hayo mawili yana mshikamano na upendo mithili ya watoto mapacha wanaoishi katika mteremko wa mlima Meru, Kaskazini mwa Mji wa Arusha. Wameru waliuita mlima unaowazunguka jina la Meru na Waarusha, nao wakaupa mji jina la Arusha.
Inasemekana kuwa baada ya kugawana maeneo hayo maarufu walikubaliana wilaya iitwe Arumeru, kwa kuchukua maneno mawili ya mwanzo kutoka katika kabila la Arusha na Meru. Tofauti na kabila la Wamaasai, ambao wanaishi katika nyumba kubwa zilizojengwa kwa umbo la mstatili, Waarusha wanaishi katika nyumba ndogo za mviringo.
Kwa kawaida nyumba moja inatosha familia moja, ila kuna ripoti zinazoonesha kuwa baadhi ya familia huishi na ndugu kwa lengo la kusaidiana na kuboresha upendo na mshikamano katika familia. Kutokana na uongezeko la watu, Waarusha wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa ardhi, ambao hauendani na mahitaji halisi ya Waarusha, ambao wanahitaji ardhi na eneo la kujenga katika makao yao ya asili.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, baadhi ya Waarusha hutunza makazi yao ya asili na kwenda kutafuta ardhi ya kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi katika maeneo mengine tambarare kama Kisongo, Mbauda, Oljoro na Oldoinyo Sambu. Familia moja inaweza kuhodhi ardhi katika eneo la makazi mapya Monduli na Makuyuni na pia Kiteto, ambako ni mbali kutoka eneo lenye makazi yao ya asili.
Kwa kuwa Waarusha ni miongoni mwa makabila machache yanayoshika ardhi kwa ajili ya kizazi kijacho, wana tabia ya ku kodisha ardhi ambayo hawaitumii. Kwa kawaida ardhi ya Waarusha hugawiwa kwa vijana wa kiume ili waiendeleze. Utaratibu wa kugawa ardhi, huzingatia mfumo wa kurithishana kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine.
Hata hivyo, vijana hao hufanyakazi kwa bidii ili waweze kupata fedha za kununua ardhi atakayorithisha watoto wao badala ya kutegemea ardhi ya kutoka enzi za mababu ambayo haitoshelezi kizazi cha sasa. Kabila la Arusha ni miongoni mwa makabila ambayo utamaduni wake unaathirika, kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na ukuaji wa miji.
Baadhi ya watu wa Arusha wameuza maeneo yao ya asili ili kupisha ujenzi wa kisasa katika mji wa Arusha, kisha kwenda kununua ardhi kubwa zaidi katika maendeleo ya mbali na Arusha. Kitendo hicho kinasababisha wimbi kubwa la Waarusha, ambao wanahama kutoka maskani ya kale na kwenda kuishi sehemu mbalimbali, hali inayoathiri pia mila na desturi za Waarusha ambao wanafuata mfumo wa maisha ya kisasa.
Katika kabila la Waarusha kuna baadhi ya watu ambao wanafuga mifugo mingi, mithili ya Wamaasai na kiasi kwamba inakuwa vigumu kuwatofautisha na Wamaasai. Waarusha wenye mifugo mingi, kama Wamaasai wanapatikana katika maeneo ya Olakii, Terat, Makuyuni na pembezoni mwa Ngorongoro.
Mwandishi wa kitabu kuhusu makabila ya Kaskazini mwa Tanzania, Gervase Mlola, anasema wanawake wa Kiarusha, hutumia njia ya asili maarufu kama sherehe ya Mbessi, kwa lengo la kujikwamua kiuchumi. Sherehe za Mbessi hufanyika wakati mwanamke anapojifungua, ndoa, ubatizo au mtoto anapofikisha siku arobaini.
Ili kufanikisha sherehe hizo, kikundi cha marafiki hujikusanya na kununua zawadi mbalimbali kisha kuzikabidhi kwa mama wa familia, kama njia ya kusaidiana kwa hali na mali katika kuimarisha ustawi wa jamii.
Mfano, sherehe za Mbessi kwa ajili ya kumpongeza mama aliyejifungua, wanawake wa Kiarusha huchangishana fedha za kununua vitu mbalimbali kama vile nguo, sukari, unga wa sembe, mafuta ya kula, kuku, mkaa, kuni na mikungu ya ndizi.
Wanawake hao huvaa nguo nzuri na safi kisha kukusanyika kwa lengo la kwenda kumtembelea rafiki yao aliyejifungua na baada ya kucheza na kufurahia kukabidhi zawadi walizoleta.
Siku hizi sherehe za Mbessi huambatana na zawadi kubwa, kama seti ya nguo za mtoto mchanga, vyombo vya kutunza mtoto mchanga na fedha taslimu ili kumliwaza na kumuwezesha mama kufurahia maisha katika kipindi cha uzazi na baada ya uzazi.
Ingawa kuenea kwa dini ya Kikristo, uhaba wa ardhi na mabadiliko ya mfumo wa maisha, umesababisha Waarusha kuacha ndoa za kijadi, ambazo zinaruhusu mwanamume kuoa mke zaidi ya mmoja, bado kuna baadhi ya wanaume wanaoa wake wengi.
Waarusha ni miongoni mwa makabila yanayosifika, kutokana na utaalamu wake wa kudumisha umoja, upendo na mshikamano katika familia.
Mwanamume mwenye wake wengi hutumia mfumo maarufu kama Alwashe, ambao hutoa fursa kwa mwanamume kuwakutanisha wake zake, watoto na hata wajukuu na kufanyakazi za shambani kwa pamoja kisha kugawana mavuno ambapo kila mtoto anapata haki yake pasipo upendeleo.
Pasipo kujali kama familia ina wake wengi au la, Waarusha wanamshikamano mkubwa. Mjomba ni miongoni mwa watu wanaoheshimiwa sana katika kabila la Waarusha. Pia mama wa Kiarusha hujenga uhusiano wa karibu na binti yake, hata kama binti huyo, atakuwa ametoka nyumbani na kwenda kuolewa mbali.
Kwa kawaida kabila la Waarusha, halipotezi watu wa ukoo kwa kuwa wana mfumo wa kufuatilia kwa karibu safu za mababu ili kubaini asili yao kutoka babu wa kale. Kama ilivyo kwa kabila la Wamaasai, watu wa kabila la Arusha huwapatia watoto wao majina yenye kuashiria neema na baraka siku za usoni.
Mfano jina la Epasuka ni maarufu kama jina la Mary katika familia za Kikristo. Pia jina la Einotti ni maarufu kwa watoto wa kike na linamaanisha mtoto wa wa kwanza wa kike ambaye alizaliwa baada ya shauku ya muda mrefu kwa wazazi kutaka mtoto. Majina marufu kwa watoto wa kiume ni Tomoto, lenye maana ya mtoto aliyemaliza shida.
Kwa maneno mtoto alizaliwa wakati familia ipo katika wakati mgumu, lakini mara baada ya kuzaliwa mtoto huyo shida zikaisha. Melau ni jina la mtoto wa kiume lenye maana ya kuridhika. Kwa mujibu wa Mlola, Kabila la Arusha lina koo nne ambazo ni Mollel, Laiser, Kipuyo na Lukumay.
Vijana wa Kiarusha hawana vikwazo katika kuchagua mchumba kwani huruhusiwa kuoa au kuolewa na mtu wa kabila lolote ndani na nje ya nchi. Ingawa hakuna kikwazo katika dini, vijana wengi huoa au kuolewa na Wakristo, dini maarufu miongoni mwa Waarusha.
Kama iliyo kwa Wamaasai, mfumo wa maisha wa Waarusha, unazingatia umri na umegawanyika katika makundi kwa kuzingatia rika la watoto wenye umri sawa katika kijiji, au tukio ambalo lilijumuisha kundi fulani la watu hasa vijana. Rika ambalo linapewa kipaumbele katika jamii ni like la vijana wanaoingia jangoni kwa lengo la kutahiriwa.
Kabla na baada ya kutahiriwa vijana hao kufanyiwa sherehe na kucheza pamoja hivyo kujenga mahusiano mazuri na kuendelea kushirikiana hadi uzeeni. Vijana wanaotoka jandoni huendelea kushirikiana na kusaidiana kwa hali na mali pia hushirikiana wakati wa raha na shida, kujenga hulka ya kuheshimiana pia kutaniana ili kudumisha umoja.
Kama ilivyo kwa Wamaasai, Waarusha huzingatia uhusiano wa rika moja kwenye rika jingine ambapo madaraja ya marika yanatofautiana kutokana na umri, tabia, majukumu na wakati mwingine upendeleo, mfano rika la watoto na wazee kupata upendeleo maalumu katika jamii.
Hata hivyo kundi la wazee maarufu kama ilmuruos hupewa heshima ya kipekee kwa sababu wana uzoefu mkubwa katika maisha hivyo huwa tegemeo katika jamii hasa kutoa elimu wa jamii hususani kupendekeza mbinu za kutatua matatizo mbalimbali.
Mavazi ya Waarusha hayana tofauti kubwa na yale ya Kimaasai kwa kuwa huvaa rubega rangi ya kahawia na nyekundu na shanga. Vijana wa kimaasai kusuka nywele zao na kuziweka shanga na mapambo mengine. Wanawake huvaa rubega rangi ya bluu pamoja na shanga, mikufu mikubwa shingoni na bangili za asili ambazo zimetengenezwa kwa ustadi mkubwa.
Hata hivyo wanawake wa siku hizi kupendelea kuvaa nguo zinazovaliwa na idadi kubwa ya Watanzania zenye asili mataifa ya Magharibi. Wanawake wengi wa kisasa hupenda kuvaa nguo tofauti kama vile khanga, magauni, sketi pia wapo wanavaa suruali, sweta na viatu vya wazi.
Pia wanawake wa siku hizi wanapenda kubeba mzigo kichwani kama Wabantu, badala ya mgongoni kama walivyokuwa wakifanya siku za nyuma, mtindo ambao ni maarufu kwa watu ambao lugha yao iko kwenye kundi la Nailoti. Wanawake na wanaume hutoboa masikio na kuvaa mapambo ambayo yanawatofautisha na watu wa makabila mengine.
Hata hivyo, Waarusha wa kisasa wameacha baadhi ya mila za asili ikiwa ni pamoja na kutoboa na kuvaa vitu vizito masikio, kujichanga katika paji la uso na kwenye mashavu ili kujitofautisha na makabila mengine.
Kwa kuwa Waarusha ni watu wanaopenda amani, wana utaratibu wa kumaliza migogoro inayotokea katika familia au katika ukoo. Migogoro au kesi husikilizwa na wazee wenye busara na mlalamikiwa anapopatikana na hatia hulazimika kulipa faini, hasa ng’ombe na kugharimia kikao cha upatanisho.



