Ukatili wa kijinsia unavyoathiri watoto kisaikolojia

WATOTO ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi kisaikolojia wanapofanyiwa matendo mbalimbali, ikiwemo unyanyasaji wa kingono. Ukatili wa kingono ni tukio ambalo hutokea kwa vitisho ambalo husababisha madhara ya kisaikolojia, kimwili na hata kiakili.

Mtoto kwa sheria nyingi duniani ni binadamu mwenye umri kuanzia mwaka sifuri hadi miaka 18. Akifikisha umri huo hujulikana kama mtu mzima. Kumekuwapo na kesi nyingi hasa kwa watoto wa kike ambao wanafanyiwa ukatili wa kijinsia na wanaume katika familia zao, majirani, ndugu zao, viongozi wa dini na wa kisiasa.

Hata hivyo, imezoeleka kwamba matukio ya unyanyasaji wa kingono kwa mtoto ni kubakwa, kulawiti, utumikishwaji wa kingono na udhalilishwaji wa kingono. Miongoni mwa vitu ambavyo wengi wao hawavifahamu ni pamoja na mwanamume kuchezea sehemu za siri za mtoto (kumnajisi) kwa lengo la kutaka kutimiza haja zake za kimwili.

Mwandishi wa Kitabu cha Tanzania Parent Plus, kinachoelezea namna ya kumlea mtoto, Nilu Kalutanga anaeleza kuwa matukio mengine yanayoweza kumuathiri mtoto ni pamoja na kumuonesha picha za ngono, kuweka mikao ya kingono wakati wa kupiga picha na kugusianisha sehemu za siri za mtu mzima na mtoto.

Kalutanga anasema kuwa vitendo vingine ni kutumia bafu la kuogea pamoja na mtoto, pia kutafuta picha za ngono katika mitandao. “Suala la kumuonesha mtoto picha za ngono ni kumhamasisha kuingia katika vitendo viovu. Kwa mzazi anayefanya matendo hayo, humuathiri mtoto na huchangia kumnyanyasa,’’ anasema Kalutanga.

Anasema kwa watu ambao hupenda kuangalia vitu hivyo wakiwa na watoto wao, wanatakiwa kupata msaada jinsi ya kuzuia tabia hizo zinazomuathiri mtoto kisaikolojia. Anasema katika makuzi ya mtoto, mzazi anatakiwa kuwaeleza watoto wake kuhusu mabadiliko ya miili yao na kuepuka unyanyasaji wa kingono.

Anaeleza kuwa mzazi anapoona ishara za unyanyasaji wa kingono au mwingine wa kijinsia kwa mtoto, anatakiwa kumpeleka mtoto huyo kwa daktari ili aweze kumsaidia kwa kumpima magonjwa ya zinaa. Anafafanua kuwa ishara ya kwanza ni maumivu, kutokwa damu sehemu za siri na kubadilika rangi midomoni.

Pia anapaswa kuangalia kama mtoto anaendelea kupata maumivu ya tumbo na maumivu wakati wa kukojoa. Kwa mujibu wa Kalutanga, kila mmoja anafahamu kwamba mtoto hukua kupitia hatua mbalimbali na kwamba kuhusu uelewa, udadisi na mada kuhusu mahusiano hubadilika kuanzia utoto hadi balehe.

Kila mtoto hukua katika njia yake na kwamba hatua za maendeleo ya ukuaji wa mtoto hulingana. Ni vigumu kujua tofauti kati ya umri na ukuaji sahihi wa kijinsia na ishara za hatari kuhusu tabia. Mara kwa mara unaweza kuhitaji kuelezea kwa mtoto kwa nini wanapendelea au kutoendelea na tabia fulani.

Kama mtoto anaweza kufanyiwa matendo ya kingono na mzazi, binamu, rafiki, ndugu na jirani, anatakiwa kutoa taarifa kituo cha Polisi katika dawati la jinsia ili kuchukuliwa hatua za haraka.

‘’Kama mtoto hataweza kusema, anaweza kumueleza mtu yeyote ambaye hatakuwa na wasiwasi naye kwa lengo la kupata ufumbuzi mapema,’’ anasisitiza Kalutanga. Kalutanga anafafanua kuwa kuanzia mwaka sifuri hadi mitano, mtoto huanza kusoma darasa la awali hivyo mzazi anatakiwa kutumia lugha za kitoto kuzungumzia sehemu za mwili za mtoto huyo ili apate ufahamu.

“Mzazi unaweza kumueleza mtoto jinsi mtoto anavyotengenezwa na wapi anatokea kwa kumuonesha kupitia sehemu za mwili wake. Taarifa hiyo itamsaidia pindi atakapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono ataeleza amefanyiwa wapi,’’ anasema Kalutanga.

Anaeleza kwa miaka sita hadi 12, mtoto huanza shule ya msingi ambapo mzazi anatakiwa kumuuliza maswali mtoto wake kuhusu hedhi, mimba na tabia za ngono. Pia anasema katika kipindi cha ukuaji wa mtoto mzazi anatakiwa kuuliza maswali kuhusu mahusiano na kutumia lugha za mapenzi kuzungumza na binti au kijana wake.

Kitabu hicho pia kinaeleza kuwa yapo mambo ambayo huweza kumuathiri mtoto ikiwamo mzazi kupewa talaka, kifo cha mmoja wa familia, matatizo shuleni au marafiki na matukio mengine ya kuumiza. Anaeleza kuwa zipo njia saba ambazo mzazi anaweza kuzitumia kwa ajili ya kumlinda mtoto wake na unyanyasaji wa kingono.

Anasema njia ya kwanza ni kumfundisha mtoto kuwa na mipaka kwamba hatakiwi kushikwa mabega na mikono pia kutambua namna ya kuomba msaada pindi atakapopata matatizo.

Anasema mtoto ambaye anaweza kutengeneza mipaka imara inamuandaa kupambana na watu ambao watamshika kwa malengo maovu na kwamba mtoto anayejua kuomba msaada anapofanyiwa matukio ya kumnyanyasa ana uwezo wa kukemea kitendo hicho kwa mtu mwingine.

“Msaidie mtoto aweze kufuata nyayo zako kwa kusema ‘hapana’ na endapo kutatokea tatizo ajue kusema naomba msaada,” anasisitiza Kalutanga. Njia ya pili ni kumuwekea mtoto mipaka ya kucheza.

Njia ya tatu ni kumfundisha mtoto kwamba kuguswa, matatizo, michezo yote ambayo yanaashiria uovu yanatakiwa kusemwa haraka na isiwe siri kwani ndio chanzo cha matatizo. Anasema hata mtoto akipewa zawadi na mtu yeyote anatakiwa kusema kwani wengine huwa na nia mbaya kwao, pia kubusiwa, kukumbatiwa.

Njia ya nne ni kumfundisha mtoto kuwa na michezo ya salama kwamba akiona mtoto, ndugu ama rafiki ambaye anaashiria vitendo viovu anatakiwa kumwambia aache, aondoke na wakati huohuo aombe msaada.

Vile vile, njia nyingine ni kumfanya mtoto azungumzie ni namna gani hapendi kuguswa; kwani kuna kuguswa kwa madaktari wakati wa maradhi, hiyo haitamfanya aumie lakini kwa namna nyingine ya kuguswa itamfanya asijisikie huru.

Pia kumfundisha mtoto ujuzi wa aina mbalimbali ambao ni salama bila ya kumpatia taarifa ambazo zitamkwaza kwa kukemea maovu au kumwambia mtu yeyote kuhusu matukio hayo kwa ajili ya msaada.

Njia ya saba ni kumuelekeza mtoto namna ya kupata msaada endapo atafanyiwa unyanyasaji: kwa mfano mwanamume kumuambia mtoto anampenda au anataka amuoe hali hiyo huwa inawaumiza watoto na kumuona mtu yule mbaya.

Endapo mtoto atakuwa na Tania ya kusema kwamba hapendezwi na hali hiyo, mzazi au mlezi anaweza kumkataza mtu huyo kuendelea na tabia yake. Akizungumzia kitabu hicho, Kalutanga anasema kuwa Tanzania Parent Plus kilizinduliwa Oktoba mwaka jana na ni jarida la kwanza na la aina yake linalohusiana na malezi na uzazi kuchapishwa nchini Tanzania.

Kalutanga anasema ni jarida linalopata utambuzi na kukubalika kwa haraka katika jamii kutokana na uelimishaji wake kuhusu mambo ya malezi. Anasema jarida hilo linachapishwa mara moja kila baada ya miezi miwili na linawalenga wasomaji wa jinsia zote kuanzia umri wa miaka 20 hadi 60 na kuendelea.

Tanzania Parent’s Plus inafanya kazi ili kuendeleza Tanzania kuwa na jamii bora na salama katika masuala mbalimbali ya malezi. Anaeleza kuwa malengo ya jarida hilo ni kuwasaidia wazazi kuelewa masuala na changamoto ambazo ni muhimu kwao kuzijua ambazo pia zinawakabili watoto wao.

“Tanzania Parent Plus ina lengo la kuelimisha jamii juu ya masuala halisi kama vile haki za binadamu, kuongeza ajira, kupunguza umaskini, uwezeshaji wa vijana, kuzuia uonevu, ukatili na unyanyasaji kwa watoto,’’ anasema Kalutanga.

Pia anasisitiza kuwa jarida hilo linasambaza nakala kwenye shule mbalimbali kwa ajili ya walimu na wawezeshaji kuwaelimisha watoto na vijana kuhusu mada zilizozungumziwa katika jarida.

Anafafanua kuwa jarida hilo pia linatoa nafasi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, na makampuni ya kijamii kutambua umuhimu wa malezi. Tanzania Parent Plus inatoa makala mbalimbali zinazohusu ujauzito na baada ya kujifungua kwa watu wanaotarajia kuwa wazazi, makala za watoto na hatua za utoto kwa wazazi wapya juu ya malezi chanya, nidhamu na elimu.

Pia jarida hilo linaweza kutumika na walimu na wawezeshaji kama rasilimali ya elimu. Kwamba makala zitawapa uwezo wanafunzi wao na walimu wenyewe. “Tunafanya kazi na washirika wetu kuhakikisha jarida linasambazwa katika shule zote za serikali na hata zisizo za serikali kuhakikisha zinawafikia wanafunzi na walimu wote ili liweze kuwa msaada kwao,” anasema Kalutanga.