Uchaguzi Kenya wafanywa katika hofu na matarajio
- In Makala
- Post 05 Machi 2013
- By Magnus Mahenge
- Imesomwa mara: 569
UCHAGUZI Mkuu nchini Kenya umefanyika jana Machi 4, lengo likiwa lile la kumpata rais wa nne wa nchi hiyo atakayetekeleza Katiba mpya ya nchi hiyo sambamba na kuwapatia Wakenya maendeleo wanayoyatarajia.
Gazeti hili wakati linakwenda mitamboni, bado matokeo ya nani ameibuka mshindi katika kiti hicho yalikuwa bado kutangazwa. Wapigakura kutoka katika majimbo manane ya nchi hiyo ya; Kati, Pwani, Mashariki, Nairobi, Kaskazini- Mashariki, Nyanza, Bonde la Ufa na Magharibi walishiriki katika kumchagua rais na wagombea wa ngazi nyingine za chini.
Historia inaonesha kwamba nchi hiyo iliyopata uhuru wake Desemba 12, 1963, Kenya ilitawaliwa na Gavana Mkuu, Marcolm Mac- Donald wa Uingereza. Rais wa Kwanza wa nchi hiyo alikuwa Mzee Jomo Kenyatta, aliyezaliwa Oktoba 20, 1893 na kufariki dunia Agosti 22, 1978.
Kenyatta anayeheshimika kama mwasisi wa taifa hilo alishika madaraka kwa tiketi ya chama cha Kanu tangu Desemba 12, 1964 hadi Agosti 22, 1978. Rais wa pili alikuwa Daniel arap Moi; aliyezaliwa Septemba 2, 1924 na anaishi hadi leo. Yeye alianza kuongoza Kenya kwa tiketi ya chama cha Kanu tangu Agosti 22, 1978 hadi Desemba 30, 2002.
Rais wa tatu ni Mwai Kibaki aliyemaliza muda wake. Yeye alizaliwa Novemba 15, 1931 na akashika madaraka kwa tiketi ya DP- NARCPNU tangu Desemba 30, 2002 hadi sasa. Kenya jana ilifanya uchaguzi ikiwa na makovu ya uchaguzi wa 2007 ambao uliibua machafuko makubwa yaliyosababisha takribani watu 1,000 kupoteza maisha na wengine 350,000 kuishi kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Katika uchaguzi huo ulioleta maafa na wengine kuishi kwenye mahema ulitokana na malumbano ya nani ameshinda kati ya Rais Mwai Kibaki, aliyekuwa akikitafuta kipindi cha pili cha uongozi na mshindani wake, Raila Odinga ambaye naye aliamini kuwa ndiye ameshinda.
Kitendo hicho kilizua balaa baada ya uchaguzi huo, ukawagawa Wakenya kwa misingi ya kikabila na kimaeneo, na hasa makabila ya wagombea, yaani Wakikuyu ambalo ni kabila la Rais Kibaki na Waluo ambalo ni kabila la Odinga. Inasemekana kwamba kabila la watu wengi nchini Kenya ni Wakikuyu na Waluo ni kabila la pili kwa ukubwa lakini katika tafrani hiyo makibila mengine nayo yaliingia.
Kumalizika kwa machafuko hayo, Februari 2008, nchi hiyo iliandika katiba mpya ambayo iliweka utaratibu mpya huku washindani wawili wakubwa wakikubaliana kugawana madaraka; Kibaki akiwa Rais na Odinga Waziri Mkuu. Katika matukio ya baada ya uchaguzi huo, Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, iliwatuhumu viongozi wanne waandamizi kuhusika.
Hawa ni aliyekuwa Makamu wa Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta; Katibu wa Bunge, Francis Muthaura; Waziri wa zamani wa Kilimo, William Ruto na Mwandishi Joshua Arap Sang. Uchaguzi huo wa jana, umefanyika baada ya kipindi cha miaka minne ambapo katiba imebadilishwa na wagombea wamefanya mijadala miwili iliyoshirikisha wagombea wote wanane na kujadili kuhusu uchumi na ardhi pamoja na mambo mengine.
Katika mabadiliko ya katiba, Rais Kibaki haruhusiwi kugombea kutokana na kutumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili, lakini pia kama wagombea watashindwa kupata ushindi, inaonesha kwamba wagombea wawili waliopata kura za juu watarudia. Uchaguzi wa jana umefanyika Wakenya wengi wakiwa hawataki kurudi kwenye historia ya kumwaga damu na kuzalisha wakimbizi ndani ya nchi yao wenyewe.
Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Issak Hassan, imepitisha na kuruhusu wagombea wa urais wanane kupeperusha bendera za muungano ya vikundi vyao kutoka vyama 20 vilivyosajiliwa kisheria.
Karatasi ya kupigia kura ambayo Wakenya waliingia nayo kwenye vyumba vya kupigia kura ilisomeka; Peter Kenneth (Eagle), Uhuru Kenyatta (Jubilee), Raila Odinga (Cord), Martha Karua (NARC-Kenya), Wycliffe Musalia Mudavadi (Amani), James ole Kiyiapi (RBK), Paul Muite (Safina) na Mohamed Abduda Dida (ARK).
Wagombea hao wengi wapo serikalini, mfano Waziri Mkuu, Odinga amekiwakilisha ODM, Makamu wa Waziri Mkuu, Kenyatta amekiwakilisha TNA, Mbunge wa zamani, Karua wa NARC- Kenya na Makamu Waziri Mkuu, Wycliffe Musalia Mudavadi anakiwakilisha UDF.
Wengine waliostaafu au kuacha madaraka ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara ya elimu, Prof Kiyiapi mwakilishi wa RBK; Mbunge wa zamani, Kenneth wa chama cha KNC; Mwanasheria, Muite wa Safina na mwalimu wa sekondari Mohamed Dida wa muungano wa Alliance for Real Change (ARC).
Makundi makubwa manne ya wagombea yalikuwa Coalition for Reforms and Democracy (Cord) lililomsimamisha Odinga huku mgombea mwenza wake akiwa Makamu wa Rais, Kalonzo Msyoka wa chama cha Wiper (WDP). Katika muungano huo pia yumo Waziri wa Biashara, Moses Watengura anayewakilisha Ford-Kenya.
Kundi la Jubilee lilimemsimamisha Kenyatta anayewakilisha chama cha TNA na mgombea mwenza wake akiwa ni Waziri mstaafu, William Ruto wa chama cha URP. Kiongozi mwingine maarufu katika kundi hilo ni Waziri wa Maji, Charity Ngiru anayewakilisha chama cha NARC.
Mwalimu wa Sekondari mstaafu, Dida, alimteua mgombea mwenza, Joshua Odongo kutoka chama cha ARC, wakati Mdavadi, mgombea mwenza wake alikuwa Jehemia Ngayu ambaye ni mwakilishi wa UDF.
Karua, mbunge wa zamani wa Gichugu alimchagua Augustine Lotode kuwa mgombea mwenza wake kutoka National Rainbow Coalition (NARC-Kenya; Mbunge wa zamani wa Gatanga, Kenneth mgombwea mwenza wake alikuwa Ronald Osumba ambaye amekiwakilisha chama cha KNC.
Katibu Mkuu wa zamani, wizara ya Elimu, Kiyiapi alimteua mgombea mwenza wake, mwanamama Winnie Kaburu wa chama cha RBK na Mbunge wa zamani wa Kikuyu, Muite alisimama na mgombea mwenza wake, Shem Ochuodho wa chama cha Safina. Muungano wa Cord ni wa vyama vya ODM, Wiper, na Ford-Kenya, wakati muungano wa Jubilee una vyama vya TNA, URP na UDF ambacho kilijimega kutoka muungano huo mwishoni mwa mwaka jana.
Muungano wa Eagle ambao una vyama vya KNC na POA, huku muungano wa Pambazuka ukiwa na vyama vya New FORD Kenya, National Vision, Federal na KADDU. Muungano wa Amani umeshirikisha vyama vya UDF, New Ford Kenya na KANU na umeundwa baada ya UDF kujitoa kwenye muungano wa Jubilee.
Wagombea wawili walitegemewa kushinda uchaguzi huo kutokana na kura za maoni nao ni Odinga na Kenyatta na watabiri mbalimbali wanabashiri kuwa huenda uchaguzi huo ukarudiwa kwa washindani hao wawili kuingia katika duru ya pili. Katiba ya nchi hiyo imekubali vyama kuungana na kutengeneza muungano, katika kuweka historia ya vyama. Vyama hivyo 20 ni National Unity, NARC Kenya, New Ford Kenya, Restore and Rebuild Kenya, United Republican na Alliance.
Vyama vingine ni National Vision, The National Congress, United Republican, Orange Democratic Movement na Mkenya Solidarity Movement. Vingine ni Republican Congress, Kadu Asili, Shirikisho, Chama Cha Uzalendo, Agano, Action, Grand National Union, Democratic na Wiper Democratic Movement.
Siku chache kabla ya uchaguzi wa jana, baadhi ya Wakenya walioathirika na uchaguzi wa mwaka 2007 waliripotiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakikimbia nchi hiyo wakiogopa yasije yakawakuta ya nyuma.
Mmoja wa watu hao alikaririwa akiliambia BBC kwamba yeye ni mmoja wa aliyeshuhudia nduguze wakiuawa, akajikuta kwenye kambi za wakimbizi na kwamba alikuwa hapendi kuona jambo kama hilo likitokea tena mbele yake na ndio maana akaamua ‘kukimbiza ubawa wake’.
Mwingine alikuwa ni mwanamama, mkazi wa kitongoji cha Kibera aliyebakwa na kundi la wahuni wakati wa machafuko hayo ya mwaka 2007/2008 na ambaye alisema toka atendewe unyama huo hajawahi kusaidiwa lolote. Waangalizi wa nje walitabiri uchaguzi kwenda vyema lakini wakasema Tume Huru ya Uchaguzi haikuwa imejiandaa vya kutosha kuhimili chaguzi mbalimbali zipatazo sita zinafanyika kwa wakati mmoja.
Chaguzi hizo ni ule wa rais, wabunge, maseneta, magavana, madiwani na wawakilishi wa wanawake. Hata hivyo, Wakenya wengi wana matumaini kwamba kwa kupitia Tume huru ya uchaguzi mambo yatakuwa shwari na wote walioshiriki kugombea watakubali matokeo.



