Tamasha la Selebuka kufanyika Songea

TAMASHA la pili la Majimaji Selebuka linalohusisha michezo, utalii wa ndani na biashara linatarajiwa kufanyika kwa wiki moja kuanzia Mei 28, mwaka huu mjini Songea na kushirikisha washiriki kutoka Tanzania na nchi jirani za Afrika.

Tamasha hilo linaandaliwa na Kampuni ya Mwandi kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Songea Mississipi (SOMI) kwa lengo la kuibua vipaji vya michezo na biashara na kuviendeleza.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa tamasha hilo, Reinfrida Rwezaura alisema tamasha hilo litafanyika viwanja vya makumbusho ya mashujaa Songea na kuhusisha michezo kama mbio za nyika, mbio za baiskeli na ngoma za asili.

“Kutakuwa na mashindano ya mbio za nyika kilometa 42, kilometa 21, kilometa 10 na kilometa 5, mbio za baiskeli ambazo tunaamini kwa mwaka huu zitakuwa za aina yake kwa sababu tunategemea kupata washiriki wa mbio za baiskeli kutoka nchi jirani kama Rwanda,” alisema.

Alitaja nchi zilizothibitisha ushiriki wao kwenye tamasha hilo kuwa ni Rwanda, Zimbabwe na Msumbiji.

Rwezaura alisema siku ya ufunguzi wa tamasha hilo kutakuwa na mbio za nyika na siku ya kufunga kutakuwa na mbio za baiskeli. Alisema washindi wa mashindao hayo watanyakua medali, vikombe, ngao, vyeti na fedha taslimu zitakazotolewa na wadhamini, Kampuni ya Bakhresa na benki ya CRDB.

Kwa washindi wa baiskeli, alisema watapata nafasi ya kwenda Rwanda kwa ajili ya mafunzo ya mbio za baiskeli za kimataifa. Naye Balozi wa tamasha hilo, Nathan Mpangala amehimiza Watanzania kushiriki kwa wingi na kujishindia zawadi, lakini pia kujifunza mambo mbalimbali kuhusu mkoa wa Ruvuma.