21Mei2013

 

Amani ni tunu ya Taifa, isichezewe

KATIKA siku za karibuni kumeibuka matukio mbalimbali hapa nchini yanayoashiria kutikisa nguzo kubwa ya taifa hili, yaani amani.

Amani kwa miaka mingi imekuwa ni tunu maalumu kwa taifa hili kama utalinganisha na mataifa mengine yakiwemo yanayotuzunguka.

Matukio ya karibuni zaidi yanahusisha uvamizi na mauaji ya viongozi wa dini ambayo ukiyaangalia kwa undani utaona kwamba yanaendeshwa katika msingi kuwafitinisha waumini wa dini kuu mbili, Ukristo na Uislamu, watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali bila kujali imani zao.

Ni wazi kuwa haya yanayotokea si ya bahati mbaya bali kuna watu wana malengo yao binafsi ambayo si mema na wanakusudia wafanikisha kile walichokikusudia. Mbalimbali na matamko yaliyotolewa na viongozi wa dini pamoja na Serikali juu ya kuilinda amani ya nchi hii, Baraza la Waislamu pia liliandaa jukwaa la kuzungumzia amani ambapo Dk Abdullah Omar Nasseef alitoa nasaha murua kwa Watanzania.

Dk Nasseef aliyejipatia umaarufu katika mataifa mbalimbali duniani kutokana na kuhubiri kwake suala la amani, alisema ni vyema kujenga hali ya kuvumiliana kwa watu wa dini zote kwa kuwa suala hilo ndio njia pekee waliotofautiana kiimani kuweza kuishi pamoja bila kubaguana, kudhalilishana na kukashifiana.

Akizungumza katika Mkutano huo wa ‘Amani na Uvumilivu wa kidini’ ulioandaliwa na Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Rais wa ‘Wapo Mission International’, Askofu Sylvester Gamanywa, Dk Nasseef alisema ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha anailinda amani iliyopo kutokana na umuhimu wake.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Dk Nasseef aliwakemea vikali wale wote wanaohalalisha kumuua mtu asiyekuwa Muislamu bila hatia yoyote wakidhani kwamba kufanya hivyo ni ibada na watakwenda peponi.

“Jambo hilo si kweli hata kidogo, kwa mtu yeyote atakayemuua mtu asiyekuwa Muislamu bila ya kosa lolote malipo yake ni moto siku ya kiama,” anasema Dk Nasseef aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo uliofanyika wiki mbili zilizopita.

Anasema ni jambo la faraja sana kuona Watanzania wakidumisha amani waliyonayo kwa kuwa ndiyo misingi iliyoagizwa na Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wa mataifa yote pasina kujali imani za dini walizonazo na kwa kufanya hivyo kunawaweka katika hali la kumpendeza muumba wao.

“Niwapongeze Watanzania kwa kitendo cha kukaa katika mkutano wa pamoja wa Masheikh na Maaskofu kwa ajili ya kunisikiliza na kuupokea ushauri juu ya kudumisha suala zima la amani,” anasema Dk Nasseef aliyeungwa mkono na Rais Mwinyi aliyewataka viongozi hao kukaa pamoja na kutafuta chanzo cha vurugu hizo na viashiria vyake.

Rais Mwinyi anasema viongozi wa dini zote nchini ndio wenye uwezo wa kutafuta njia mpya za ushirikiano zitakazosaidia kudhibiti vyanzo vya sababu zinazovuruga amani nchini kwa lengo la kuilinda amani hiyo. Alisema viongozi hao wana nafasi ya kuzuia sababu zinazovuruga amani hapa nchini kutokana na nafasi waliyonayo hasa pale panapotokea uwepo wa mambo mabaya katika jamii.

“Sababu zinazovunja amani mara nyingi huwa ni za kisiasa na viongozi katika siasa ndio huwajibika kutafuta njia za kurudisha amani, lakini inapotokea kwamba sababu za uvunjifu wa amani ni za kidini, nasi Serikali hupata tabu kukabiliana na vurugu za aina hiyo na wanaotakiwa kushughulikia kadhia za aina hiyo huwa ni viongozi wa dini.”

“Napenda kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini katika kulinda amani na kudumisha hali ya kuvumiliana, ni rahisi kwa viongozi wa kiroho wanapoamua kutumia mbinu za siasa katika shughuli zao za dini, wao wanaweza hata kuwa wanasiasa lakini ni hatari sana kwa wanasiasa kujiingiza katika uongozi wa dini na kutia ushawishi wa kidini kwa wananchi ambao tayari wanaohasimiana,” anasema Mwinyi.

Alisema vurugu zinazojitokeza hivi sasa zinaweza zikapatiwa majibu kama viongozi hao watakaa pamoja na kuamua kushirikiana kwa dhati kujua chanzo chake badala ya kila upande kukaa na kuushutumu ama kudhani upande mwingine wa dini unahusika na matukio hayo.

Kwa upande wake, Askofu Gamanywa alisema katika taifa hili kila mmoja ana haki ya kuabudu na kwamba tofauti zinazojitokeza sasa hazina msingi wowote na zaidi zimelenga kuchafuana na kubaguana kwa misingi ya kidini. Aliutahadharisha umma wa Watanzania na kuutaka kuwa makini juu ya wasioutakia mema ushirikiano uliopo kwa lengo la kuivuruga nchi kwa lengo la kuifanya kitivo cha vurugu, jambo alilosisitiza kuwa ndilo limeanza kujitokeza hivi sasa.

Gamanywa alisema wanaochochea vurugu hizo wana lengo la kuigeuza Tanzania kuwa moja ya masoko yao ya kuuzia silaha zao ili watu wauane wenyewe kwa wenyewe kwa lengo la kujifaidisha na biashara hiyo. Alisema kazi ya dini iliyopo ni tatu, kuhubiri na kueneza dini, kutafuta na kuongeza wafuasi pamoja na kutoa huduma katika jamii na siyo kusambaza chuki ambazo mwisho wake ni uvunjifu wa amani katika Taifa.

A l i s e m a mkutano huo wa pamoja kwa viongozi mbalimbali wa dini unaonesha ni namna gani wanaweza kukaa pamoja na kulijadili tatizo linalojitokeza huku akiwataka wale wote wanaoeneza chuki kwa misingi ya dini kuacha tabia hiyo.

Kimsingi matukio ya vurugu hizi zilizojitokeza zinapaswa kulaaniwa na kila upande kwa kuwa ni dhahiri kuwa zimelenga kuvunja amani ya nchi hii inayoliliwa na mataifa mengine huku jukumu likibaki kwa vyombo vya Dola kuhakikisha linachukua hatua kali kwa kuanza na uchunguzi wa kina kwa wote wanaohusika kwa lengo la kuilinda.

Ni imani yangu kuwa hakuna dini yoyote inayohusika katika suala hili zaidi ya baadhi ya watu hao ninaowaita ‘wahuni’ ambao kwa mujibu wa Askofu Gamanywa, lengo lao ni kuligeuza taifa letu kuwa soko la silaha ambazo madhumuni yake ni kupoteza maisha yetu.