Kibaki awaaga Watanzania, awapa ujumbe murua
- In Makala
- Post 05 Machi 2013
- By Theopista Nsanzugwanko
- Imesomwa mara: 198
MAKALA haya yanavyotoka gazetini leo, pengine Wakenya watakuwa wamepata Rais mwingine.
Hii inafuatia uchaguzi uliofanyika jana. Lakini siku chache katika kuelekea uchaguzi huo, Watanzania walipata wasaa wa kuagwa na Mwai Emilio Stanley Kibaki, Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Kenya aliyemaliza muda wake. Alikuja kuwaaga majirani zake Tanzania katika ziara ya siku mbili, si kwa lingine isipokuwa mahusiano mazuri ambayo yamekuwepo baina ya Tanzania na Kenya.
Mwai Kibaki aliwasili nchini mwetu Februari 20 mwaka huu, jioni na kuanza ziara ya kiserikali. Kwa heshima kubwa alizindua barabara iliyokuwa ikitambulika kama Old Bagamoyo na kupewa jina lake ambapo sasa itajulikana kama Mwai Kibaki.
Baada ya kuwasili uwanja wa ndege, alipigiwa mizinga 21 kisha akakagua gwaride la heshima na kisha akapata burudani toka katika vikundi mbalimbali, kisha akaondoka na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete, kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam.
Baadaye alifanya mazungumzo na mwenyeji wake kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano wa nchi hizo mbili pamoja na uchaguzi mkuu wa nchi yake.
Siku hiyo baadaye kulikuwa na dhifa ambayo Kibaki aliandaliwa na mwenyeji wake pale Ikulu jijini Dar es Salaam . Akizungumza mara baada ya kuwasili Kibaki, Balozi wa Kenya nchini Mutinda Mutiso, anasema ziara hiyo ya Rais Kibaki aliishaipanga mahususi kuwashukuru Watanzania kwa ushirikiano mzuri waliokuwa nao na Kenya, kabla na baada ya uongozi wake.
Anasema kwa kipindi chote ambacho Rais Kibaki amekuwa madarakani kumekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliokuwa na mafanikio makubwa. Siku ya pili ambayo jioni yake alirejea nchini Kenya ndipo Kibaki alizindua Barabara ya Mwai Kibaki katika makutano ya Morocco.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kibaki aliwashukuru Watanzania kwa heshima aliyopewa na kutaka wananchi wa Wilaya ya Kinondoni kutafuta kitu ambacho Kenya watasaidia ili kuimarisha kumbukumbu hiyo muhimu.
“Kutokana na heshima mliyonipa nami nitaenda na kukaa na wenzangu ili kuhakikisha ninaipa Tanzania heshima kama mliyonipa kwa kutafuta sehemu muhimu kama barabara za Kenya kuzipa majina ya viongozi wa Tanzania,” alisema.
Naye Meya wa Wilaya ya Kinondoni, Yusuph Mwenda, alisema barabara hiyo iliyopewa jina kwa kumbukumbu yake iko katika makazi ya viongozi wakubwa wa nchi hii, kama Baba wa Taifa Julius Nyerere na Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi. Akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa PTA uliopo katika Viwanja vya Sabasaba katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Rais Kibaki amewataka Watanzania kudumisha ushirikiano na umoja na nchi ya Kenya.
Anasema kwa sasa anastaafu na kupumzika, lakini akasema anaamini Watanzania watadumisha uhusiano baina ya nchi hizo ulioanza tangu enzi za kutafuta uhuru na kutaka uwe wa milele. Alisema anatamani kuona urafiki wa nchi hizo unaimarishwa katika nyanja zote za biashara, siasa na nyinginezo ili kuleta faida kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Pia Rais Kibaki alihamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili kwa nchi za Afrika kwani walishakubaliana kukitumia. Aliwataka wana Afrika Mashariki kujifunza Kiswahili na kutembeleana ili kupanua urafiki huku akiwataka Watanzania kutembelea na nchi nyingine na kuacha kutembea Pwani pekee “Niseme Kwaheri, tutakuwa pamoja na kuonana mara baada ya kustaafu.
Nikija kutembea ninawataka Watanzania na wana Afrika Mashariki wote kuwa pamoja na kusaidiana katika changamoto mbalimbali,” alisisitiza. Katika hafla hiyo maalumu ya Kibaki kuwaaga Watanzania, Wazee walimkabidhi zawadi mbalimbali Kibaki. Zawadi hizo zilizokabidhiwa kwa Kibaki na Mzee Abdalah Tamba ni pamoja na fimbo ya mkononi ya mti wa mninga aliyoitumia tangu akabidhiwe hadi anaondoka, msuli, pamoja na bao (ili akacheze bao akishapumzika).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Huruma Mkuchika anasema Rais Kibaki ameonesha kuithamini sana Tanzania kwani katika nchini nyingine za Afrika Mashariki alichagua kuiaga Tanzania pekee. Pia alimsifu Rais Kibaki kwa kukubali kuondoka madarakani kuheshimu Katiba ya Kenya baada ya kukaa kwa vipindi viwili mfululizo huku akiwa ametumikia serikali zote nne za Kenya na kwamba kwa mujibu wa udikteta angeweza kung’ang’ania madarakani.
Baada ya kumaliza mkutano na Wazee, Kibaki alitembelea Gereza la Ukonga na anasema amefika kuona jinsi wanavyotengeneza vifaa mbalimbali kwa nia ya kwenda kuendeleza magereza nchini mwake. Baada ya kutoka Ukonga alikwenda Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere tayari kwa safari ya kurudi nyumbani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema katika mazungumzo ya Kibaki na Rais Kikwete, Rais Kibaki aliahidi kwamba uchaguzi wa jana ungekuwa huru na kwamba hatarajii kuona vurugu kama zilizotokea mwaka 2007.
Lakini, Membe anasema Kibaki aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoingilia maamuzi ya Wakenya kwani wao ndiyo waamuzi wa mwisho na kwamba alihamasisha mazungumzo yenye tija katika kukabili tatizo la kisiasa na kiusalama nchini Somalia.
Alisema marais hao wawili pia walikubaliana katika kuhimiza katika kutafuta maeneo zaidi ya ushirikiano huku wakikubaliana kuongeza nguvu katika kupambana na ujangiri wa wanyama pori. Kabla ya kuwa Rais aliwahi Naibu Waziri wa Fedha, Mwenyekiti wa Tume ya Mipango, Waziri wa Biashara na Viwanda, na Waziri wa Fedha na Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Rais wa Pili wa Kenya, Daniel arap Moi.
Mwaka 1988 Kibaki alianza kuwa na mgongano na Rais Moi. Mwaka huo huo alivuliwa umakamu wa Rais na kupelekwa Wizara ya Afya. Mwaka 1991 Kibaki aliondoka chama cha Kanu kilichokuwa kinatawala Kenya toka uhuru na kuanzisha chama cha Democratic Party, Katika uchaguzi wa Urais wa mwaka 1991, Kibaki alikuwa wa tatu na mwaka 1997 alikuwa wa pili.
Katika uchaguzi wa 2002 Kibaki alishinda na kutangazwa kuwa Rais wa Kenya akiwa mgombea wa muungano wa vyama vingi vya upinzani vilivyoshirikiana kwa jina la “NARC”. Kibaki ameweka historia mwezi Novemba 2005 baada ya kuwa Rais wa kwanza nchini Kenya kuondoa Baraza lote la Mawaziri kufuatia kura ya maoni ambayo ilikuwa inahusu Katiba mpya ya Kenya.
Uchaguzi wa mwaka 2007, uliomrudisha Kibaki madarakani kwa kipindi cha pili ulipingwa na chama cha upinzani cha ODM na kusababisha machafuko nchini humo.
Katika uchaguzi uliofanyika jana ushindani mkubwa ulikuwa kati ya Waziri Mkuu Raila Odinga akiongoza muungano wa CORD na Uhuru Kenyatta akiongoza muungano wa Jubilee, matokeo yake yataifanya Kenya kupata Rais mpya. Hadi tunakwenda mitamboni jana, uchaguzi ulikuwa unaendelea.



