Simba, Azam presha tupu

SIMBA na Azam zinacheza fainali za michuano ya Kombe la Mapinduzi kesho, katika mechi inayotarajiwa kuwa ya vuta nikuvute kutokana na upinzani wa timu hizo zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi Kuu iliyochezwa mwishoni mwa mwaka jana, Simba ilishinda bao 1-0, hata hivyo mara kwa mara Azam huisumbua timu hiyo zinapokutana na hilo ndilo linafanya mechi ya kesho kuwa na mvuto zaidi.

Simba ilitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya hasimu wake, Yanga baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 kwenye mechi yao ya nusu fainali juzi usiku, na Azam ilifika hatua hiyo baada ya kuifunga Taifa Jang’ombe bao 1-0.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti makocha wa timu hizo kila mmoja amepania kushinda mechi hiyo na kutwaa ubingwa uliokuwa ukishikiliwa na URA ya Uganda. Kocha wa muda wa Azam, Iddi Cheche alisema walishaanza kujipanga na fainali baada tu ya kuing’oa Taifa Jang’ombe katika mechi yao ya nusu fainali.

Alisema kuwa hivi sasa kazi kubwa iliyopo mbele yake ni kuzidi kuwapa maelekezo wachezaji wake ili kuhakikisha wanashinda na kutwaa ubingwa.

“Tunajipanga kuchukuwa ubingwa tu sina kikubwa cha kuongea,” alisema.

Naye kocha msaidizi wa Simba Jackson Mayanja, amesema wana uhakika wa ubingwa wa michuano hiyo na baada ya kuitoa Yanga hakuna wa kuwazuia.

Mayanja alisema Yanga ndiyo timu waliyokuwa wakiihofia na baada ya kufanikiwa kuwatoa wana uhakika wa ubingwa huo ambao walikuwa wakiuhitaji kwa udi na uvumba.

“Najua tunacheza fainali na Azam, lakini huo ni mchezo mwepesi kwetu kwa sababu timu ambayo ilikuwa ikituumiza kichwa ni Yanga na tayari tumeshaitoa, kwenye mashindano,” alisema kocha huyo msaidizi.

Akiuzungumzia mchezo na Yanga Mayanja alisema, ulikuwa mgumu na wapinzani wao walicheza vizuri lakini anawashukuru wachezaji wake kwa kucheza kwa kujitolea na kufanikiwa kupata matokeo hayo ambayo ni mazuri kwa kila Mwanasimba.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alikubali matokeo hayo na kuwapongeza Simba kwa kutinga fainali huku akisema bahati haikuwa upande wao ndiyo sababu ya kushindwa.

Mwambusi alisema timu yake ilicheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini walishindwa kuzitumia hadi mchezo huo kumalizika kwa sare ya bila kufungana na kutolewa kwa mikwaju ya penalti.

“Hatuna cha kulaumu isipokuwa nawapongeza wachezaji wangu walicheza vizuri na kufanikiwa kuutawala mchezo kwa sehemu kubwa ingawa bahati haikuwa upande wetu na penalti ni jambo la bahati hata Simba wangeweza kukosa,”alisema Mwambusi.