Yanga hasira zote kwa Majimaji

NAHODHA wa Yanga, Haruna Niyonzima amesema kwa sasa akili yao na mawazo wameelekeza kwenye mchezo wa Ligi Kuu bara dhidi ya Majimaji utakaochezwa Januari 17 kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea.

Akizungumza na gazeti hili jana, Niyonzima alisema baada ya kuondolewa na Simba kwenye mchezo wa nusu fainali wa kombe la Mapinduzi wanajiandaa na mchezo huo wa Ligi Kuu, lengo likiwa kutetea ubingwa wao.

Yanga ilifungwa na Simba kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 kwenye mechi hiyo ya nusu fainali za Mapinduzi iliyochezwa uwanja wa Amaan Zanzibar.

“Tumekubali tumefungwa na siku zote kwenye soka matokeo ni matatu lakini kwenye mchezo wa nusu fainali matokeo yalikuwa mawili tu kushinda na kufungwa hivyo sisi tumefungwa na sasa tunajiandaa na Ligi Kuu,” alisema Niyonzima.

Pia Niyonzima alisema timu yake ilikosa bahati kwani wachezaji walicheza vizuri lakini kadri siku zilivyozidi kwenda mashindano yalibadilika na kila timu ikawa inahitaji ushindi.

Niyonzima alisema mchezo dhidi ya Majimaji FC utakuwa na ushindani kwani kila timu imejiandaa vema kuhakiksha inapata ushindi hivyo watajipanga kuhakikisha wanashinda.

“Tutacheza ugenini na kwa sasa Majimaji imebadilika hivyo tunajiandaa na kusahau yaliyopita,” alisema Niyonzima.

Yanga mabingwa watetezi wana shika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 40, pointi nne nyuma ya vinara Simba na Majimaji ina pointi 17 kwenye nafasi ya 14 huku zote zikiwa zimecheza michezo 18.