28 kucheza Kombe la FA

TIMU 28 zinatarajiwa kushuka dimbani Jumapili kwenye michuano ya Kombe la FA. Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano hiyo itaendelea tena kwa timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) kuwakaribisha Kiluvya United keshokutwa Jumamosi.

Mechi nyingine za michuano hiyo zitachezwa Jumapili, ambapo timu 28 zitashuka dimbani kwenye viwanja 14 tofauti kuwania tiketi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF.

Bingwa mtetezi wa michuano hiyo ya FA ni Yanga ambayo iliinyuka Azam mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliopigwa uwanja wa Taifa Mei mwaka jana.

Hata hivyo,Azam ndio itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF pamoja na kufungwa kwenye fainali hizo, hiyo inatokana na Yanga kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

Mechi zitakazochezwa Jumapili ni Friends Rangers itakayoikaribisha Ashanti United kwenye uwanja wa Karume huku Coastal Union ikivaana na Mgambo Shooting uwanja wa Mkwakwani. Panoni watakuwa wenyeji wa African Sports kwenye uwanja wa Ushirika Moshi, huku Alliance ikimenyana na Pamba kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Mbeya Warriors watakaomenyana na Kimondo kwenye uwanja wa Sokoine, huku Kurugenzi ikimenyana na Lipuli kwenye uwanja wa Mafinga, Polisi Mara itatifuana na Rhino (Karume Musoma), Singida United watawakaribisha Mvuvumwa uwanja wa Namfua.

Polisi Moro watakuwa wenyeji wa Polisi Dodoma (Jamhuri Morogoro), wakati Njombe Mji watamenyana na JKT Mlale kwenye uwanja wa Njombe.

Michuano hiyo itaendelea tena Jumatatu ijayo kwa timu ya Mshikamano kumenyana na Polisi Dar es Salaam kwenye uwanja wa Karume.

Michuano hiyo, imedhamini na Kampuni ya Azam Media kwa Mkataba wa miaka minne wenye kitita cha Sh bilioni 3.3.

Bingwa atajinyakulia kitita cha Sh milioni 50 wakati kila timu itakayokwenda kucheza ugenini itapata Sh milioni 3 za safari na mwenyeji anapatiwa Sh milioni moja za maandalizi.