Royal mabingwa halali Arusha

TIMU ya Royal FC imetangazwa rasmi kuwa mabingwa halali wa ligi soka daraja la nne ngazi ya wilaya Arusha.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Chama cha Soka Wilaya ya Arusha baada ya Kamati ya Rufaa kupitia malalamiko yaliyotolewa na timu ya Polisi Moran.

Awali, timu ya Polisi Moran iliyoshiriki Ligi Daraja la Tatu ngazi ya Wilaya ya Arusha iliikatia rufaa timu ya Royal FC kwa madai ya kushiriki ligi bila ya kuwa na usajili pia kumchezesha mchezaji Erick Omond kwa madai kuwa si raia wa Tanzania.

Akitangaza ubingwa halali wa timu ya Royal Katibu msaidizi wa Chama cha Soka Wilaya ya Arusha (ADFA), Athumani Juma alisema baada ya timu ya polisi kukata rufaa kamati husika ndio ilikuwa na mamlaka ya kufuatilia na kutoa maamuzi.

“Kama ADFA tunatambua Royal ndio mabingwa halali baada ya Kamati ya Rufaa kutolea maamuzi yaliyolalamikiwa, ambapo ilibaini kuwa timu ya Royal ilisajiliwa rasmi kisheria kwa msajili wa vyama vya michezo Novemba 15, 2016 kwa namba 16619,” alisema Juma.

Alieleza kuwa kamati hiyo ilitolea ufafanuzi suala la mchezaji Erick Omond aliyelalamikiwa kuwa sio raia na kusema kuwa mchezaji huyo sio mali ya timu ya Royal bali yuko timu hiyo kwa mkopo akitokea timu ya Kaloleni na suala la mchezaji si raia ni la idara husika sio ADFA.

“Maamuzi ya kamati ni kuwa mchezaji huyo anauhalali wa kucheza Royal na suala la rufaa ingekatiwa timu ya Kaloleni,”alieleza Juma.

Naye Katibu Mkuu wa timu ya Royal FC Obedi Mollel alisema ukweli umebainika kuwa ubingwa wetu ni wa halali baada ya maamuzi kutolewa.

“Tunashukuru ADFA, pia Kamati ya Rufaa na timu ya polisi kukata rufaa kwani imesaidia kuondoa sintofahamu iliyoibuka kwani kila kitu kimeonekana wazi bila upendeleo,” alisema Mollel.

Mollel alisema siku zote mpira unachezwa uwanjani na si kwingine timu yake ilionesha ushindani wa aina yake na ilishinda michezo yote ya hatua ya fainali ya tano bora ambapo ilimaliza ligi ikiwa na pointi 12 huku wapinzani wao Polisi Moran pointi 9.

Timu zilizoingia hatua ya tano bora ni Royal FC, Old Boys, Sorenyi FC na New Vision, Polisi Moran.

Ligi soka wilaya Arusha ilianza kutimua vumbi Septemba mwaka jana ikishirikisha timu 13 ambazo ni Polisi Moran, NMC Marker, Dogo Sam, Royal Fc, Njiro, Old boys, Morombo, New Vision, Moshono,Tanzanite, Zamzam, Sorenyi na Jamhuri zilichuana vikali ambapo timu tano zilifuzu kucheza hatua ya fainali.