21Mei2013

 

Suala la Yondani latua Polisi

SUALA la beki Kelvin Yondani kudai kuchukuliwa bila ridhaa yake na kupelekwa kwa kigogo mmoja wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, sasa limeripotiwa Polisi.

Polisi Mkoa wa Temeke ilisema jana kuwa imepokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa klabu ya Yanga, waliodai kutaka kutekwa kwa mchezaji wao Yondani na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni Simba.

Akizungumza na gazeti hili Kamanda wa Mkoa huo, David Misime, alisema viongozi hao juzi usiku walifika kituo cha Polisi Kilwa Road, wakiwa na lengo la kutaka kufungua kesi ya utekaji huo.

Misime bila kuwataja viongozi hao, alisema mara baada ya kufika kituoni hapo na kukutana na maofisa wa polisi waliokuwepo zamu walianza kutoa maelezo juu ya mkasa mzima wa suala hilo.

“Walifika wakiwa na mchezaji huyo (Yondani) na kutaka kufungua kesi ya utekaji nyara, lakini kwa taratibu zetu kwa kuwa mtu wanayedai alitaka kutekwa waliongozana naye, tulimtaka yeye mwenyewe aeleze namna tukio lilivyokuwa, ” alisema Misime.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo mara baada ya kumsikiliza na mazungumzo hayo kwa ujumla, viongozi hao wa Yanga waliondoka na Yondani na kuliacha suala hilo likiendelea kufanyiwa kazi.

Awali akizungumza na Mwandishi Wetu Dar es Salaam juzi usiku, muda mfupi baada ya kutoka Polisi, Yondani alisema alishauriana na viongozi wa Yanga baada ya tukio lake la kuchukuliwa bila ridhaa, kwamba njia sahihi ni kulifikisha jambo hilo polisi.

“Tumejadiliana na viongozi wa Yanga tukaona tukatoe taarifa polisi, hilo tumelifanya,“ alisema Yondani kauli iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Ahmed Seif ‘Magari’ ambaye alimsindikiza Polisi.

Jana gazeti la michezo litokalo kila Jumatatu la Spoti Leo, ambalo ni gazeti dada na hili, lilimkariri Yondani akisema alifuatwa nyumbani kwake Mbagala, Dar es Salaam juzi jioni na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe ambaye wanaheshimiana kwa kiasi kikubwa.

Alisema Mwakingwe aliondoka naye wakaelekea maeneo ya Kurasini, wakiwa katika matembezi ya kawaida na hakuwa na wasiwasi, lakini walipofika eneo hilo la Kurasini alishangaa kupelekwa ofisi za mmoja kati ya viongozi wa Simba na alipouliza kulikoni akaambiwa asiwe na wasiwasi.

Alisema alishangaa kuletewa karatasi na kuambiwa asaini na akane kwamba si mchezaji wa Yanga, huku akiahidiwa fedha na gari, hali iliyompa hofu kuona anaweza kuharibiwa maisha yake, hivyo kumjulisha Magari na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Francis Kifukwe, ambao haraka walianza harakati za kuhakikisha wanadhibiti tukio hilo.

Naye Kifukwe akizungumza jana alithibitisha kupeleka malalamiko polisi na si kufungua kesi kwa maelezo kuwa hawana haja ya kufungua kesi ila waliona ni vyema tukio hilo likafahamika kwa vyombo vya dola.

Lakini Mwakingwe amekana kutumika kutaka kumrubuni Yondani na kusema kuwa hafahamu taarifa hizo zinatokea wapi na kueleza kuwa soka la Tanzania sasa linaelekea pabaya kama ikitokea wachezaji wa Simba na Yanga kushindwa kutembeleana, huku pia akisema kwa sasa yeye si mchezaji wa Simba, hivyo hawezi kutumika kwa namna yoyote ile.

Pia Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga naye jana alikaririwa na Spoti Leo akisema Simba haiwezi kumtuma Mwakingwe kwa jambo lolote na haina sababu ya kumchukua kwa njia hiyo Yondani na kutaka Simba isihusishwe kwa jambo hilo.

Kauli kama hiyo pia ilizungumzwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Pope aliyekaririwa na mtandao wa bongostaz.com akisema Simba haiwezi kumteka Yondani maana ni mchezaji wao na wana mkataba naye na kama kuna mtu amefanya hivyo huyo hajui atendalo na hajapewa baraka na uongozi.

Yondani alikuwa na mgogoro na Simba aliyochezea msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo klabu hiyo imemuwekea pingamizi katika usajili wake wa Yanga kwa madai bado ina mkataba naye uliosainiwa Desemba mwaka jana.

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilitarajiwa kukutana jana kutoa uamuzi wa masuala mbalimbali ikiwemo pingamizi la Simba kwa usajili huo, ambapo hadi tunaenda mitamboni kikao hicho kilikuwa bado kinaendelea.