‘Watanzania mshukuruni Mungu kwa Rais bora’

WATANZANIA wameaswa kumshukuru Mungu kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa amani na utulivu, jambo lililowezesha kupata rais bora anayejali wanyonge na kusimamia kwa moyo rasilimali za nchi.

Mwito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu wa Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea, Padri Camilius Haule katika Misa Takatifu ya shukrani ya Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Leonidas Gama. Ibada hiyo iliandaliwa na waumini wa kanisa hilo katika Parokia ya Peramiho, Jimbo Kuu la Songea.

Padri Haule alisema, ni Mungu pekee ndiye aliyependa Watanzania kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kuwa salama kwani yapo mataifa mbalimbali ulimwenguni yaliyoshindwa kufanya uchaguzi.

“Watanzania lazima tusema Mungu asante kwa zawadi kubwa ya kufanikisha uchaguzi wa mwaka huu kwa amani na nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani, upendo na utulivu hata kwa watu wa mataifa mengine duniani,” alisema Padri Haule.

Alisema, uchaguzi umeshapita na viongozi wameshapatikana kwa hiyo hakuna sababu ya kuendeleza kinyongo kwani suala la uongozi anayemchagua kiongozi ni Mungu mwenyewe hivyo watu hawapaswi kukimbilia kutafuta uongozi kwa nguvu na kutumia fedha nyingi.

Aidha, alimpongeza Dk John Magufuli kwa ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi huo na pia mbunge wa Songea, Gama na kusema ni kielelezo kizuri cha wananchi wa jimbo la Songea, kwani ni kiongozi wa wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa, kidini na kikabila.

Alisema, kuchaguliwa kwake kumetokana na upendo mkubwa wa watu wa Songea, kwa hiyo amemtaka kuhakikisha anatekeleza ahadi zote alizotoa wakati akiomba kura ili kujijengea heshima na imani kwa wananchi wa jimbo lake.

Pia amewataka viongozi wote waliochaguliwa kuanzia madiwani, wabunge na Rais kuwa na hofu ya Mungu kwa kuwapenda wananchi bila kujali tofauti ya kipato, siasa, dini na ukanda. Kwa upande wake, Gama amewataka wananchi wa Songea kumpa ushirikiano katika kutekeleza mipango ya maendeleo na kila mara kumtanguliza Mungu ili waweze kufanikiwa katika malengo yao.

Alisema mchakato wa uchaguzi wa ubunge kwake ulikabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo baadhi ya watu walio mshawishi kwenda kwa waganga wa jadi kutambika, jambo ambalo hakukubaliana nalo kwa sababu kila siku imani yake ni Mungu.