Awamu ya 4 yaongoza fursa za elimu

SHIRIKA la Elimu la Hakielimu limezindua ripoti ya miaka 10 ya Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, iliyobainisha kuwa ni awamu iliyofanya vizuri katika kupanua fursa za elimu kwa watoto wengi wa Kitanzania.

Katika kipindi cha miaka 10, kumekuwa na upanuzi mkubwa wa miundombinu ya vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, ongezeko la idadi ya walimu, vitabu, udahili na kuimarika kwa uwiano wa wasichana na wavulana, wanaojiunga na kuhitimu elimu ya msingi na sekondari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hakielimu, John Kalage alisema hayo jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, ambayo imeainisha changamoto ambazo bado zinaikabili sekta ya elimu hapa nchini na kupendekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa ili kufikia elimu bora yenye usawa na haki.

“Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais mstaafu Kikwete imefanya vizuri katika kupanua fursa za elimu kwa watoto wengi wa Kitanzania ,” alisema Kalage na kuongeza kuwa shule za msingi zimeongezeka kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015.

Alisema kwa kipindi cha miaka 10 hiyo, wanafunzi wa shule ya msingi waliongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892, huku shule za sekondari zimeongezeka kutoka 1,745 mwaka 2005 hadi 4,753 mwaka 2015. Kwa upande wa wanafunzi shule za sekondari, alisema wameongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,804,056 mwaka 2015.

Kalage alisema vyuo vya ufundi pia vimeongezeka kutoka 184 mwaka 2005 hadi 744 mwaka 2015, huku wanafunzi katika vyuo hivyo wakiongezeka kutoka 40,059 hadi 145,511 mwaka 2015.

Katika kipindi hicho, pia bajeti ya sekta ya elimu ilikuwa kubwa kuliko sekta nyingine yoyote, ikiongezeka kutoa Sh bilioni 669.5 mwaka 2005/2006 hadi Sh trilioni 3.4 mwaka 2014/2015.

Alisema upanuzi huo umewezesha asilimia 98 ya watoto wanaostahili kupata elimu ya msingi kuandikishwa, kiwango cha udahili kwa shule za msingi kuongezeka kwa zaidi ya asilimia 26, huku kikiwa kiwango kikubwa zaidi kwa sekondari na elimu ya juu kwa asilimia 244 na 438.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mtafiti Profesa Kitila Mkumbo alipongeza awamu ya nne ya uongozi kwa kufanya vizuri katika elimu, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vyuo vikuu nchini.

“Rais Kikwete amefanya yake mazuri kwa kipindi cha uongozi wake… wakati anaingia madarakani Watanzania waliokuwa na elimu kiwango cha shahada ya kwanza walikuwa asilimia moja, lakini ameondoka na kuacha asilimia 2 hadi 3,” alisema Profesa Mkumbo na kuongeza kuwa jambo la muhimu ni kuangaliwa falsafa ya nchi kuhusu elimu.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Elimu, Dk Joviter Katabaro alisema falsafa ya nchi kuhusu elimu, inatakiwa kusema wanaosoma ni kwa ajili ya nini ili kusiwepo watakaoachwa nyuma.

Alisema Rais Kikwete alifanya yake, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ujenzi wa maabara katika kila shule na kinachosubiriwa kwa sasa ni vifaa gani vitakavyoingizwa, ili kuziwezesha kufanya kazi kwa umakini na kwa manufaa.

Pamoja na mafanikio hayo, ripoti hiyo imefafanua kuwa kiwango cha ubora wa elimu, kilishuka kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania Bara.