Malumbano ya kisheria yatawala kesi ya Mwale

MALUMBANO ya kisheria yameibuka jana baina ya mawakili upande wa Serikali na utetezi katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili washtakiwa wanne akiwemo wakili maarufu wa jijini Arusha, Median Mwale hali iliyosababisha Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kuendesha kesi ndani ya kesi.

Hayo yaliibuka mbele ya Jaji Gadi Mjemas anayesikiliza shauri hilo namba 61/2015 mara baada ya shahidi wa kwanza kwa upande wa serikali, Fadhili Mdemo kueleza mahakama kuwa aliandika maelezo ya mshtakiwa wa nne, Elias Ndejembi na mshtakiwa wa pili Don Bosco.

Baada ya shahidi huyo kuyasema hayo wakili wa utetezi, Albert Msando alikataa kupokelewa mahakamani hapo maelezo ya mshtakiwa wa nne, Ndejembi kwa kile alichodai kuwa maelezo hayo yanaonesha kuwa alihojiwa saa 9:18 alasiri lakini hayaonyeshi alikamatwa na kushikiliwa na Polisi kuanzia muda gani.

Msando aliendelea kusema kuwa maelezo hayo yana upungufu wa kisheria kwani hayajaambatanishwa na fomu ya uthibitisho (certification form) kuonesha mshtakiwa alisoma na kuridhia kuwa yale ni maelezo yake.

Alisema inaonesha mshtakiwa alipigiwa simu saa mbili asubuhi lakini haelezi alikuwa chini ya ulinzi wa Polisi kuanzia saa ngapi na muda gani ulipita kabla hajahojiwa kwa wakili. Baada ya malumbano hayo ya pingamizi ya maelezo ya mshtakiwa kukubaliwa kama kielelezo au la Jaji Mjemas anayesikiliza shauri hilo aliamua suala hilo kusikilizwa kwenye kesi ndani ya kesi ambapo upande wa serikali uliahidi kuleta mahakamani hapo mashahidi watatu huku upande wa utetezi ukiahidi kuleta mashahidi wawili.

Mawakili wengine wa utetezi kwa pamoja walipinga kupokelewa kwa maelezo hayo huku wakitoa hoja mbalimbali za kisheria. Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Moses Mahuna alipinga kupokelewa kwa maelezo hayo kwa kile alichoeleza mahakamani hapo kuwa yaliandikwa bila kuonesha kifungu cha sheria kilichokiukwa na mshtakiwa. Alisema kutoandikwa kwa kifungu cha sheria kilichokiukwa kunamfanya mtuhumiwa ashindwe kuelewa mtiririko mzima wa maelezo ya onyo.

Hoja hiyo ya utetezi pia iliungwa mkono na wakili, Innocent Mwangi ambaye alipinga vikali kupokelewa kwa maelezo hayo huku akinukuu vipengele mbalimbali vya sheria za uendeshaji mashauri ya jinai (CPA) na maamuzi mbalimbali yaliyowahi kutolewa na mahakama za juu nchini vinavyopinga ofisa upelelezi kuandika maelezo ya watuhumiwa wawili kwenye shauri moja. Washtakiwa hao wanne wanakabiliwa na mashtaka 44 yakiwemo ya kula njama kutenda kosa, utakasaji fedha haramu na kughushi ambapo kwa sasa linasikilizwa mfululizo.