Yanga, Simba kucheza usiku
- Imeandikwa tarehe 22 Septemba 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 658
MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga uliopangwa kufanyika Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa utafanyika usiku.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa mechi tano za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ambazo zitaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport zitaanza kati ya saa 11:30 jioni na saa moja kamili usiku.
“Septemba 28 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili usiku. Mechi ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Septemba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itaanza saa 11 kamili jioni.
“Yanga na African Lyon zenyewe zitapambana Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni wakati Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar zitaoneshana kazi Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
“Mechi ya mwisho katika Super Weekend itakuwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ikiwakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba na itaanza kutimua vumbi saa 1 kamili usiku,” alisema Wambura.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo, ambapo Yanga iliyoanza kwa kusuasua inajitupa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kucheza na JKT Ruvu katika raundi ya tatu ya ligi hiyo.
Timu zote mbili zitaingia uwanjani zikiwa na kumbukumbu mbaya ya mechi zao zilizopita Jumatano, ambapo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri Morogoro, huku JKT Ruvu ikioneshwa kazi na Simba kwa kufungwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa.
Tofauti na JKT Ruvu ambayo mchezo wake wa kwanza iliifunga Ruvu Shooting ambayo kesho inacheza na Simba mabao 2-1, hivyo kuwa na pointi tatu kibindoni, Yanga katika mchezo wake wa kwanza ilitoka 0-0 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya hivyo kuwa na pointi moja na haijafunga bao.
Mazingira hayo yanaufanya mchezo wa leo kuwa wa ushindani mkubwa huku kila timu ikitaka kushinda ili ijiweke kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi.
Ni wazi Yanga inayofundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet haitakubali kupoteza mchezo huo, huku pia JKT Ruvu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nayo ikitaka kuwaonesha Yanga kwamba inaweza hasa kwa vile inaundwa na wachezaji wazoefu akiwemo Credo Mwaipopo na Omary Changa ambao wamewahi kuchezea Yanga.
Pia safu ya ulinzi ya JKT chini ya George Minja, Stanley Nkomola na Kessy Mapande haitakubali kuwaachia kirahisi washambuliaji wa Yanga wakiongozwa na Said Bahanunzi, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbagu wamuone kipa wao kirahisi.
JKT Ruvu inafundishwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Charles Kilinda. Wakati huohuo, Kocha wa Yanga,Tom Saintfiet amemuondoa mshambuliaji mahiri Saidi Bahanunzi kwenye kikosi kitakachoivaa JKT Ruvu kutokana na kukabiliwa na maumivu ya vidole vya mguu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kocha huyo alisema pia katika kikosi hicho hatakuwepo chipukizi Frank Domayo na David Luhende.
Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya Azam itakayoikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Azam Complex mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali, ambapo mara nyingi timu hizo zinapokutana huwa hautabiriki.
Azam Jumatano ilifungana mabao 2-2 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wakati Mtibwa Sugar iliifunga Yanga, timu zote hizo zina pointi nne katika msimamo wa ligi zikiwa zimeshinda mechi moja na kutoka sare moja.
Mechi nyingine leo itakuwa kati ya JKT Oljoro itakayokuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kuikabili Polisi Morogoro.
JKT Oljoro mchezo wake wa Jumatano ilitoka 0-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, hivyo kuwa na pointi mbili baada ya mchezo wake wa kwanza kutoka 1-1 na Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba.
Polisi Morogoro yenyewe mchezo uliopita ilifungwa na African Lyon bao 1-0, wakati mchezo wake wa kwanza ilitoka 0-0 na Mtibwa Sugar hivyo kuwa na pointi moja.
Kivumbi kingine leo kitakuwa Uwanja wa Mkwakwani Tanga, ambapo wenyeji Coastal Union wataikaribisha Toto Africans ya Mwanza. Coastal mchezo wake wa kwanza iliifunga Mgambo Shooting mabao 2-1, kisha ikatoka 1-1 na Prisons Jumatano, hivyo nayo kuwa na pointi nne kibindoni.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho wakati vinara Simba yenye pointi sita baada ya kushinda mechi zake zote mbili ilizocheza, itakapovaana na Ruvu Shooting yenye pointi tatu baada ya kushinda mechi moja na kupoteza moja.
Mechi nyingine kesho ni Mgambo JKT dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, huku African Lyon ikiikaribisha Prisons Uwanja wa Azam Complex.



