Panone yaitangazia maumivu Azam

TIMU ya soka ya Panone FC iliyoshiriki Ligi Daraja la Kwanza imesema itahakikisha inaifunga Azam FC katika mchezo wake wa Kombe la FA hatua ya 16 bora Jumatatu Uwanja wa Ushirikia mjini Moshi.

Panone FC inayonolewa na Felix Minziro, haikufanya vizuri katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL), lakini ipo nafasi nzuri katika michuano ya Kombe la FA ambayo bingwa atawakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf) mwakani.

Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Habari, Cassim Mwinyi, alisema timu yake ipo katika maandalizi ya mwisho kuwakabili wapinzani wao ili waweze kuwaondoa katika michuano hiyo.

“Tumejipanga vilivyo kuhakikisha tunawafunga Azam, kwani maandalizi ambayo tunayo itadhihirisha mtanange huo utakaokuwa na ushindani wa aina yake pia kwa taarifa ya mwalimu timu yetu ipo vizuri na hakuna majeruhi yeyote,” alisema Mwinyi.

Alisema Azam ni timu nzuri, lakini watahakikisha wanafanya mabadiliko kwa kuwaondoa vibonde hao katika mashindano hayo licha ya timu yake kufanya vibaya katika ligi daraja la kwanza.