Simba SC kimenuka
- Imeandikwa tarehe 05 Machi 2013
- By Dennis Fussi, Luanda
- Imesomwa mara: 1079
WAKATI Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig akiwalaumu wachezaji wake kwamba walicheza chini ya kiwango dhidi ya Recreativo de Libolo na kukung’utwa mabao 4-0 juzi, mwanachama wa Simba amemgeuzia kibao na kutaka Kamati ya Utendaji imfute kazi.
Mbali na pendekezo la kumfuta kazi kocha huyo Mfaransa, baadhi ya mashabiki walioshuhudia mechi hiyo juzi kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo nchini Angola, wametaka timu hiyo ifumuliwe.
Wametoa maoni hayo baada ya Simba kukubali kipigo cha aibu cha mabao 4-0 kutoka kwa Libolo na kutolewa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika raundi ya awali, kwa jumla ya mabao 5-0 baada ya kufungwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam, Februari 17, mwaka huu.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu Liewig aliwalaumu wachezaji akisema walicheza chini ya kiwango na pia wamecheza kama wachezaji wasio na uwezo.
Kwa upande wao, Watanzania wanaoishi nchini Angola katika miji ya Luanda na Calulo, wameutaka uongozi wa Simba kuivunja timu kwa sababu inaonesha wazi haina kiwango na inahitaji wachezaji wapya.
Wakiongozwa na Balozi Mdogo wa Tanzania nchini Angola, Mbwana Mziray, alisema Simba ya juzi siyo ile anaiyoijua kwa sababu ilicheza kichovu.
Mwanachama maarufu wa Simba ambaye amefuatana na timu hapa, Majaliwa Mbasa ameutaka uongozi kuachana na kocha huyo kwani ameonesha hana uwezo.
Simba ambayo pia mwenendo wake katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ni wa kusuasua ikiwa ni ya tatu ikiachwa pointi 11 na watani wao wa jadi Yanga, inatarajiwa kurejea nchini leo.
Iliondoka katika Mji wa Calulo jana asubuhi kwa basi kwenda Luanda, umbali wa kilometa 300 na leo inatarajiwa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kurejea Dar es Salaam kupitia Nairobi.



