25Mei2013

 

Azam yarejea, yapelekwa Liberia

TIMU ya Azam FC iliwasili nchini jana mchana kutoka Juba nchini Sudan Kusini ambako juzi ilifuzu kwa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo itacheza na Barrack Young Controllers ya Liberia.

Akizungumza baada ya timu hiyo kurejea Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Iddi alisema kwa sasa wanasubiri ratiba ya mwalimu ya kueleza mikakati yake ya kujiandaa na mechi hiyo.

Iddi alisema wachezaji kwa sasa wanajipanga na kuendelea na mechi za Ligi Kuu, na jana walipewa mapumziko kabla ya kurejea leo kambini.

Azam FC juzi iliikung’uta Al Nasir kwa mabao 5-0 na kufuzu raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 8-1 baada ya kushinda mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, wa mabao 3-1.

Kwa kuitoa Al Nasir Juba, Azam sasa itacheza raundi ya kwanza ya michuano dhidi ya Barrack Young Controllers ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone.

Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha sare ya kutofungana juzi jijini Freetown. Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15, 16 na 17, mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5, 6 na 7, mwaka huu.

Ofisa Habari wa Azam alisema wakati wakiwa Juba, wachezaji walipata bahati ya kukutana na mchezaji wa zamani wa Ureno, Luis Figo ambaye alikwenda nchini humo kufuatilia mradi wa soka wa watoto.

Alisema kitendo hicho kiliongeza morali kwa wachezaji ambao wanaona kuwa hiyo ilikuwa ni kama bahati kwao kukutana na gwiji huyo wa kimataifa.

“Najua hizi ndio nafasi ambazo kama mchezaji wa timu kama yetu hii akimuona mchezaji wa kimataifa kama huyu na pengine alikuwa na ndoto ya kuwa kama yeye, basi inakuwa ni faraja kwao,” alisema Iddi.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa pongezi kwa Azam kwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

“Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika,” ilisema taarifa ya Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.

“Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata,” iliongeza taarifa hiyo.