18Mei2013

 

JKT Oljoro yahitaji pointi sita iwe salama

TIMU ya soka ya JKT Oljoro mkoani Arusha, imesema inahitaji kutia kibindoni pointi sita kuanzia sasa ambazo zitawahakikishia kubaki na kuendelea kushiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika msimu ujao.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema hayo mwishoni mwa wiki mjini hapa baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.

Mchezo huo pia ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.

Timu hiyo ambayo hadi mchezo wao dhidi ya Polisi Morogoro ilikuwa imefikisha pointi 22 na Kocha Msaidizi huyo alisema hivi sasa mkakati wao ni kuhakikisha wanashinda michezo miwili ama zaidi kwa lengo la kufikisha pointi 28 zitakazowawezesha kubakia Ligi Kuu.

“Ligi bado ni ngumu hasa katika kipindi hiki cha lala salama, na sisi lengo letu ni kufikisha zaidi ya pointi 28 zitakazotuweka salama na harakati hizi tunazianzia na timu ya Prisons ya Mbeya kwenye uwanja wetu wa nyumbani mwishoni mwa wiki hii,” alisema Elias.

Akizungumzia mchezo wao dhidi ya Polisi Morogoro, Kocha Msaidizi huyo alisema vijana wake walicheza kwa tahadhari na kujihami zaidi wakihitaji matokeo ya sare kutokana na kucheza uwanja wa ugenini.

Naye Kocha Mkuu wa Polisi, Mohamed ‘Adolf’ Richard alisisitiza kuwa matumaini ya kubaki Ligi Kuu yapo mikononi mwa kila mmoja wao katika timu hiyo, viongozi na wapenzi wa soka wa Mkoa wa Morogoro.

“Tunasubiri miujiza, lakini tunaweza kubakia Ligi Kuu, na hii itatokana na matokeo ya michezo ya timu pinzani zipo kwenye mlolongo wa kushuka daraja, lakini sisi Polisi bado tuna wakati mgumu sana,” alisema Adolf ambaye timu yake tangu kuanza duru la pili, haijapoteza mchezo na imefikisha pointi 16.