Mashindano ya baiskeli Mbeya yafufuliwa
- Imeandikwa tarehe 05 Machi 2013
- By Joachim Nyambo, Mbeya
- Imesomwa mara: 163
BAADA ya kusuasua kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, hatimaye mashindano ya mbio za baiskeli jijini Mbeya yamefanyika mwishoni mwa wiki jana.
Katika mashindano hayo ya kilometa 140, Mashaka Jonas aliibuka bingwa baada ya kutumia saa tatu na dakika 47 akiwaacha nyuma washiriki wengine 15.
Mshindi wa pili alikuwa Kiang Samson aliyetumia saa tatu na dakika 59 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Jailos John aliyetumia muda wa saa nne na dakika 11 kumaliza kilometa hizo.
Mshindi wa kwanza wa mbio hizo zilizoandaliwa na Kampuni ya Range of Vision Marketing Limited (RVMCL) ya jijini Mbeya, alizawadiwa 150,000, mshindi wa pili Sh 100,000 na wa tatu Sh 50,000.
Akikabidhi zawadi hizo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Vincent Msolla kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro alisema mbio za baiskeli ni miongoni mwa michezo inayotambuliwa na Serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wanaoandaa mashindano hayo.
Msolla alisema jamii inapaswa kutambua umuhimu wa michezo na kusisitiza kufufuliwa kwa michezo mbalimbali ambayo kwa sasa inaonekana kutochezwa ili kutoa fursa kwa vijana kushiriki kwa kila mmoja na kipaji chake.
“Pamoja na kuwa michezo kwa sasa ni ajira, tunapaswa pia kutambua kuwa michezo pia inatukutanisha na marafiki wapya wenye kutuma mawazo zaidi ya yale tuliyokuwa nayo awali,” alisema Msolla.


